1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Sarkozy wa Ufaransa ziarani Syria

Mohamed Dahman2 Septemba 2008

Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa leo anawasili mjini Damascus Syria katika ziara iliotangazwa mno yenye lengo la kurudisha uhusiano wa ngazi ya juu kati ya nchi hizo na kuiondowa Syria zaidi katika kutengwa kimataifa.

https://p.dw.com/p/FACj
Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa.Picha: AP

Hii ni ziara ya kwanza kufanywa na kiongozi wa nchi wa mataifa ya magharibi katika kipindi cha miaka mitano.

Ziara hiyo ya siku mbili ni hatua ya hivi karibuni kabisa katika kurudisha uhusiano wa kawaida ambao ulikuwa umesitishwa baada ya mauaji ya mwaka 2005 ya waziri mkuu wa zamani wa Lebanon Rafik al Hariri rafiki wa karibu wa aliemtangulia Sarkozy, rais Jaques Chirac.

Ziara hiyo nchini Syria inaonekana kuwa ni ushindi wa kidiplomasia kwa Rais Bashar al- Asaad wiki sita baada ya kurudi tena katika jukwaa la dunia kwa ziara iliopigiwa debe mno mjini Paris Ufaransa.

Wachambuzi wa mambo pia wanaiona ziara ya kiongozi huyo wa Ufaransa kama fursa kwa Syria kuboresha uhusiano wake na Marekani ambayo inaendela kuiorodhesha Syria kuwa taifa lenye kudhamini ugaidi.

Akiandamana na waziri wake wa mambo ya nje Bernard Kouchner,Sarkozy atakutana na kula chakula cha jioni na Asaad leo hii.

Hapo kesho Alhamisi Sarkozy ambaye nchi yake inashikilia wadhifa wa kupokezana wa urais wa Umoja wa Ulaya atashiriki mkutano wa viongozi wanne wa nchi juu ya amani ya Mashariki ya Kati nchi nyengine zikiwa ni Uturuki na Qatar.

Serikali ya Uturuki imekuwa ikisuluhisha tokea mwezi wa Mei katika mazungumzo yasio ya moja kwa moja kati ya Syria na Israel ambazo vita havikumalizika rasmi tokea mwaka 1948.

Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na Kiongozi wa Qatar Sheikh Hamad bin Khalifa la Thani wote watakuwepo Syria kwa mazungumzo hayo.

Wakati alipokuwa Paris mwezi wa Julai Assad amesema alikuwa akitaraji Ufaransa na Marekani zitaweza kutowa msaada mkubwa kwa makubaliano ya amani kati ya Syria na Israel.

Mhariri mwelekezi wa gazeti la lugha ya Kingereza la Syria Today Andrew Tabler litolewalo kila siku anasema ziara ya Sarkozy inaonekana kama ni mlango na fursa kwa Syria kuboresha uhusiano wake na Marekani.

Wiki iliopita wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema ilikuwa haipangi kufuata mfano wa Ufaransa na kuonya kwamba hadi hapo Syria inatimiza dhima nzuri katika eneo la Mashariki ya Kati nchi hiyo itaendelea kujitenga yenyewe.

Lakini Imad Shaiby mkuu wa kituo cha utafiti wa mikakati mjini Damascus ambaye ana mawasiliano ya karibu uongozi wa Syria amesema anaamini ziara ya Sarkozy itaendeleza uhusiano wa nchi hiyo na Marekani.

Amesema Syria inavuna matunda ya kipindi kilichopita na kwamba uvumilivu wake umelipa.

Syria uhusiano wake na Ufaransa na Marekani umedhoofika tokea kuuwawa kwa Hariri katika mripuko mkubwa wa gari mjini Beirut.

Serikali ya Ufaransa na Marekani miongoni mwa nchi nyengine ziliituhumu Syria kwa kupanga mauaji hayo na mengine ya wapinzani wake nchini Lebanon.

Syria mara kwa mara imekanusha madai hayo lakini miezi miwili baadae iliondowa vikosi vyake kutoka Lebanon na kumaliza miongo mitatu ya udhibiti wake kwa nchi hiyo ndogo jirani.

Ufaransa ilichukuwa hatua mwaka jana ya kurekebisha uhusiano wake na Syria lakini ilisita na kuishutumu Syria kwa kukwamisha uchaguzi wa rais mpya wa Lebanon na hiyo kuchochea mzozo wa kisiasa uliodumu kwa miezi kadhaa nchini Lebanon.

Kuchaguliwa kwa Rais wa Lebanaon Michel Suleiman hapo mwezi wa Mei kulikofuatiwa na tangazo kwamba Lebanon na Syria zitaanzisha uhusiano wa kibalozi kwa mara ya kwanza kabisa kumefunguwa njia ya kurudishwa kwa uhusiano kamili.