Rais Chavez awasili Moscow kwa ziara rasmi nchini Urusi | Matukio ya Kisiasa | DW | 28.06.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Rais Chavez awasili Moscow kwa ziara rasmi nchini Urusi

Ameitaka Urusi isaidie katika mapinduzi kote duniani dhidi ya Marekani.Bwana Chavez anatarajiwa pia kuzuru nchi za Belarus na Iran ambazo Marekani inauelezea uongozi wao kuwa usiokubalika.

Rais Hugo Chavez wa Venezuela

Rais Hugo Chavez wa Venezuela

Ziara ya Rais Chavez nchini Urusi huenda ikaikirihisha Marekani kwani ni siku kadhaa kabla yeye kusafiri huko kwa mazungumzo na na Rais George Bush yanayolenga kutafuta suluhu baada ya kutangaza mpango wa kuweka makombora ya kujihami katika nchi za Ulaya mashariki.Bwana Chavez anapongeza msimamo mkali wa Rais wa Urusi Vladimir Putin wa kupinga hatua hiyo.

Hata hivyo kwa mujibu wa wadadisi,Urusi inaonyesha ishara kuwa inapunguza umuhimu wa ziara ya Rais Chavez baada ya kuamua kutomualika kiongozi huyo kutoa hutuba rasmi.Jambo hilo linatiwa nguvu mkono na bunge la Urusi linalomuunga mkono Rais Vladimir Putin.

Kiongozi huyo wa Venezuela ameandamana na kundi la wachezaji na waimbaji pamoja na ujumbe wa maafisa wa kijeshi.Rais Chavez ameionya Marekani dhidi ya kutotumia nguvu dhidi ya Urusi huku akielezea ushirikiano wa nchi yake na Moscow.

“Nchi yetu ni ya amani.Tunapigania amani na tunatekjeleza amani kwa ajili yenu.Kama ilivyo katika Amerika ya Kusini,eneo la Karibik na pia duniani.Sisi si nchi inayoendeleza vita.Wenye kuendesha vita ni wengine vinavyoleta mauaji ya watu na hujma za mabomu…Na hivyo kujaribu kudhibiti ulimwengu.Lakini naamini hawatafanikiwa”, alisisitiza Chavez.

Kiongozi huyo aliongeza kuwa hatua ya kununua silaha haipo katika ajenda ya ziara yake.Hata hivyo mwaka jana nchi yake ilinunua helikopta za vita,ndege za vita na bunduki zilizo na thamani ya euro bilioni 2.2.Kabla ya kuanza ziara yake Bwana Chavez alisema kuwa huenda akatathmini uwezekano wa kununua nyambizi.

Rais Chavez ameyakaribisha makampuni ya Urusi yanayopanga kuwekeza nchini mwake ili kuimarisha sekta ya nishati iliyonawiri.Kwa upande mwingine Rais Chavez anasema kuwa makampuni ya Marekani yasiyotaka kufuata sheria zake mpya za rasilmali ya mafuta hazina budi kuondoka.

Kampuni za mafuta za ExxonMobil na ConocoPhillips za Marekani zilijiondoa katika shughuliza kutafuta mafuta nchini Venezuela mwanzoni mwa juma hili.

Kwa mujibu wa gazeti la Kommersant Rais Putin wa Urusi amemtaka Rais Chavez kumuunga mkono katika mipango yake ya kuandaa mkutano wa mwaka ujao wa mataifa yanayouza nje gesi.Hiyo ni sehemu ya juhudi za kuunda shirika linalosimamia biashara ya gesi kuwa sawa na lile la mafuta la OPEC.

Viongozi wa nchi hizo mbili wanatarajiwa pia kujadilia mipango ya kuanzisha miradi nchini Venezuela kupitia kampuni kubwa ya mafuta ya Urusi ya Gazprom na Yukoil ya mafuta.Mipango hiyo pia inalenga katika ujenzi wa bomba la gesi litakalounganisha mataifa ya Argentina,Bolivia,Brazil,Paraguay na Venezuela.

 • Tarehe 28.06.2007
 • Mwandishi Mohammed Abdul-Rahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHBv
 • Tarehe 28.06.2007
 • Mwandishi Mohammed Abdul-Rahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHBv

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com