Rais George Bush wa Marekani ataka pesa zaidi kwa ajili ya vita | Matukio ya Kisiasa | DW | 23.10.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Rais George Bush wa Marekani ataka pesa zaidi kwa ajili ya vita

Wakati baadhi ya wananchi wa Marekani na duniani kote wakimtaka Rais George Bush wa Marekani kuondoa majeshi yake nchini Iraq, kiongozi huyo amelitaka bunge la nchi hiyo kuidhinisha kitita cha karibu dola 200 kwa ajili ya matumizi ya kivita nchini Iraq na Afghanistan

Rais George W. Bush wa Marekani

Rais George W. Bush wa Marekani

Rais George Bush wa Marekani amewasilisha maombi ya karibu dola bilioni 200 kwa ajili ya kufanikisha shughuli za kijeshi nchini Iraq na Afghanistan katika kipindi cha mwaka ujao.

Uamzi huo wa Rais Bush umepokelewa kwa hisia tofauti na baadhi ya wananchi wa Marekani ikizingatiwa kwamba wengi wao wanataka majeshi yao yarejeshwe nyumbani baada ya kipindi kirefu cha kuishi nchini Iraq.

Baada ya kuwasilisha matakwa yake hayo Rais George Bush amesema anajua kwamba anapingwa na watu wengi katika mkakati wake wa vita lakini akasema ikiwa Wamarekani wanataka majeshi yao yarejee nyumbani ni lazima wapewe nyenzo zitakazowawezesha kukamilisha shughuli yao haraka ndiyo waondoke katika uwanja wa vita.

Ameongeza kwa kusema kwamba pamoja na kuwa wapinzani wake wanafikia hatua ya kuandamana kutokana na mgogoro wa vita ya Iraq, hawana budi kutoa ushirikiano kwa kupitisha muswada aliouwakilisha kwa Bunge la Congress, ambao utayawezesha majeshi yote kurejea nyumbani.

Uchambuzi wa pesa zilizoombwa na Rais Bush unaonesha kuwa dola bilioni 196.4 zitatumika katika kusawazisha mambo kwenye uwanja wa vita huko Iraq na Afghanistan, katika kipindi cha mwaka ujao, yakiwemo masula ya utawala vitani.

Hata hivyo mpango huo wa Rais Bush umeonekana kutomridhisha spika wa Bunge Bibi Nancy Pelosi anayetokea katika chama cha upinzani cha Demokrat kufuatia kile alichokiita kwamba ni juhudi finyu na zisizo muafaka.

Kiongozi huyo mkubwa kabisa Bungeni ameongeza kwa kusema kwamba kitendo cha Rais Bush kuwasilisha maombi ya karibu dola bilioni 200 kwa ajili ya vita ya Iraq na Afghanistan wakati akipuuza masuala ya afya kwa zaidi ya watoto milioni 10 nchini Iraq, inaonesha walakini katika utawala wake.

Chama cha upinzani cha Demokrat kinasisitiza kwamba gharama za kushughulikia vita nchini Iraq zimekuwa zikipanda siku hadi siku, wakati watu wengi zaidi wakizidi kupoteza maisha pamoja na kuitia madoa Marekani kwenye uso wa dunia.

Ikiwa matakwa hayo ya Rais Geoge Bush yatapitishwa kwa kuidhinishwa kiasi hicho cha pesa, jumla kuu itakuwa imefika dola bilioni 757.4 tangu aliponza mkakati wake dhidi ya magaidi kufuatia mashambulizi ya Septemba 11 2001.

Utafiti uliofanywa na kituo cha Washington Post-ABC unaonesha kwamba asilimia 43 ya Wamarekani wanataka bajeti ya Iraq na Afghanistan iondolewe, wakati asilimia 23 wakisema ipunguzwe, na asilimia 27 wanaiunga mkono serikali iliyoko madarakani juu ya gharama za vita nchini Iraq na Afghanistan.

 • Tarehe 23.10.2007
 • Mwandishi Tuma Provian Dandi
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/C7gV
 • Tarehe 23.10.2007
 • Mwandishi Tuma Provian Dandi
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/C7gV

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com