1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Mubarak aiachisha kazi serikali

29 Januari 2011

Polisi wanaendelea kukabiliana na waandamanaji nchini Misri huku Rais Hosni Mubarak akiiachisha kazi serikali yake.

https://p.dw.com/p/106x7
Rais Hosni Mubarak wa MisriPicha: picture-alliance/dpa

Rais wa Misri, Hosni Mubarak hii leo amekataa kuitikia wito wa kujiuzulu, baada ya kuamuru wanajeshi na vifaru kuingia mijini katika jitahada ya kutuliza maandamano makubwa dhidi ya utawala wake wa miaka 30.

Proteste in Ägypten gegen Mubarak Regime Kairo
Picha: AP

Mubarak ameiachisha kazi serikali yake na ametoa wito wa kufanywa majadiliano ya kitaifa ili kuzuia vurugu, kufuatia siku moja ya mapambano, kati ya polisi na waandamanaji wanaolalamika kuhusu umaskini na utawala wa kidikteta.

Duru za kitengo cha afya zinasema, hadi watu 24 wameuawa na zaidi ya wengine 1000 wamejeruhiwa katika mapigano yaliyotokea katika miji ya Cairo,Suez na Alexandria.

Demonstration in Suez, Ägypten
Picha: ap

Machafuko hayo yamewashtusha wengi katika eneo la Mashariki ya Kati ambako viongozi wengine wa kiimla huenda wakakabiliwa na changamoto na mtikisiko katika masoko ya kimataifa. Hapo jana, Rais wa Marekani Barack Obama alisema kuwa alizungumza na Rais Mubarak na alimuomba kuchukua hatua madhubuti zitakazoendeleza haki za wananchi wa Misri.

Muda mfupi baada ya Mubarak kutoa hotuba yake, waandamanaji walirejea barabarani kwa wingi ,licha ya kutangazwa amri ya kutotoka nje.

Mwandishi: Maryam Abdalla/Rtre
Mhariri:Prema Martin