1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia wanasa katika mashambulizi ya Fallujah

28 Mei 2016

Mamia ya wananchi wamenasa na wengine mamia wameukimbia mji wa Fallujah wakati operesheni ya kuukombowa mji huo kutoka kundi la Dola la Kiislam ikipamba moto kwa vikosi vya serikali kuingia katika viunga vya mji huo.

https://p.dw.com/p/1IwTC
Picha: Getty Images/AFP/A. Al-Rubaye

Mamia ya wananchi wameukimbia mji wa Fallujah wakati operesheni ya kuukombo mji huo kutoka kundi la Dola la Kiislam ikipamba moto wakati vikosi maalum vya kupambana na ugaidi vya Iraq kwa mara ya kwanza vikiwekwa kwenye viunga vya mji huo.

Kikosi cha kupambana na ugaidi nchini Iraq ambacho ni kikosi kulichonolewa vizuri kabisa kwa mapambano kimeingia katika maeneo ya ukingo wa mji huo Jumamosi (28.05.2016) ambao ni ngome kuu ya Kundi la Dola la Kiislamu.

Kamanda mkuu wa operesheni ya kuukombowa mji wa Fallujah Abdulwahab al-Saadi ameliambia shirika la habari la AFP kwamba kikosi hicho cha CTS kwa kushirikiana na polisi wa kupambana na hali ya hatari wa Anbar pamoja na wapiganaji wa kikabila wameingia maeneo ya Tareq na Mazraa yalioko kusini na mashariki ya Fallujah na kwamba wataingia katika mji huo masaa machache yajayo kuukombowa kutoka kundi la Dola la Kiislamu.

Fallujah ambao uko kama kilomita 50 tu magharibi ya Baghdad ni mojawapo ya miji miwili mikubwa ya Iraq mwengine ukiwa ni Mosul inayoendelea kudhibitiwa na kundi la Dola la Kiislamu.

Raia wanaokadiriwa kufikia 50,000 wamenasa katika mji huo wa Fallujah huku wengine ambao idadi yao ni maradufu ya hiyo wakiwa wamenasa kwenye mpaka kati ya Syria na Uturuki kutokana mashambulizi ya kundi la Dola la Kiislamu karibu na mji wa Allepo nchini Syria.

Juhudi za kukombowa Fallujah

Hapo Mei 22 maelfu ya wanajeshi wa Iraq walianza mashambulizi ya kuukombowa mji wa Fallujah ambao ni mojawapo ya ngome muhimu kabisa za kundi la Dola la Kiislamu.

Wapiganaji wanaoiunga mkono serikali katika mapambano ya kukombowa Fallujah.
Wapiganaji wanaoiunga mkono serikali katika mapambano ya kukombowa Fallujah.Picha: Getty Images/AFP/A. Rubaye

Wapiganaji wa kundi la IS waliojibanza Fallujah wanafikia 1,000 na huo ni mji wa kwanza wa Iraq kutekwa na kundi hilo hapo mwezi wa Januari mwaka 2014 na muongo mmoja uliopita ni mahala ambapo jeshi la Marekani limeshuhudia mapigano makali kabisa tokea Vita vya Vietnam.

Mji huo umekuwa ukizingirwa na vikosi vyenye kuiunga mkono serikali kwa miezi kadhaa sasa na wasi wasi umekuwa ukiongezeka miongoni mwa mashirika ya haki za binaadamu kwamba wananchi wamekuwa wakinyimwa chakula kwa makusudi ili wafe njaa.

Ulinzi wa raia upewe kipau mbele

Sheikh mkuu wa Kishia ametowa wito wa kulindwa kwa raia waliokwama huko Fallujah ambapo wapiganaji wa kundi la IS wanawazuwiya wasiondoke.

Seikh Ali al-Sistani wa Iraq.
Seikh Ali al-Sistani wa Iraq.Picha: AFP Photo/Getty Images

Sheikh Ali al- Sistani amesema kulindwa kwa raia waliokwama katika mji huo uliozingirwa lazima kupewe kipau mbele kutokana na wasi wasi kwamba wanakabiliwa na mashambulizi ya kuukombowa mji huo.

Kwa mujibu wa tovuti huru ya Habari ya Alsumaria mwakishi wa sheikh huyo Ahmed al-Safi amesema katika hotuba aliyoitowa msikitini kwamba kumuokowa binaadamu asiyekuwa na hatia kutokana na madhara ni muhimu na adhimu kuliko hata kumlenga adui.

Hali ni mbaya kila uchao

Hali katika mji huo wa Fallujah inaelezwa kuwa inazidi kuwa mbaya kila uchao na licha ya kuwepo kwa mipango ya kuwafungulia njia za salama kwa wananchi kuondoka katika mji huo ni wachache wameweza kukimbia vita hivyo vya Fallujah katika siku za hivi karibuni.Kundi kubwa lilifanikiwa kuondoka hapo Ijumaa.

Wapiganaji wanaoiunga mkono serikali nchini Iraq.
Wapiganaji wanaoiunga mkono serikali nchini Iraq.Picha: Getty Images/AFP/A. Rubaye

Kwa upande wa pili wa mpaka nchini Syria mji wa Raqa unaotumiwa na kundi la Dola la Kiislamu kama mji mkuu wao pia umekuwa chini ya mashambulizi mazito. Hakuna mtu anayetembea nje na mashambulizi ya anga yamekuwa yakifanywa na majeshi ya muungano unaongozwa na Marekani na pia mashambulizi ya Urusi na vikosi vya serikali.

Muungano wa wapiganaji wa Kiarabu na Wakurdi umeanzisha operesheni ya kuukombowa mji huo ambao watu wanaokadiriwa kufikia 300,000 bado wanaishi na wanahangaika kutafuta upenyu wa kuukimbia mji huo.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/dpa/

Mhariri : Yusra Buwayhid