1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Guinea-Bissau na mkuu wa majeshi wauawa

Thelma Mwadzaya2 Machi 2009

Rais wa Guinea-Bissau Joao Bernado Vieira amefariki dunia baada ya kuuawa kwa risasi nyumbani mwake.

https://p.dw.com/p/H40v

Wanajeshi wanaripotiwa kuyavamia makao makuu ya kiongozi huyo punde baada ya mkuu wa majeshi Jenerali Tagme Na Waie kushambuliwa katika makao makuu ya jeshi mjini Bissau alikokuwa akifanya mkutano na maafisa wa ngazi za juu.Watu wengine watano wanaripotiwa kujeruhiwa katika shambulio hilo.

Milio ya risasi na milipuko vilisikika katika mji mkuu wa Bissau mapema hii leo.Kwa mujibu wa taarifa risasi hizo zilisikika zikitokea karibu na makao makuu ya jeshi nchini humo.Mkuu wa majeshi Jenerali Batista Tagme Na Wai anaripotiwa kuuawa katika shambulio la jana jioni lililotokea karibu na makao rasmi ya Rais Joao Bernado Vieira.

Kulingana na mwanadiplomasia mmoja aliyezungumza na shirika la habari la Reuters taarifa za kuuawa kwa mkuu huyo wa majeshi zimethibitishwa.Watu wengine watano wanaodhaniwa kuwa maafisa wa kijeshi wanaripotiwa kujeruhiwa katika shambulio hilo na tayari wamepelekwa hospitali.Jengo moja nalo linaripotiwa kuharibiwa katika shambulio hilo.

Ghasia hizo zinaripotiwa kupungua wakati wa alfajiri ila risasi bado ziliendelea kusikika.Mpaka sasa haijabainika waliohusika na shambulio hilo.Jenerali Na Wai alihudumu katika utawala wa junta uliopindua utawala wa kiongozi wa kijeshi Vieira katika miaka ya 1990.Mkuu huyo wa majeshi alikuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya Vieira aliyerejea madarakani mwaka 2005.


Rais Joao Bernado Vieira aliingia madarakani kwa mara ya kwanza mwaka 1980 na kuongoza hadi mwaka 1999 huku akiungwa mkono na jeshi la nchi hiyo pamoja na chama cha ukombozi cha PAIGC.Itakumbukwa kuwa kiongozi huyo ni mmoja wa wakongwe wa kisiasa waliohusika katika harakati za kuikomboa Guinea-Bissau kutoka kwa minyororo ya Ureno.

Kiongozi huyo alienda uhamishoni baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe na kurejea nchini mwake mwaka 2004 na akachaguliwa tena kuwa rais mwaka uliofuatia.

Kulingana na mwanadiplomasia mmoja aliyezungumza na shirika la habari la Reuters taarifa za kuuawa kwa mkuu huyo wa majeshi zimethibitishwa.Watu wengine watano wanaodhaniwa kuwa maafisa wa kijeshi wanaripotiwa kujeruhiwa katika shambulio hilo na tayari wamepelekwa hospitali.Jengo moja nalo linaripotiwa kuharibiwa katika shambulio hilo.


Kwa mujibu wa msemaji wa jeshi la Guinea-Bissau Samuel Fernandes jana jioni, maafisa wa kijeshi waliviagiza vituo viwili vya redio binafsi kusitisha kurusha matangazo nacho kituo cha televisheni ya taifa kilisitisha kurusha matangazo baada ya kifo cha Jenerali Na Wai.

Guinea-Bissau imekumbwa kwa muda mrefu na mivutano kati ya uongozi na majeshi ya usalama.Kwa mujibu wa duru za kijeshi walinzi wa Rais Vieira walijaribu kumpiga risasi Jenerali Na Wai mwanzoni mwa mwaka huu.Hata hivyo mmoja wa walinzi hao alikanusha taarifa zilizosema kuwa lilikuwa jaribio la kumuua kiongozi huyo wa kijeshi.Baada ya tukio hilo jeshi liliamrisha kusambaratishwa kwa kundi hilo la wapiganaji waliokuwa wakimlinda Rais Vieira.

Wizara ya mambo ya ndani iliamua kukitumia kikosi hicho cha maafisa 400 ili kumlinda Rais Vieira baada ya makao yake rasmi kushambuliwa kwa risasi na guruneti tarehe 23 mwezi Novemba mwaka uliopita.Rais Vieira alinusurika katika shambulio hilo.

AFPE / RTRE