Ripoti zinatatanisha kuhusu afya ya Rais Hugo Chavez wa Venezuela, baada ya kiongozi huyo kufanyiwa operesheni ya dharura nchini Cuba, wiki mbili zilizopita.
Rais wa Venezuela, Hugo Chavez
Gazeti moja la Miami likinukulu duru zilizokaribu na idara ya upelelezi ya Marekani, limesema Rais Chavez yupo katika hali mbaya lakini sio mahututi.
Waziri katika ofisi ya rais, Erika Farias amesema, Chavez anaendelea vizuri kama ilivyotarajiwa, lakini Waziri wa Mambo ya Nje Nicolas Maduro, alionekana kuwa na wasiwasi wakati wa mahojiano yaliyotangazwa katika televisheni ya taifa. Waziri huyo alisema, Chavez anapigania afya yake na mustakabali wa taifa.
Upande wa upinzani unamtaka makamu wa rais kushika madaraka ya Chavez wakati kiongozi huyo akiwa nje ya nchi.