1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Mali na Waziri Mkuu washikiliwa na jeshi

25 Mei 2021

Maafisa wa kijeshi wa Mali waliokasirishwa na mabadiliko ya baraza la mawaziri wanamshikilia rais na waziri mkuu katika kambi ya jeshi, hatua inayolaaniwa vikali na jumuiya ya kimataifa na kutaka waachiliwe huru.

https://p.dw.com/p/3ttKv
Mali Präsident der Übergangsregierung Bah N'Daw
Picha: Präsidentschaft der Republik Mali

Taarifa ya pamoja iliyotolewa na Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya, Marekani na Uingereza imetoa wito wa kuachiliwa huru mara moja kwa Rais Bah N'Daw na Waziri Mkuu Moctar Ouane, ambao wameshikiliwa katika kambi ya kijeshi.

Kukamatwa kwao viongozi hao wanaongoza serikali ya mpito ambayo iliundwa kufuatia mapinduzi ya kijeshi mnamo mwezi Agosti, kumeongeza hofu ya kutokea mapinduzi mengine. Viongozi hao walikamatwa baada ya kufanya mabadiliko ya baraza la mawaziri mapema jana ili kutuliza ukosoaji mkubwa uliokuwa ukiikabili serikali yao ya mpito.

Aidha Umoja wa Ulaya umesema uko tayari kuzingatia kuwachukulia hatua viongozi wa kisiasa na kijeshi ambao wanazuia kufanyika mabadiliko nchini Mali.

"Tunalaani kilichotokea Mali katika masaa machache yaliyopita, utekaji nyara wa Rais na Waziri Mkuu, na tunaunga mkono ujumbe uliotumwa na SADC na Umoja wa Afrika," amesema Charles Michel, Rais wa Baraza la Ulaya.

Michel amesema kwa pamoja wanatoa  wito wa kurudishwa kwa serikali ya mpito, na kwamba klichotokea ni kitu kikubwa na wako tayari kuzingatia kuchukua hatua zinazohitajika.

 Vereidigung von Präsident Bah Ndaw in Mali
Rais Bah N'Daw akiapishwa rasmi mjini Bamako September 25, 2020Picha: Michele Cattani/AFP

Wasiwasi iwapo serikali ya mpito itafanikiwa

Matukio hayo yamezua wasiwasi iwapo serikali ya mpito itaweza kuendelea na mipango yake ya kuandaa uchaguzi mpya kama ilivyoahidi kuwa utafanyika Febuari ijayo. Umoja wa Mataifa umekuwa ukitumia dola bilioi 1.2 kila mwaka kuweka ujumbe wake wa askari wa kulinda amani nchini humo.

Viongozi hao wawili waliapishwa Septemba iliyopita baada ya jeshi la mapinduzi kukubali kukabidhi uongozi kwa serikali ya mpito ya kiraia kufuatia shinikizo la kimataifa.

Jeshi lilikamata madaraka mwezi mmoja kabla ya wanajeshi kuizingira nyumba ya Rais Ibrahim Keita na kufyatua risasi hewani. Baadae Keita aliamuwa kujiuzulu kupitia kituo cha televisheni ya taifa na kusema hatomwaga damu ili aweze kubakia madarakani.

Wanajeshi kisha walijitangaza katika kituo cha televisheni ya taifa kama Kamati ya Kitaifa ya Ukombozi wa Watu na kuahidi kurudisha haraka utawala wa kiraia. Lakini, hatua ya kuwakamata rais na waziri mkuu wa nchi inaonekana kutia shaka ahadi hiyo.

Kukamatwa kwa viongozi hao kulitokea saa moja au zaidi baada ya Baraza la Mawaziri la serikali mpya kutangazwa na kutowajumuisha Waziri wa Usalama wa Mambo ya Ndani Modibo Kone au Waziri wa Ulinzi Sadio Camara, wote wakiwa wanachama wa jeshi la mapinduzi.

Hakuna sababu iliyotolewa kuhusu kutengwa kwao, lakini hatua hiyo inaashiria kuongezeka kwa mgawanyiko ndani ya serikali ya mpito.

Vyanzo: ap,afp,rtre