1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rafael Correa ashinda muhula wa tatu Ecuardo

18 Februari 2013

Rais wa Ecuardo Rafael Correa amepata ushindi katika uchaguzi wa Jumapili, na kuimarisha udhibiti wa serikali kwa uchumi wa nchi hiyo, na kuuongezea nguvu muungano wa viongozi wakisoshalisti katika Amerika ya Kusini.

https://p.dw.com/p/17ftS
Rais Rafael Correa akisherehekea na makamu wake Jorge Glass baada ya kupata habari za ushindi.

Kiongozi huyo wa mrengo wa kushoto mwenye haiba kubwa alikuwa na asilimia 57 ya uungwaji mkono, ikilinganishwa na asilimia 24 ya mshindi wa pili Guillermo Lasso, baada ya asilimia karibu 40 ya kura kuhesabiwa. Tume ya uchaguzi ilisema haikutarajia matokeo kubadilika kwa kiasi kikubwa. Lasso alikubali kushindwa na kumpongeza Correa. Correa aliwambia wafuasi wake waliokuwa wanashingilia akiwa katika ubaraza wa ikulu, kuwa hakuna anayeweza kuyazuia mapinduzi, na kwamba mataifa ya kikoloni hayana tena udhibiti wa nchi hiyo.

Rais Correa akihutubia wafuasi wake akiwa katika ubaraza wa Ikulu mjini Quito pamoja na makamu wake Jorge Glass siku ya Jumapili.
Rais Correa akihutubia wafuasi wake akiwa katika ubaraza wa Ikulu mjini Quito pamoja na makamu wake Jorge Glass siku ya Jumapili.Picha: Reuters

Msingi wake wa ushindi

Mpiganaji huyo, ambaye ni mtaalamu wa uchumi aliesomea nchini Marekani alichukua madaraka kwa mara ya kwanza mwaka 2007 na amekonga nyoyo za wa Ecuardo wengi wa tabaka la chini kutokana na kutumia mapato makubwa yatokanayo na uuzaji wa mafuta kujenga barabara, shule na hospitali katika maeneo ya vijijini na maeneo ya mabanda poromoka ambako maskini wengi wa mijini wanaishi.

Ecuardo pia ilifanya uchaguzi wa wabunge ambao matokeo yake hayatatangazwa kwa siku kadhaa, lakini Correa aliiambia Televisheni ya Amerika Kusini ya Telesur, iliyoanzishwa na Chavez na washirika wake kama mbadala kwa vyombo vingine vilivyokuwepo, kuwa ana uhakika chama chake kitapata ushindi na kumuwezesha kuendelea na mipango yake ya mageuzi bila kujadiliana na wapinzani.

Sauti mpya dhidi ya Marekani?

Rais huyo mwenye umri wa miaka 49 anaweza kugeuka kuwa sauti kuu ya upinzani dhidi ya Marekani, na kiongozi asiye rasmi wa kanda ya ALBA inayoundwa na serikali za mrengo wa kushoto, wakati ambapo Hugo Chavez yuko kimya kutokana na mapambano dhidi ya ugonjwa wa saratani. Correa haoni haya kuanzisha mapambano hata kama yanahusu wamiliki wa hati za dhamana, makampuni ya mafuta, mabenki ya ndani, Kanisa Katoliki au vyombo vya habari vinavyokosoa sera zake. Aliahidi siku ya Jumapili kupanua udhibiti wa serikali kwa makundi ya vyombo vya habari alivyoviita mbwa na wauaji wa kukodi.

Ukosoaji wake wa Marekani na kupishana kauli na wawekezaji wa kigeni na Benki ya Dunia vimeongeza umaarufu wake kama kiongozi imara inayeweza kusimama dhidi ya nguvu kutoka nje, ambazo wengi wanasema zimeingilia masuala ya ndani ya Ecuardo kwa miongo kadhaa. Alipamba vichwa vya habari kimataifa mwaka uliyopita alipompa hifadhi mwanzilishi wa mtandao wa Wikileaks, Julian Assange. Wakosoaji wanasema alifanya hivyo kukwepa shutuma za kuzuia uhuru wa kujieleza nchini Ecuardo.

Mgombea wa upinzani na mshindi wa pili Guillermo Lasso.
Mgombea wa upinzani na mshindi wa pili Guillermo Lasso.Picha: Reuters

Baada ya ushindi

Changamoto kuu inayomkabili itakuwa kuvutia wawekezaji wanaohitajika kuongeza uzalishaji wa mafuta na kuchochea sekta ya madini. Kushindwa kulipa deni la dola bilioni 3.2 mwaka 2008 na majadiliano ya kishari ya mikataba ya mafuta yaliwatisha wengi. Wakosoaji wanamuona Correa kama kiongozi mbabe ambaye amezuia uhuru wa habari, na kuwateua wasaidizi wake katika nafasi za juu katika idara ya mahakama.

Lakini upinzani uliogawanyika ulishindwa kufua dafu kwake, na wagombea wake saba walifanya ushindi wa Correa kuwa rahisi zaidi, na sasa anaelekea kutimiza muongo mzima katika ikulu ya taifa hilo, ambako marais watatu wameondolewa ofisini kupitia mapinduzi au maandamano katika muongo moja kabla ya yeye kuchukua madaraka mwaka 2007.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre, ape, dpae
Mhariri: Daniel Gakuba