1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Senegal apigia upatu Umoja wa Afrika kujiunga G20

8 Julai 2023

Rais wa Senegal Macky Sall amesema ana matumaini kuwa mpango wa kuupatia Umoja wa Afrika kiti cha kudumu ndani ya kundi la mataifa ya G20 utakamilika wakati wa mkutano wa kundi hilo baadaye mwaka huu.

https://p.dw.com/p/4TcOd
Rais Macky Sall wa Senegal
Rais Macky Sall wa Senegal Picha: Lewis Joly/AP/picture alliance

Akihutubia kwa njia ya mtandao mkutano wa masuala ya uchumi unaofanyika kwenye mji wa kusini mwa Ufaransa wa Aix-en-Provence, Sall amesema kuukaribisha Umoja wa Afrika ndani ya kundi la G20 utakuwa uamuzi wa kutenda haki iliyocheleweshwa.

Amewambia wajumbe wanaoshiriki mkutano huo kuwa ameridhishwa na hatua inayopigwa kuelekea kuridhia Umoja wa Afrika kujiunga na kundi la G20 akikumbusha kuwa kwa jumla bara hilo linashika nafasi ya nane kwa thamani ya pato ghafi duniani.

Afrika Kusini ndiyo nchi pekee ya Afrika iliyo mwanachama wa kundi la G20 linaloyaleta pamoja mataifa 19 tajiri na yale yanayoinukia pamoja na Umoja wa Ulaya.