1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Qatar: Kuna mkwamo kwenye mazungumzo ya usitishaji vita Gaza

John Juma
14 Mei 2024

Waziri Mkuu wa Qatar ambaye pia ni waziri wa mambo ya kigeni, amesema kwa sasa kuna mkwamo kwenye mazungumzo ya usitishaji vita vya Gaza, kufuatia operesheni ya kijeshi ya Israel mjini Rafah.

https://p.dw.com/p/4fqbr
Mzozo wa Gaza | Israel yashambulia Mashariki mwa Rafah
Kulingana na Qatar swali la kuwaachilia huru mateka baada ya vita au vita vikiendelea ndilo chanzo cha mkwamo kwenye mazungumzo ya usitishaji vita Gaza.Picha: -/AFP

Akizungumza kwenye mkutano wa Kiuchumi huko Doha Qatar leo, mwanadiplomasia huyo mkuu wa Qatar, Mohammed bin Abdulrahman amesema kumekuwa na "tofauti ya kimsingi" kati ya pande mbili husika kwenye machafuko hayo.

Ameeleza kuwa upande mmoja unataka kumaliza vita kabla ya kuwaachilia mateka wote waliobaki, ilhali upande mwingine unataka mateka waachiliwe huru huku vita vikiendelea.

Kulingana na Abdulrahman, anaamini kwamba ikiwa mkwamo huo utasuluhishwa, basi makubaliano yanaweza kupatikana ndani ya siku chache zijazo.

Wiki iliyopita, Israel ilichukua udhibiti wa kivuko cha mpaka wa Rafah na Misri, operesheni ambayo imesimamisha usambazaji misaada muhimu kwa wakaazi wengi wa ukanda wa Gaza.

Soma pia: Zaidi ya watu 500,000 wakimbia mapigano Rafah, UN

Israel inatizama Rafah kama ngome ya mwisho ya wapiganaji wa Hamas, kundi lililofanya shambulizi baya mnamo Oktoba 7 kusini mwa Israel na kuua watu 1,200 na kuwashika mateka wengine 250.

Israel, Marekani na Umoja wa Ulaya huliorodhesha Hamas kuwa kundi la kigaidi.

Qatar, Misri na Marekani zimekuwa zikijaribu kupa makubaliano ya kutanzua mgogoro huo unaoendelea.

Mahakama ya ICJ kusikiliza ombi la Afrika Kusini dhidi ya Israel Alhamisi

Katika tukio jingine, mahakama ya juu ya Umoja wa Mataifa imesema itafanya vikao siku ya Alhamisi na Ijumaa kuhusu ombi la Afrika Kusini la kuweka amri ya dharura kwa Israel kusitisha mashambulizi yake ya Rafah.

Soma pia: Israel yafanya Kumbukumbu ya Siku ya Mashujaa

Kupitia taarifa, Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) ya mjini The Hague imesema itawasikiliza mawakili kutoka Afrika Kusini siku ya Alhamisi, ikifuatiwa na jibu la Israel siku inayofuata.

Mapema mwezi huu, Afrika Kusini iliwasilisha ombi katika mahakama ya ICJ ikiomba mahakama iamuru Israel kujiondoa mara moja na kusitisha mashambulizi yake ya kijeshi kule Rafah.

Mahakama ya ICJ kusikiliza ombi la Afrika Kusini dhidi ya Israel Alhamisi
Mahakama ya ICJ kusikiliza ombi la Afrika Kusini dhidi ya Israel AlhamisiPicha: Peter Dejong/AP Photo/picture alliance

Pia iliomba mahakama kuamuru Israel kuchukua "hatua zote madhubuti" kuwezesha misaada ya kibinadamu kufikishwa bila kuzuiwa huko Gaza.

Watu Nusu 450,000 wamekimbia mapigano Gaza katika siku za hivi karibuni

Katika siku za hivi karibuni, takriban watu 450,000 wameyakimbia makaazi yao kutoka Rafah na takriban 100,000 wamekimbia kaskazini mwa Gaza. Hayo ni kulingana na mashirika ya Umoja wa Mataifa yakisema hakuna mahali salama ndani ya eneo hilo.

Soma pia: Israel: Mapambano yanaendelea mashariki mwa mji wa Rafah

Kulingana na wizara ya afya ya Gaza inayodhibitiwa na Hamas, operesheni ya kijeshi ya Israel imewaua watu wasiopungua 35, 173.

Shirika la Afya Duniani WHO limeonyesha Imani yake na takwimu za vifo zinazotolewa na wizara hiyo, likisema walikuwa wanakaribia zaidi kuthibitisha ukubwa wa maafa, baada ya Israel kutilia shaka mabadiliko kwenye takwimu hizo.

Wiki iliyopita, wizara ya Afya ya Gaza iliainisha jumla ya vifo vya karibu 35,000 tangu Oktoba 7.

Mashirika ya Umoja wa Matafa yasema karibu watu nusu milioni wamekimbia Rafah katika siku chache zilizopita.
Mashirika ya Umoja wa Matafa yasema karibu watu nusu milioni wamekimbia Rafah katika siku chache zilizopita.Picha: AFP

Ilisema takriban 25,000 kati yao hadi sasa wametambuliwa kikamilifu, ambapo zaidi ya nusu yao walikuwa wanawake na watoto.

Soma pia: Hali ya kibinaadamu yazidi kuwa mbaya Gaza

Hii ilizusha madai ya Israeli kuhusu ukosefu wa usahihi kwani hapo awali Mamlaka ya Palestina ilikadiria kuwa zaidi ya Asilimia 70 ya waliouawa walikuwa wanawake na watoto.

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yamechapisha upya takwimu hizo hizo za Wapalestina.

Vyanzo: DPAE, AFPE, RTRE