1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Saleh asaini makubaliano ya kuacha madaraka

24 Novemba 2011

Hatimaye Rais Ali Abdulla Saleh wa Yemen amesaini makubaliano yanayofungua njia ya kuondoka madarakani, akikabidhi madaraka hayo kwa makamo wake, naye akihakikishiwa kinga ya kutoshitakiwa.

https://p.dw.com/p/13GHW
Rais Ali Abdullah Saleh akisaini makubaliano ya kuachia madaraka.
Rais Ali Abdullah Saleh akisaini makubaliano ya kuachia madaraka.Picha: dapd

Kitendo cha kuweka saini makubaliano haya, kinamfanya Saleh kuwa kiongozi wa nne katika ulimwengu wa Kiarabu kulazimika kuachia madaraka kwa sababu ya shinikizo la umma, ndani ya mwaka huu.

Lakini akilinganishwa na Zine Ben Ali wa Tunisia, Saleh hatalazimika kuishi uhamishoni. Kinyume na Hosni Mubarak wa Misri, Saleh hatafikishwa mahakamani. Na labda kinyume na Muammar Gaddafi wa Libya, yumkini hatakamatwa na waasi na kuuliwa kwa risasi.

Makubaliano aliyoyaweka saini jana mjini Riyadh, mbele ya Mfalme Abdullah wa Saudi Arabia, yanamtaka Saleh kukabidhi madaraka kwa makamo wake, Abd-Rabb Mansour hadi ndani ya siku 30 hizi, ambaye naye anatakiwa aitishe uchaguzi ndani ya siku sitini zijazo.

Makubaliano hayo yaliyoandaliwa na Baraza la Ushirikiano la Nchi za Ghuba (GCC) yanatoa kinga ya kutoshitakiwa pia kwa familia na watu wa karibu na Saleh.

Waandamanaji wakipinga makubaliano ya Rais Saleh na Baraza la Ghuba.
Waandamanaji wakipinga makubaliano ya Rais Saleh na Baraza la Ghuba.Picha: dapd

Waandamanaji katika mji mkuu wa Yemen, Sanaa, waliyapinga hapo hapo yalipotiwa saini wakiyaita makubaliano ya Saleh na mataifa ya nje, na sio kati yake na wao.

Maandamano makubwa zaidi yameitishwa leo na kesho dhidi ya Saleh, huku waandamanaji wakishikilia kwamba wanataka kiongozi huyo apandishwe mahakamani kwa mauaji na sio kupewa kinga.

Mara baada ya kutia saini makubaliano hayo, Saleh aliahidi kushirikiana na upinzani akisema kilichotokea katika nchi yake hakikuwa sehemu ya utamaduni wa Kiarabu, wa Yemen wala wa Waislamu.

"Saini hii sio muhimu. Muhimu ni dhamira njema na kujitolea kwa moyo mmoja kwa ajili ya kazi kubwa na ya kiadilifu kushiriki kwenye ujenzi mpya wa kile kilichoharibiwa na mgogoro wa miezi 10. Nataraji ukabidhianaji madaraka utakuwa wa salama, kwani vurugu zimeuvunja umoja wa taifa letu." Amesema Saleh.

Mwandamanaji wa Yemen akiwa amejichora bendera za Libya, Tunia, Misri na ya nchi yake.
Mwandamanaji wa Yemen akiwa amejichora bendera za Libya, Tunia, Misri na ya nchi yake.Picha: dapd

Pamoja na Saleh, waliotia saini makubaliano hayo ni viongozi wa vyama vya upinzani na chama tawala, mbele ya Mfalme Abdullah wa Saudi Arabia na mjumbe wa Umoja wa Mataifa wa Yemen, Jamal Bin Omar. Upinzani uliwakilishwa na mkuu wa Baraza la Taifa, Mohamed Basindwa.

Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton, ameyapongeza makubaliano haya kama mwanzo muhimu sana na kuwataka raia wa Yemen kukubaliana nayo kwa moyo safi.

Rais Barack Obama wa Marekani, amesema makubaliano hayo yanawakaribisha watu wa Yemen karibu na lengo lao la kuwa na demokrasia na mwanzo mpya.

Kwa upande wake, Mfalme Abdullah wa Saudi Arabia, ambaye amesimamia makubaliano hayo, alimpogeza Rais Saleh, akiwataka raia wa Yemen kufungua ukurasa mpya wa historia.

Mara tatu, Saleh alikataa kusaini makubaliano haya. GCC imeufanyia marekebisho kadhaa mpango huu, kabla ya Saleh kukubali kuuweka saini. Watu 900 wamepoteza maisha na maelfu kujeruhiwa, tangu maandamano dhidi ya Saleh yaanze hapo Januari mwaka huu.

Waandamanaji wanataka sio tu kuondoka madarakani kwa Saleh, bali pia kufikishwa mahakamani kwa mauaji hayo. Wameapa kuendelea kubakia kwenye uwanja wa Taghyir hadi madai yao yatakapotimizwa.

Mwandishi: Mohammed Khelef/DPA/AFP/AP
Mhariri: Josephat Charo