1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Rais Putin ziarani mashariki ya kati

Rais wa Urussi Vladmir Putin anaendelea na ziara yake mashariki ya kati.

Amefanya mazungumzo na viongozi wa Saudi Arabia mjini Riyadh na kuahidi kuimarisha uhusiano na ulimwengu wa kiislamu pamoja na kuisaidia Saudi Arabia kutengeneza nishati ya atomiki.Rais Putin atatembelea pia Qatar na Jordan

Rais Putin ameanza ziara hiyo ya mashariki ya kati ambayo huenda ikawa ndio ziara yake ya mwisho katika eneo hilo kama rais.

Ni mara ya kwanza pia kwa kiongozi wa urussi kutembelea mataifa hayo ya Saudi Arabia,Qatar na Jordan ambaye yanatazamwa kama ni washirika wakubwa wa nchi za magharibi.

Urussi inayaangalia mataifa hayo kama kifaa muhimu cha kujenga uchumi mpya,siasa na hata uhusiano wa kijeshi na ulimwengu wa kiarabu.

Akizungumzia juu ya masuala ya kiuchumi rais Putin amesema,

Saudi Arabia kama Urusi inafanya juhudi za kupanua uchumi kwa kutumia technologia ya hali ya juu na kwa hivyo ni kwa manufaa yetu na inatuvutia.

Hii leo akiwa mjini Riyadh nchini Saudi Arabia rais Putin amejitolea kuisaidia nchi hiyo kutengeneza nishati ya atomiki na kuahidi kujenga ushirikiano na ulimwengu wa kiislamu.

Urusi imetoa pendekezo hilo la kuimarisha uhusiano wa kijeshi na nishati na taifa hilo la Saudi Arabia ambalo ni mshirika wa karibu wa Marekani baada ya mataifa ya ghuba yenye utajiri mkubwa wa mafuta miezi miwili iliyopita kuonyesha azma ya kutaka kuwa na technologia ya nishati ya Nuklia.

Saudi Arabia mshirika wa dhati wa Marekani imeonekana kulainika mbele ya rais Putin kwani mfalme Abdullah amemsifu Putin hapo jana na kumtaja kama ni mtu wa watu,mpenda amani na mwenye kuzingatia haki.

Hata hivyo Urussi pia inajaribu kurudisha ushawishi wake katika siasa za kimataifa kwa kuzishambulia sera za nje za marekani.

Akizungumza na wafanyibiashara huko Riyadh leo hii rais Putin amesema pia nchi yake inatafuta njia za kuleta mwafaka katika maeneo yote ikiwa ni pamoja na mashariki ya kati na nchi za ghuba.Hakutaja lakini hata dakika moja juu ya kampeini ya kijeshi ya Urussi iliyosababisha mauaji ya maelfu ya watu huko Chechniyah.

Ziara ya Putin imekuja baada ya Urussi kukosoa waziwazi sera za nchi za magharibi kuelekea mzozo wa Israel na Palestina.

Kwa upande mwingine ziara hii ni muhimu kwa Putin kwani Urussi inataka kuiuzia Saudi Arabia silaha. Duru za kidiplomasia pia zinaeleza kwamba mazungumzo ya Putin mjini Riyadh yanatarajiwa kufikia mwafaka juu ya uuzaji wa vifaru kiasi 150 aina ya T90 kwa nchi hiyo ambayo imekuwa ikinunua vifaa vyake vya kijeshi kwa nchi za magharibi.

Putin anaelekea jioni hii nchini Qatar ambako wadadisi wa mambo wanasema lengo kuu nchini humo ni kujadili juu ya gesi.Kutoka Qatar Putin ataelekea Jordan ambako atakutana na mfalme Abudullah wa pili na rais wa palestina mahmoud Abbas.

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com