Sanaa ya Uganda yapata muelekeo mpya
Soko la sanaa ya Uganda ni dogo, kwani wasanii hutoa kazi zinazopendwa na kununuliwa na watalii tu. Hili halitowi nafasi ya ubunifu. Kitabu cha Kumbukumbu ya Sanaa ya Uganda 2014 huenda kikabadili hayo.
Mwaka 2014 wenye rangi kibao
Muelekeo mpya kwa sanaa ya Uganda. Wasanii 52 wakubwa wanaonyesha kazi zao kwa pamoja katika karatasi za kiwango cha juu kwenye muundo wa kitabu cha kumbukumbu. Kila wiki kazi mpya na msanii mpya hutambulishwa. Wapenzi wa sanaa pia watakuta anwani za maduka na masoko ya kazi za sanaa kwenye mji mkuu wa Uganda, Kampala. Picha hii inaitwa "Matumaini" na ilibuniwa na Ronald Ro Kerango.
Wazo jipya kutoka Kenya
Kitabu hiki cha kumbukumbu kiliandaliwa na kufadhiliwa na mjasiriamali wa Kiingereza na mkaazi wa muda mrefu nchini Uganda, Sam Rich. Wazo la mradi huu lilitoka nchi jirani ya Kenya. Picha hii ya Mark Kassi Byamugisha inaitwa "Muda wa Mapumziko."
Kuwa msanii
Joseph Ntensibe alinunua gari aina ya Mercedes kutokana na mauzo yake ya kwanza ya kazi ya sanaa. Alisema baadaye hilo lilimfanya ajione mpumbavu. Sasa akiwa na miaka 62, anakumbuka alipokuwa mtoto alikuwa akitengeneza wanasesere kutokana na majani ya mgomba. Siku hizi michoro yake inaonesha uzuri wa mchangayiko asilia wa Uganda wenye kiwango cha juu. Kazi hii imeitwa "Shimo la Maji."
Kupigania roho
"Mlo Mwengine" ndivyo picha hii ya Arnold Brungi inavyoitwa. Mwanamke wa Kiganda anadondoa buni. Hivi ndivyo anavyoyakimu maisha yake ili awe kununua chakula kwa ajli yake na wanawe. Kahawa ya Uganda inajulikana duniani kote na pia ni ghali. Birungi mwenye umri wa miaka 41 anafundisha sanaa na anafanya kazi kama mchoraji kulipia mlo wake mwenyewe.
Kumbukumbu za utotoni
Kazi kwenye Kitabu cha Kumbukumbu ya Sanaa ya Uganda 2014 zinaakisi maisha mapya na makongwe ya jamii ya Waganda. Tairi bovu la baiskeli na fimbo, kama vinavyoonekana kwenye picha hii ya David Kigozi, ni vitu maarufu vya kuchezea watoto nchini Uganda. Kigozi ni mmoja wa wasanii mashuhuri wa Uganda na kazi zake zimeonyeshwa Ulaya.
Sanaa ya kuishi
Picha ya Paul Kaspa iitwayo "Mti wa Maisha" inaonesha tambiko la kiasili la Afrika, ambapo wanakijiji hukusanyika chini ya kivuli cha mti mkubwa. Kaspa, mwenye umri wa miaka 33, alisomea sanaa na pia hufanya kazi kama mshauri nasaha kwa wanaougua Virusi vya Ukimwi/Ukimwi na watoto wa mitaani. Ana ndoto ya kumiliki skuli ya sanaa kwa ajili ya watoto.
Kufikiri Nyumbani
Taga Nuwagaba aliuza picha yake ya kwanza akiwa bado yuko skuli. Kisha alihamia London kujaribu bahati yake. Lakini akawa anakukumbuka sana nyumbani Uganda, hisia ambazo pia zinaelezewa kwenye michoro yake. Kuvua samaki kwenye Ziwa Viktoria ni moja ya mada zake maarufu.
Rangi za kuvutia zinazosimulia hadithi
Picha za Robert Yiga ni kielelezo cha vichekesho na zinazungumzia maisha yake magumu ya utotoni akiwa yatima kwenye kijiji kimoja nchini Uganda na vipi alivyopambana kupata fedha za kumuendesha kimasomo. Manjano na rangi ya chungwa iliyotitia ni alama ya kazi yake. Alilipia kozi yake kwenye chuo cha sanaa kwa kuuza picha zake.
Zogo la mjini
Mji mkuu wa Uganda, Kampala, linaweza kuwa eneo lenye ghasia sana na vile tu kuishi kwenye mji huo kwenyewe ni sanaa. Lakini bado unawavutia watu wenye vipaji nchini kote. Mjini Kampala, wanaweza kujenga mtandao, kufanya maonyesho na kuuza kazi za sanaa. Kwa Cliff Kibuuka, jiji hilo pekee ni chanzo cha mwamko.
Kupambana na ufisadi kwa kisumba cha kuchorea
Kampeni ya wasanii wa Uganda dhidi ya ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka. Picha ya Eria Nsubuga mtumishi wa umma fisadi, "anayekula" mamilioni ya fedha za walipa kodi zilizokusudiwa sekta ya afya, inaonesha kwamba wasanii wa Uganda wanajiona kama mwamko wa taifa. Nsubuga pia anapenda kuwachora wanamuziki nyota na wanasiasa kwenye gari za kifahari.
Sanaa katika kuwahudumia wanyamapori
Mwanzoni, Sam Rich hakutaka picha za wanyama kwenye kitabu hiki cha kumbukumbu. Hayo ni mambo ya watalii tu. Lakini kisha akaona picha hii ya sokwe wa milimani ya Jjuuko Hoods. Kutokana na fedha za mauzo ya kazi yake, Hood anataka kusaidia kunusuru misitu mikubwa na makaazi ya sokwe. Sasa hii ni sehemu ya kitabu cha kumbukumbu, ambayo inaweza kuonekana hapa: facebook.com/ugandaartsdiary