1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ROMA: Mkutano kuhusu Afghanistan waanza leo

2 Julai 2007
https://p.dw.com/p/CBmg

Mkutano wa siku mbili kuhusu Afghanistan unaanza leo mjini Roma Italia. Mkutano huo unawaleta pamoja wajumbe wa Umoja wa Mataifa, jumuiya ya kujihami ya kambi ya magharibi NATO na viongozi wa Afghanistan.

Mbali na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon, katibu mkuu wa jumuiya ya NATO, Jaap de Hoop Scheffer, wanadiplomasia kutoka nchi zaidi ya 20 wanahudhuria mkutano huo wa mjini Roma.

Mazungumzo yatahusu utawala wa sheria na utengamano huku Afghanistan ikiendelea kutumbukia katika mzozo mkubwa.

Afghanistan inakabiliwa na ufisadi na machafuko yanayoitatiza serikali ya rais Hamid Karzai, yapata miaka saba tangu majeshi yaliyoongozwa na Marekani yalipowaangusha wanamgambo wa Taliban kutoka madarakani.

Mkutano wa mjini Roma unalenga kuunda mkakati wa kukabiliana na kushindwa kwa vyombo vya sheria vya Afghanistan.

Huko Afghanistan mwanajeshi wa Uingereza anayefanya kazi na shirika la NATO aliuwawa jana kwenye shambulio lililofanywa na wanamgambo wa Taliban kusini mwa nchi hiyo.

Wizara ya ulinzi nchini Uingereza imesema huyo ni mwanajeshi wake wa pili kuuwawa katika kipindi kirefu.

Idadi ya wanajeshi wa Uingereza waliouwawa nchini Afghanistan sasa imefikia 63 tangu mwishoni mwa mwaka wa 2001.