Safari ya tija
17 Januari 2013
Alinisihi babangu, habari za uhakika
Niwambie na wenzangu, Ujerumani zatoka
Tena ni kwa lugha yangu, Kiswahili zasikika
Nusu karne ya kheri, Mungu awape uhai
Hadi leo sijajuta, ukweli nihadithie
Miaka shirini sita, dunia niitambue
Na bado sijaichoka, niko nayo ina miye
Nusu karne ya kheri, Mungu awape uhai
Kwa makala moto moto, vijana tunajifunza
Kwa magoma na mikito, hakika nyinyi wa kwanza
Mafanikio si ndoto, ni nyendo tumejifunza
Nusu karne ya kheri, Mungu awape uhai
Haki mnosimamia, ukweli mtuambie
Hata iwe ni Korea, tawala zao tujue
Njia gani wapitia, jibu watutangazie
Nusu karne ya kheri, Mungu awape uhai
Kongo mpaka Kenya, kwa Kiswahili mwatamba
Hamida bila mumunya, Burundi anawapamba
Uganda sijawaminya, Leila anawabamba
Nusu karne ya kheri, Mungu awape uhai
Shangwe mshangilieni, Othmani wa Miraji
Kipindiche cha maoni, nakiona kama taji
Mola mjaze imani, kwetu huyu ndiye gwiji
Nusu karne ya kheri, Mungu awape uhai
Kalamu i mkononi, Mnete u salamuni,
Ssesanga u mdomoni, Umilkheri moyoni
Situmai yu makini, Idi msalimieni
Nusu karne ya kheri, Mungu awape uhai
Hadhi ya wenye imani, iko kwa Mola Azizi
Sitasita kumhini, abisha si wabobezi
Kwingineko sitamani, redio yenu makazi
Nusu karne ya kheri, Mungu awape uhai
Chanda changu ki shidani, kuendelea siwezi
Nawaaga kwaherini, Amina we mtetezi
Radhi ninawaombeni, iwapo nimewaudhi
Nusu karne ya kheri, Mungu awape uhai
Tanbihi: Shairi hili limeandikwa na Mwalimu Shaaban S. J. Lissu wa Dar es Salaam - Tanzania kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 50 ya DW.
Mhariri: Mohammed Khelef