1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Raia waangukia mhanga wa mashambulio Afghanistan

Shirika la Msalaba mwekundu lakosoa ukosefu wa usalama na shida zinazowakumba wananchi wa kawaida nchini Afghanistan

default

Vikosi vinavyoongozwa na Marekani nchini Afghanistan vimewauwa,bila ya kukusudia,askari polisi sabaa wa Afghanistan ,kufuatia shambulio la wataliban dhidi ya wanajeshi wa Afghanistan.Wakati huo huo shirika la kimataifa la Msalaba mwekundu limeonya dhidi ya madhara ya hujuma za madege ya kivita kwa maisha ya watoto.

Mbali na polisi hao sabaa waliouliwa kwa makosa,wengine 13 hawajulikani waliko kufuatia kisa hicho kilichojiri jana usiku katika mkoa wa Khogiani katika jimbo la Nangahar linalopakana na Pakistan.

Msemaji wa jeshi la Marekani amesema amearifiwa juu ya tukio hilo lakini hana maelezo zaidi.

“Shambulio hilo la jeshi la wanaanga la nchi shirika zinmazoongozwa na Marekani limetokea baada ya wataliban kuhujumu vituo vya polisi na kutumwa wanajeshi ziada katika wakati ambapo vikosi vya Marekani vilikua vimeombwa kusaidia” amesema hayo mkuu wa polisi wa eneo hilo Adel Balwal.

Msemaji wa wataliban amesema kwa simu,wanaharakati wao wamewauwa askari polisi 12.

Sambamba na hayo wanajeshi wa jumuia ya kujihami ya magharibi NATO wamewauwa raia watatu wa Afghanistan jana katika mkoa wa Kunar.Wengine wawili wamejeruhiwa.

Zaidi ya waafghanistan 120 wameuliwa na wanajeshi wa kigeni miezi ya hivi karibuni.

Shirika la kimataifa la Msalaba Mwekundu limesema hii leo hali imezidi kua mbaya miongoni mwa jamii katika kipindi cha mwaka mmohja uliopita na raia wanazidi kuangukia mhanga wa mashambulio na hujuma za madege ya vikosi vya nchi shirika.

“Raia wanasumbuliwa vibaya sana na hali hii ya kuzidi mashambulio na vitisho vyenginevyo ikiwa ni pamoja na miripuko inayozikwa chini ya ardhi,mashambulio ya watu wanaojitolea mhanga maisha na mashambulio ya madege ya vikosi vya nchi shirika.

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa harakati za shirika la kimataifa la Msalaba Mwekundu Pierre Krähenbühl ,huduma za afya zimepooza katika maeneo ya mbali ya Afghanistan ambako mahitaji ya kimsingi ni shida kuyatekeleza.Bwana Krähnebühl amekosoa ukosefu wa usalama nchini Afghanistan.

Ukosefu wa usalama na umuhimu wa kuimarishwa demokrasia ni miongoni mwa lawama zilizotolewa hivi karibu na muakilishi maalum wa umoja wa mataifa kuhusu Afghanistan Tom König.

Mwenyewe lakini rais Hamid Karzai anasema.

„Tumeshaanza kuzungumza na jumuia ya kimataifa na mataifa jirani kwa lengo la kuimarisha amani nchini Afghanistan.Na tumeafikiana.Hakuna haja ya kuingiwa na wahka.Uamuzi tumeufikia katika baraza la wawakilishi-Jirga.“

Wakati huo huo Holland inafikiria mustakbal wa wanajeshi wake nchini Afghanistan.Waziri mkuu Jan Peter Balkenende akiwa ziarani mjini Ottawa Canada amesema nchi yake itaamua mwezi Agosti ujao kama wanajeshi wake wataendelea kuwepo Afghanistan baada ya mwaka 2008.

 • Tarehe 12.06.2007
 • Mwandishi Oummilkheir
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHCn
 • Tarehe 12.06.2007
 • Mwandishi Oummilkheir
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHCn

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com