1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Sarkozy harezi kamba

8 Septemba 2010

Wagomaji waahidi migomo zaidi kupinga sera zake za bima.

https://p.dw.com/p/P772
Rais Sarkozy wa Ufaransa (kulia)Picha: AP

Rais Nicholas Sarkozy wa Ufaransa, amebakia leo na ukaidi wake kutoitikia malalamiko makubwa ya waandamanaji barabarani wanaopinga mpango wake wa kupandisha umri wa kustaafu kutoka miaka 60-62 na ameahidi kusonga mbele na mageuzi yake muhimu aliopanga.

Chama cha kijamaa cha upinzani (Socialist) kimesema rais Sarkozy hasemi kweli na vyama vya wafanyikazi navyo vimeapa kupambana na sera zake za uchumi na mageuzi anayopanga.

Wapinzani wa rais Sarkozy, waliitikia kwa hasira kubwa msimamo aliouchukua Rais Sarkozy hii leo wa kutojali madai yao waliotoa kupitia maandamano na migomo ya jana.Chama cha upinzani cha Kisoshalist, kimemuuita Sarkozy "muongo " na vyama vya wafanyikazi vimeonya kuandaa maandamano zaidi kufuatia migomo ya jana kuchafua usafiri,kufunga shule .

Shina la sera zake za mageuzi, ni kuongeza umri wa kustaafu .Anapanga kupandisha umri huo hatua kwa hatua hadi kufikia miaka 62 kutoka miaka 60 ifikapo 2018. Sarkozy, ameapa hakuna swali la kuregeza kamba juu ya swali hili.

Rais Sarkozy, akakariri kuwa, atajumuisha katika mageuzi yake matarajio maalumu kwa wale wanaoanza kazi wakiwa na jumri mdogo wa miaka 18 na kwa kazi maalumu zenye ugumu viwandani.

Msemaji wa chama cha Upinzani cha kisocialist, Benoit Hamon, amesema Rais Sarkozy ameregeza kidogo tu kamba."Mageuzi aliyoahidi ni uwongo mtupu." alisema Hamon.Kwanini lakini, kuna upinzani mkubwa juu ya sera za mageuzi ya bima aliopendekeza Rais Sarkozy ?

Rais Sarkozy, anadai, mfumo wa bima ya uzeeni kwa wastaafu lazima ufanyiwe marekebisho kama sehemu ya juhudi za kupunguza nakisi kubwa ya bajeti ya serikali .Lakini ,vyama vya wafanyikazi na wapinzani wake wa kisiasa vinadai sera zake zinawaumiza zaidi wanyonge na wafanyikazi.

Maandamano ya jana yaliungwamkono na watu milioni 1.12 kwa muujibu wa wizara ya ndani ya Ufaransa.Na vyama vya wafanyikazi vimeapa kugoma zaidi ikiwa Sarkozy hatabadili msimamo wake na vilipanga mkutano alaasiri ya leo kuzingatia mkakati wao unaofuata.

Rais Sarkozy, amedhofika nguvu zake kutokana na kashfa mbali mbali na umaarufu wake umepungua hadi 34% na hivyo, uko chini kabisa kuliko wakati wowote ule.Na hii ,ni miaka 2 tu kabla ya uchaguzi wa urais 2012 anaopanga kugombea.

Mwandishi:Ramadhan Ali/AFPE

Mhariri:Abdul-Rahman