1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Bush aanza ziara ya Amerika kusini

Moahammed Abdul-Rahman8 Machi 2007

Lengo ni kuwaahakikishia wakaazi wa eneo hilo kwamba Marekani bado inawajali,huku kukiwa na hali ya kuvunjwa moyo na sera ya dola hilo kuu kuelekea kanda hiyo ya bara la Amerika.

https://p.dw.com/p/CHId
Rais George W.Bush wa Marekani
Rais George W.Bush wa MarekaniPicha: dpa

Rais George W. Bush wa Marekani leo anaanza ziara ya wiki moja katika Amerika kusini, akiwa na azma ya kurekebisha kile kinachotazamwa na wengi katika kanda hiyo, kuwa ni sera mbaya ya Marekani, jambo ambalo limemsaidia kiongozi wa mrengo wa Shoto wa Venezuela kuwa na ushawishi mkubwa katika eneo hilo.

Rais Bush ambaye atazitembelea nchi tano akianzia Brazil hii leo, atasisitiza juu ya hoja kwamba demokrasia imara ndiyo msingi wa maendeleo. Mbali na Brazil atazitembelea pia Uruguay, Colombia, Guatemala na Mexico. Binafsi amesema ziara yake hiyo ina madhumuni ya kuwakumbusha watu wa eneo hilo kwamba Marekani inawajali.

Ziara yake hii inafuatia mlolongo wa uchunguzi wa maoni ya wakaazi kuhusiana na safari yake katika Amerika kusini, ambako kushiriki kwake katika mkutano wa Viongozi wakuu wa bara la Amerika Novemba 2005 mjini Buenos Aires-Argentina, ilizusha maandamano makubwa ya upinzani, ambayo yalidhihirisha kwamba wengi hawapendezwi na sera ya taifa hilo kubwa.

Utawala wa Bush unasisitiza kwamba haujalipuuza eneo hilo na kwamba mwaka jana ulitoa msaada wa dola bilioni 1 na milioni 6, na ni mapema juma hili tu, ambapo Bush alitangaza mipango ya onyongeza ya msaada wa dola 385 bilioni kutanua miradi ya ujenzi wa makaazi katika eneo hilo. Akasema pia kwamba atatuma manuwari ya shughuli za matibabu huko Amerika kusini na Caribbean mwezi Juni kuwatibu wagonjwa 85,000.

Wadadisi wa mambo wanasema hii ni sehemu ya mkakati wa kukabiliana na kuzidi kwa ushawishi wa Kiongozi wa mrengo wa shoto wa Venezuela Hugo Chavez. Chavez anasemekana kuzipa baadhi ya nchi za Amerika kusini mabilioni ya dola mnamo miaka michache iliopita, na kugeuka kuwa mtu maarufu miongoni mwa walala hoi katika eneo hilo.

Hata hivyo wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani inasema Bush hakujaribu kushindana na Chavez, ambaye aliwakasirisha maafisa wa Marekani Septemba mwaka jana wakati wa hadhara kuu ya umoja wa mataifa alipomwita Kiongozi wa Marekani kuwa Shetani.

Jana waandamanaji kiasi ya 2000, wanafunzi na viongozi wa vyama vya wafanyakazi waliandamana katika mji mkuu wa Colombia-Bogota, wakitoa kauli za kuipinga Marekani kabla ya ziara ya siku tatu ya Rais Bush nchini humo badae wiki hii.

Akiwa Brazil, kesho Rais Bush atakua na mazungumzo na Rais Luiz Inacio Lula da Silva, kabla ya kuelekea Uruguay.

Viongozi hao wawili wanatarajiwa kusaini mkataba juu ya utengenezaji na uuzaji wa pamoja wa mafuta aina ya ethanol yanayotengenzwa kutokana na miwa. Na wakati atakapokua Uruguay kituo cha pili cha ziara yake, mkataba kuhusu biashara huria ni miongoni mwa masuala katika ajenda.