1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Putin ataka wapiganaji binafsi kula kiapo kwa taifa

Lilian Mtono
25 Agosti 2023

Rais Vladimir Putin amesaini amri ya kiapo siku mbili baada ya taarifa za kifo cha kiongozi wa kundi binafsi la kijeshi la Wagner, Yevgeny Prigozhin, ikilenga kuwafanya wapiganaji kuwa watiifu katika kuilinda Urusi.

https://p.dw.com/p/4VadG
Rais Vladimir Putin wa Urusi ametia saini amri ya rais wa kuyataka makundi ya wapiganaji wa kibinafsi kula kiapo, baada ya kifo cha mkuu wa kundi la wapiganaji la Wagner, Yevgeny Prigozhin.
Makundi ya wapiganaji wa kibinafsi sasa yatalazimika kula kiapo cha utii wa kuilinda nchi yao kikamilifu.Picha: Sergei Bobylev/TASS/imago images

Amri hiyo ya rais iliyochapishwa kwenye tovuti ya ikulu ya Urusi, Kremlin aidha inayalenga makundi yanayochangia kutekeleza majukumu yaliyopewa vikosi vya jeshi na vitengo vya ulinzi wa kitaifa. Sehemu ya amri hiyo inasema ni lazima wapiganaji wawe watiifu kwa Shirikisho la Urusi na kufuata amri kutoka kwa makamanda na viongozi wao kutimiza wajibu wao kwa uangalifu mkubwa.

Waraka huo umesainiwa hii leo na rais Putin ikiwa ni miezi miwili baada ya Prigozhin kuongoza wapiganaji wake kufanya uasi dhidi ya uongozi wa juu wa Moscow. Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov alipouliza kuhusiana na mustakabali wa kundi la Wagner alisema tu kwamba kundi hilo halitambuliki kisheria na kwamba makundi kama haya ya wapiganaji binafsi yamezuiwa nchini Urusi.

Huku hayo yakiendelea, waziri mkuu wa Uingereza Rishi Sunak amewaambia waandishi wa habari akiwa North Yorkshire mchana wa leo kwamba taarifa za kiintelijensia zinaonyesha kwamba Yevgeny alikuwepo kwenye ndege iliyoanguka siku ya Jumanne, lakini akasisitiza kwamba kilicho muhimu zaidi ni Putin kusitisha vita vyake nchini Ukraine.

Sunak alisema " Tunafuatilia tukio hili tukio kwa karibu sana, tukishirikiana na washirika wetu kuangalia kile kilichotokea. Lakini suala la msingi hapa ni Putin kumaliza uvamizi wake haramu nchini Ukraine, unaosababisha mateso makubwa kwa watu."

Serikali ya Ujerumani kwa upande wake imesema inaamini kuna uwezekano kwamba ajali hiyo ya ndege iliyombeba Prigozhin ilipangwa. Msemaji wake Wolfgang Büchner amesema mjini Berlin kwamba mauaji hayo ya kikatili dhidi ya Prigozhin pengine si ya kushangaza, lakini akisisitiza kwamba serikali ya Ujerumani haikuwa inajua chochote kuhusiana na mazingira ya ajali hiyo.

Rais Alexander Lukashenko(kushoto) akiwa na rais Vladimir Putin katika picha iliyopigwa Julai 23, 2023 huko St. Petesburg, Urusi.
Belarus na Ursi wamekuwa washirika wa karibu na ushirika wao umezidi kuimarika hata baada ya Urusi kuivamia Ukraine. Picha: Alexander Demianchuk/TASS/dpa/picture alliance

Lakini, rais wa Belarus na mshirika wa karibu sana wa Putin Alexander Lukashenko haamini hata kidogo kama swahiba wake huyo amemuua Prigozhin. Anasema Putin ni mtu wa mahesabu, mtulivu sana na mzito anayefanya maamuzi juu ya maswala mengine yasiyo magumu sana. Kwa hivyo hadhani kama kashiriki katika kazi hiyo anayosema haikuwa ya kitaalamu.

Urusi yasifu namna ilivyoidhibiti Ukraine katika Rasi ya Crimea.

Huku hayo yakiendelea, Urusi imesifu kazi iliyofanywa na vikosi vyake vya anga baada ya kuzindungua droni 73 katika eneo inalolidhibiti nchini Ukraine la Rasi ya Crimea katika kipindi cha masaa 24. Crimea iliyoanyakuliwa na Urusi mwaka 2014 imekuwa ikilengwa na Kyiv katika kipindi chote cha uvamizi wa Urusi nchini humo lakini imekuwa ikishambuliwa zaidi katika wiki za karibuni.

Msemaji wa Kremlin Peskov amesema mifumo yote ya ulinzi angani inafanya kazi kikamilifu na kuongeza kuwa mara nyingine huwezi kuzuia uharibifu mdogomdogo. Alikuwa akijibu swali kuhusiana na mashambulizi haya ya karibuni kwenye eneo hilo la Rasi ya Crimea.

Soma Zaidi:Shambulio la droni laitikisa Crimea, ghala la silaha lalipuka 

Na kutoka huko Kyiv, rais Volodymyr Zelensky amekutana na waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Hakan Fidan mjini humo mchana wa leo na kujadiliana juu ya makubaliano ya nafaka kupitia Bahari Nyeusi ambayo Urusi imejitoa mwezi uliopita. Zelensky ameandika kupitia mtandao wa Telegram kwamba wamejadiliana masuala mengi ya muhimu, kuanzia maandalizi ya mkutano wa kilele wa Kimataifa wa Amani ulioandaliwa na Ukraine hadi kitisho kinachoibuliwa na vizuizi vya Urusi kwenye njia ya kupitisha nafaka kwenye Bahari Nyeusi.

Makubaliano hayo yaliyosimamiwa na Uturuki na Umoja wa Mataifa yaliruhusu upitishwaji salama wa nafaka kutokea Ukraine kupitia Bahari Nyeusi na Ankara imekuwa ikijaribu kuishawishi Moscow kurejea kwenye makubaliano hayo.