1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Mubarak ziarani mjini Washington

Oumilkher Hamidou18 Agosti 2009

Juhudi za kufufua utaratibu wa amani kati ya Israel na Palastina

https://p.dw.com/p/JDOC
Rais Mubarak azungumza na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Hillary ClintonPicha: AP

Rais Hosni Mubarak wa Misri,akiwa ziarani mjini Washington,"alibadilishana mawazo" jana pamoja na waziri wa mambo ya nchi za nje bibi Hillary Clinton kuhusu utaratibu wa amani ya mashariki ya kati,kabla ya mazungumzo yake ya leo pamoja na rais Barack Obama.Suala la haki za binaadam nchini Misri nalo pia lilijadiliwa.

Wakati wa mazungumzo yao ya siri katika hoteli moja ya mjini Washington,rais Mubarak na waziri wa mambo ya nchi za nje Hillary Clinton "walibadilishana maoni" juu ya namna wanavyotathmini juhudi za amani za Marekani na mataifa mengine,zilizolengwa kufufuwa mazungumzo kati ya Israel na Palastina.

Rais Hosni Mubarak na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Hillary clinton wamezungumzia pia masuala ya haki za binaadam na demokrasia nchini Misri,hali nchini Iran,Sudan,Pakistan na Afghanistan.Kuhusu uhusiano wa pande mbili,rais Mubarak na waziri wa mambo ya nchi za nje Hillary Clinton wamezungumzia ushirikiano wao katika sekta za kiuchumi na elimu.

Hosni Mubarak in Washington
Wafuasi wa rais Mubarak wamshangiria mjini WashingtonPicha: AP

Akiwa na umri wa miaka 81 ,Mohammed Hosni Mubarak aliyeingia madarakani tangu mwaka 1981 ni mshirika mkubwa wa Marekani katika eneo la Mashariki ya kati.Nchi yake imetiliana saini makubaliano ya amani pamoja na Israel tangu mwaka 1979 na rais Mubarak amekua kila kwa mara akitilia mkazo umuhimu wa mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palastina.Rais MUbarak anasema:

"Tunapaswa kufanya kila tuwezalo ili kuzileta pamoja pande hizi mbili.Tunabidi tusake ufumbuzi wa mzozo kati yao .Tunabidi tubadilishe mitazamo yetu....hakuna njia nyengine."

Ziara yake ya sasa mjini Washington inatokea katika wakati ambapo serikali ya Marekani inaishinikiza Israel iache kujenga mitaa ziada ya wahamiaji wa kiyahudi katika maeneo ya ukingo wa magharibi na kuzitaka wakati huo huo nchi za kiarabu ziaanzishe uhusiano wa kawaida pamoja na dola hilo la kiyahudi.

Katika ziara yake hii,rais Hosni Mubarak amefuatana na waziri wake wa mambo ya nchi za nje Ahmed Aboul Gheith na waziri wa fedha Youssef Boutros Ghali.

Kwa maoni ya waziri wa mambo ya nchi za nje nwa Misri,Aboul Gheith,"ziara hii inatokea katika wakati muhimu sana kwasababu wamarekani wanakurubia kutangaza mtazamo wao wa namna ya kufikia amani na kumaliza mvutano kati ya Israel na Palastina."

Hii ni mara ya kwanza kwa rais Mubarak kufika ziarani nchini Marekani tangu mwaka 2004 alipomtembelea rais wa zamani wa Marekani George W. Bush huko Crawforf-Texas.

Mawandishi : Ommilkheir Hamidou/AFP

Mahariri:M.Abdul-Rahman