1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Qatar: Mwaka mmoja tangu mzozo wa Ghuba uanze

5 Juni 2018

Mwaka mmoja umemalizika tangu nchi 4 za kiarabu kukata uhusiano na Qatar na kuiwekea vikwazo vya kiuchumi na kisiasa. lakini Qatar imefaulu licha ya vikwazo hivyo.

https://p.dw.com/p/2yyCO
Katar Frau vor der Skyline von Doha
Picha: picture-alliance/AP Photo/K. Jebreili

Ni mwaka mmoja sasa tangu nchi nne za kiarabu kukatiza uhusiano wao wa kidiplomasia na Qatar. Hata hivyo Qatar ambalo ni taifa dogo la Ghuba limefaulu kuendeleza shughuli zake na kukabili athari kidogo zilizotokana na mzozo huo.

Siku kama ya leo, mwaka mmoja uliopita, nchi za Saudi Arabia, Misri, Bahrain na Umoja wa Falme za Kiarabu, ziliiwekea Qatar vikwazo vya kiuchumi na kisiasa huku zikiilaumu kuwa inawaunga mkono na kuwafadhili magaidi. Madai ambayo Qatar iliyakanusha.

Mipaka ya baharini na ardhini kati ya Qatar na Rasi ya Ghuba zimeendelea kufungwa, safari za ndege kati ya Qatar na nchi hizo zilisitishwa na raia wa Qatar waliokuwa katika nchi hizo waliondolewa.

Nchi zilizokatika uhusiano w akidiplomasia na Iraq ni Saudi Arabia, Misri, Bahrain na Umoja wa falme za Kiarabu
Nchi zilizokatika uhusiano w akidiplomasia na Iraq ni Saudi Arabia, Misri, Bahrain na Umoja wa falme za KiarabuPicha: Picture alliance/Zumapress/APA Images/Stranger

Saudi Arabia ilisema ilichukua hatua hiyo kulinda usalama wake wa taifa na hatari za ugaidi na misimamo mikali. Saudi Arabia pia ililifunga tawi la kituo cha utangazaji cha kimataifa cha Qatar-Aljazeera mjini Riyadh.

Katika nchi ambayo inategemea uagizaji wa vyakula kutoka nchi za nje, kuna hofu kuhusu ikiwa kufungwa kwa mipaka kutasababisha uhaba wa chakula nchini Qatar.

IMF yasema Qatar imefaulu kudhibiti athari ndogondogo kufuatia mzozo huo

Licha ya nchi hizo nne kushikilia msimamo wao dhidi ya Qatar, shirika la Fedha Duniani, IMF lilisema mwezi uliopita kuwa athari ndogo ya moja kwa moja kiuchumi kwa Qatar kutokana na msimamo wa mataifa hayo zimedhibitiwa na kwamba ukuaji wa uchumi unaendelea.

Mnamo Juni 22, mwaka uliopita, kundi la nchi hizo nne zilizoongozwa na Saudi Arabia, liliwekea Qatar masharti 13, ikiwemo kulifunga shirika la habari la Aljazeera, isitishe uhusiano wake na Iran na iifunge kambi ya jeshi la Uturuki iliyoko nchini mwake. Wakaipa Qatar siku 10 ili itimize masharti hayo, lakini Qatar ilisema masharti hayo sio ya kawaida na hayawezi kutekelezwa.

Utajiri wa gesi asilia wa Qatar na uhusiano mwema na Iran na Uturuki umeiwezesha kudhibiti athari ambazo zingesababishwa na vikwazo dhidi yake
Utajiri wa gesi asilia wa Qatar na uhusiano mwema na Iran na Uturuki umeiwezesha kudhibiti athari ambazo zingesababishwa na vikwazo dhidi yakePicha: Reuters/Qatar News Agency

Saudi Arabia na washirika wake waliendelea kutoa vitisho vya kuongeza vikwazo. Julai 25 walitangaza orodha ya makundi 18 na watu wanaoshukiwa kuwa magaidi na wenye uhusiano na kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS pamoja na Qatar. Orodha ambayo baadaye ilitanuliwa na kuyajumuisha majina 90.

Utajiri wa gesi asilia wa Qatar 

Utajiri mkubwa wa gesi asilia wa Qatar na uhusiano wa karibu na nchi nyingine katika kanda hiyo umeiwezesha kuudhibiti mzozo huo na maisha ya kila siku kuendelea bila mabadiliko makubwa.     

Maghala ya vyakula vyao yaliyojaa bidhaa kutoka Saudi Arabia sasa yanajazwa na bidhaa kutoka Uturuki na Iran.

Nalo shirika la ndege la Qatar limelazimishwa kubadilisha safari zake ili kuepuka kutumia sehemu ya anga ya nchi hizo nne zilizoifungia safari za angani, baharini na ardhini.

Ujenzi wa maghorofa unaendelea sawa na viwanja vitakavyotumiwa katika mechi za soka la Kombe la Dunia mwaka 2020.

Mwandishi: John Juma/AFPE/DPAE/AP

Mhariri: Grace Patricia Kabogo