1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Rais wa Ujerumani mashakani

Katika uandishi habari, mtu anapomg'ata mbwa ndiyo inakuwa habari nzito, lakini mbwa anapomg'ata mtu ni jambo la kawaida.Kwa mtazamo huu, waandishi habari wanapolumbana na wenye madaraka waandishi wanajikuta mashakani.

Rais Christian Wulff atoa vitisho kwa waandishi habari

Rais Christian Wulff atoa vitisho kwa waandishi habari

Mfano huu umejitokeza hapa Ujerumani baada ya kisa cha mwandishi habari mmoja kuandika kashfa ya ununuzi wa nyumba ya kibinafsi kumhusu rais wa nchi hii.Taarifa hiyo haijampendeza kiongozi huyo na sasa anamtishia mwandishi habari huyu kupitia ujumbe wa simu ya Mkononi. Kutokana na kisa hiki waandishi habari wanajiuliza je uhuru wa Uandishi nchini Ujerumani upo hatarini.

Rais wa Ujerumani, Christian Wulff, ametangaza vita dhidi ya waandishi habari, hivyo ndivyo linavyosema gazeti la kila siku la hapa nchini la BILD. Rais huyo wa taifa alijaribu kumnyamazisha mhariri mkuu wa gazeti hilo, Kai Diekmann, juu ya kutoa taarifa zinazohusu kashfa ya mkopo wa kibinafsi alioupokea yeye mwenyewe rais Wullf. Inadaiwa rais huyo amemuachia ujumbe wa sauti kupitia simu ya mkononi mhariri huyo akimtishia kuvuruga uhusiano wote uliopo na gazeti hilo ikiwa kashfa hiyo itafichuliwa.

Gazeti la Sueddeutsche Zeitung linasema ujumbe huo wa rais Wulff kwa mhariri wa gazeti la Bild ulitolewa Desemba 12, ikiwa ni siku moja kabla ya gazeti hiyo kuiweka hadharani kashfa inayomuandama rais Wullf ya kupokea mkopo wa kibinafsi wa pfedha nyingi. Gazeti hilo la Bild ambalo ni miongoni mwa magazeti yanayochapishwa na kampuni ya Springer likathitibisha juu ya taarifa hizo kuhusiana na hatua hiyo ya rais.

Rais Wulff na kashfa ya mkopo

Rais Wulff na kashfa ya mkopo

Gazeti hilo likasema kwamba rais wa Ujerumani amekasirishwa juu ya uchunguzi uliofanywa na mwandishi wake kuhusu mkopo wa nyumba na kutoa vitisho miongoni mwao ikihusisha hatua za kisheria atakazozichukua rais huyo dhidi ya mwandishi anayehusika. Mkasa huu unawakumbusha wajerumani juu ya mjadala mzito ulioibuka kiasi miaka kumi iliyopita baada ya mwandishi habari Jens König kufichua taarifa juu ya ushawishi wa wanasiasa katika vyombo vya habari nchini. Katika mwaka 2003 mwandishi habari huyo König, akiwa kama mkuu wa kitengo cha masuala ya bunge katika gazeti la Berliner Tageszeitung (Taz), alianzisha mjadala na aliyekuwa katibu mkuu wa chama cha SPD, Olaf Scholz. Kitengo cha habari ndani ya chama hicho cha SPD kikataka kipengee hicho cha habari kifutwe.

Lakini mahojiano hayo baina ya katibu mkuu huyo wa zamani wa SPD na mwandishi habari Konig yakafanyiwa marekebisho makubwa kiasi cha kwamba wahariri husika wakafikia uamuzi wa kuyachapisha maswali ya muandishi huyo na kuyabadili majibu yaliyotoka kwa mwanasiasa huyo ili kutoa sura ya mahojiano halisi yalivyokwenda.

Magazeti mengi yaliripoti juu ya kisa hicho huku yakimuunga mkono mwenzao aliyefikwa na kisa hicho kilichoonekana kutaka kuwatia mashakani na kuwanyamazisha waandishi wa habari. Hans Leyendecker, mhariri wa gazeti la Süddeutsche Zeitung na mwanzilishi wa mtandao wa utafiti, anasema Juhudi hizo za muda mrefu za kuupigania uhuru wa uandishi habari ungeweza kufanikiwa endapo tu kungekuweko mshikamano miongoni mwa vyombo vya habari ambao haupo nchini Ujerumani.

Mwandishi Schmeller Johanna/Saumu Mwasimba

Mhariri Othman Miraji

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com