1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pompeo na mwenzake wa Bahrain kuizuru Israel

Yusra Buwayhid
18 Novemba 2020

Mawaziri wa mambo ya nje wa Marekani na Bahrain wanatarajiwa kuwasili Jerusalem Jumatano kushiriki mkutano maalumu na baada ya kusaini makubaliano ya kurudisha uhusiano wa kidiplomasia na waziri mkuu wa Israel.

https://p.dw.com/p/3lUYA
Bahrain | Besuch US-Außenminister Mike Pompeo
Waziri wa Mmabo ya Kigeni wa Marekani Mike Pompeo na mwenzake wa Bahrain Abdullatif al-Zayani walipokutana mwezi Agosti mwaka huu Picha: Reuters/Handout Bahrain News Agency

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Marekani na wa Bahrain; Abdullatif al-Zayani na Mike Pompeo wanatarajiwa kuwasili nchini Israel Jumatano, kushiriki mkutano maalumu kati ya nchi hizo tatu wakipokewa na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na waziri wake wa Mambo ya nje Gabi Ashkenazi huko mjini Jerusalemu.

Ni ziara ya kwanza rasmi kwa waziri huyo wa Bahrain nchini Israel tangu nchi hizo mbili ziliposaini makubaliano ya kurudisha uhusiano wa kidiplomasia miezi miwili iliyopita.

Al-Zayani ataandamana na ujumbe wa ngazi ya juu, ambao utafanya majadiliano ya kufuatia Makubaliano ya Abraham – yaliyosainiwa mwezi Septemba ambayo yalirejesha uhusiano wa kidiplomasia kati ya Israeli na Bahrain na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Pompeo kutembelea makaazi ya walowezi 

Israel | PK US-Außenminister Mike Pompeo
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani, Mike Pompeo alipoitembelea Israel mwezi Agosti 2020.Picha: picture-alliance/AP Photo/D. Hill

Kabla ya kukamilisha ziara yake nchini Israel, Pompeo pia atatembele eneo linalotengeneza mvinyo katika Ukingo wa Magharibi.

Itakuwa ni kwa mara ya kwanza mwanadiplomasia wa Kimarekani wa ngazi ya juu kuzuru makazi ya walowezi wa Kiyahudi katika Ukingo wa Magharibi.

Sehemu ya eneo hilo, iko kwenye ardhi ambayo Wapalestina wanadai iliibiwa kutoka kwao kama wakazi asili.

Muneef Traish, ni Mjumbe wa Baraza la Manispaa ya Al-Bireh mwenye uraia wa Marekani na anasema wanaiangalia ziara ya Pompeo kama hatua ya kuhalalisha shughuli za walowezi wa Kiyahudi.

"Kwa sababu anakuja kutembelea ardhi inayomilikiwa na raia wa Palestina ambao pia wenye uraia wa Kimarekani na badala ya kuiamrisha Israeli irudishe ardhi kwa raia wake wa Marekani yuko hapa kusherehekea umiliki wa nguvu wa ardhi hii na uwepo wa walowezi hawa," ameongeza Traish.

Mauer zwischen Pisgat Zeev und dem palästinensischem Anata
Sehemu ya makaazi ya walowezi wa kijahudiPicha: Getty Images/AFP/A. Gharabli

Eneo hilo liko kwenye sehemu inayokaliwa kwa nguvu na Israel katika Ukingo wa Magharibi na mataifa mengi yanaliangalia suala hilo kama ukiukaji wa sheria za kimataifa na kikwazo kikubwa cha kupatikana amani kati ya Wayahudi na Wapalestina.

Ziara hiyo ya Pompeo katika Ukingo wa Magharibi ni tofauti na misimamo ya tawala zilizopita za Marekani za vyama vyote viwili vya Republican na Democratic, ambazo zikikemea ujenzi huo wa walowezi wa Kiyahudi.

Pompeo anawasili Israeli hii leo kufuatia ziara yake ya barani Ulaya. Israeli ni nchi ya mwanzo anayoizuru kwenye ziara inayojumuisha nchi kadhaa za Mashariki ya Kati, ikiwa ni pamoja na Qatar, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu.