Sanamu la Senegal la mwamko mpya Afrika | Masuala ya Jamii | DW | 23.02.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Sanamu la Senegal la mwamko mpya Afrika

Wengi walalamika , wasema fedha hizo zingetumiwa kwa maslahi ya jamii.

Sanamu la mwamko wa Mwafrika mjini Dakar-Senegal

Sanamu la mwamko wa Mwafrika mjini Dakar-Senegal

Sanamu lililojengwa katikati mwa mji mkuu wa Senegal-Dakar, limezusha hisia tofauti miongoni mwa  wakaazi awa nchi hiyo.

Lina uzito wa mamia ya tani, limetengenezwa kwa kiasi kikubwa kwa shaba na saruji. Ni kubwa kuliko sanamu la Uhuru la Marekani, statue of Liberty, na liligharimu zaidi ya Euro millioni 20. Kupitia sanamu hili linaloitwa, " kipindi cha mwamko mpya wa Afrika“ Rais Wade alitaka kujiwekea kumbukumbu yake wakati angali anaishi.

Lakini hali ya ujenzi wa sanamu hili imejaa ufisadi na juhudi za kufumba watu macho, na sanamu lenyewe ambalo ni kubwa ajabu pia limeleta utata baina ya Wasenegali.

Baba, mama, mwana – pàpp, yaay, doom – hivyo ndivyo waliitavyo kwa kejeli wasenegali sanamu lenye urefu wa mita 52 ambalo tangu mwaka 2010 linalipamba wingu la mji mkuu wa Senegal.

Kuna sura iliojitokeza kwamba jamii ya kiafrika inawania kuwa  kama ya Kimagharibi. Uvumi unasema kuwa kupitia  sanamu hilo Rais Wade anajiwakilisha yeye mwenyewe, mkewe na mwanawe Karim. Rais Wade mwenyewe anaeleza kwamba, sanamu hili linaashiria kipindi cha mwamko mpya wa Afrika na linawarudishia wanasenegali na waafrika wote kwa jumla utambulisho walioupoteza kupitia ukoloni na kutawaliwa na wageni.

Karibu miaka mwili sasa sanamu hili kubwa la mwamko mpya limesimama katika ncha ya magharibi ya bara la Afrika. Lakini mjadala kuhusu urembo wake, umuhimu wake au ukosefu wa umuhimu  bado unaendelea. Na hata uvumi na hutuma za ufisadi kuhusu kutengenezwa kwake bado zinaendelea kwani kuna masuala yenye utata kuhusu umiliki wa kiwanja liliposimamishwa sanamu hilo.

Werner Nowak, mkuu wa wakfu wa Friedrich-Neumann huko Dakar amejishuhulisha na mada hii. Anasema kuwa, "Sanamu hili „monument de la renaissance africane“ kwa kifaransa, ni aina ya mfano wa  jinsi mali ya umma inavyohamishwa kwa mikono binafsi na jinsi vile fedha nyingi hutumika kwa miradi ambayo haina faida yoyote kwa umma."

Mfanya biashara fulani aliagizwa na Rais wa Senegal kulijenga sanamu hilo. Thamani yake inakadiriwa kuwa zaidi ya Euro millioni 20. Kwa ajili hii mfanya biashara huyo alipatiwa kiwanja katikati mwa mji mkuu, ambacho thamani yake ni takriban mara sita zaidi ya thamani asilia .

Rais Abdoulaye Wade

Rais Abdoulaye Wade

El Hadj Ahmadou Sall, msemaji wa Rais Abdoulaye Wade anakanusha wajibu wowote wa mkuu wa nchi katika suala hili. Zaidi yake, msemaji huyu hakuzungumzia kuhusu madai kwamba Wade anapokea 35% ya mapato kutokana na uuzaji wa tiketi katika duka liliko karibu.

El Hadj Salla anasema, "ikiwa serikali inauza kitu, ni lazima basi ifahamu kuhusu bei hiyo iliyoiweka yenyewe. Katika biashara huru hata hivyo kuna ati ati."

Hii ni kusema ni biashara nzuri kwa ujenzi  wa  mali  isiyohamishika wakati  sanamu hilo likiwa halipendwi kabisa na raia.

Raia mmoja, mwanamke  mkaazi wa Dakar anasema kwamba „kwangu mimi huu ni mradi mbaya. Wade amepoteza mabilioni ya fedha na sanamu yenyewe hata haipendezi. Mtu haelewi ina maana gani au itatufaidisha vipi katika siku za usoni?”

Mwanamme mmoja mjini humo naye  alisikika akisema,

“ni dhahiri fedha zimepotezwa hovyo. Gharama hizo zingeweza kutumiwa kujenga hospitali au viwanda viwili au vitatu au pia kuwajengea nyumba watu walio na shida na kulazimika kuishi kwenye maeneo ya madongo poromoka."

Mgombea mmoja wa  kiti cha urais alitangaza Februari 26 katika mahojiano na Deutsche Welle kuwa kuna uwezekano  wa kubomolewa kwa sanamu hilo pale Wade atakaposhindwa katika uchaguzi na kuondoka madarakani.

Hata hivyo kwa upande mwengine, wafanyi biashara na wapiga picha katika eneo linalozunguka sanamu hili wameridhika sana.Wanasema, "sanamu hili linanipendeza, ni nzuri sana. Tunajivunia sana. Kitambo palikuweko na watu wengi sana ambao hawakuwa wanajua Senegal iko upande gani - shukrani kwa sanamu hili sasa wanajua. Na kutokana na mapato, sote tunafaidika. Kunakuja watalii wengi hapa," na akauliza, "hukuona kitambo hivi punde  basi lililojaa watalii?”

Pamoja na hayo wakosoaji hawakubaliana na hayo.  Mwandishi wa makala haya anasema yeye hakumuona  mtalii yeyote zaidi ya watano tu waliokuwepo siku hiyo. Ni  Watu  hao watano tu ndiyo waliokuwa wakitembezwa  hadi ncha ya sanamu hilo yenye urefu wa mita 52.

Wala hakukuwa na dalili yoyote ya basi lililojaa watalii.

Mwandishi: Köpp Dirke

Mtafsiri: Susan Kiungu

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com