1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi inamuhoji mshukiwa wa shambulizi la Istanbul

Grace Kabogo
17 Januari 2017

Polisi nchini Uturuki wameanza kumuhoji mshukiwa mkuu wa shambulizi katika klabu ya usiku mjini Istanbul, wakati wa sherehe za mwaka mpya ambalo liliwauwa watu 39 na kuwajeruhi wengine kadhaa.

https://p.dw.com/p/2Vtu5
Istanbul Türkei mutmaßlicher Terrorist verhaftet
Picha: picture alliance/Zumapress

Vyombo vya habari vya Uturuki vimeripoti kuwa polisi wanamuhoji mshukiwa huyo mpiganaji wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS aliyetambuliwa kama raia wa Uzbekistan. Abdulkadir Masharipov alikamatwa jana usiku wakati wa operesheni maalum ya polisi katika wilaya ya Esenyurt, mjini Istanbul.

Shirika la habari la taifa, Anadolu limesema mwanaume mmoja kutoka Kyrgyzstan na wanawake watatu kutoka Somalia, Senegal na Misri pia wamekamatwa katika operesheni hiyo, huku mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka minne wa mshukiwa huyo akiwa amechukuliwa kwa uangalizi maalum. Katika nyumba hiyo, polisi wamefanikiwa kuchukua kiasi cha Euro 185,000 pamoja na silaha mbili.

Kituo binafsi cha televisheni cha NTV kimesema Masharipov na watuhumiwa wengine wanne wanahojiwa katika makao makuu ya polisi mjini Istanbul. Waziri Mkuu wa Uturuki, Binali Yildirim, amewathibitishia waandishi wa habari mjini Ankara kukamatwa kwa mshukiwa huyo.

Istanbul Türkei mutmaßlicher Terrorist verhaftet
Polisi wa Uturuki walioshiriki operesheni ya kumkamata Abdulkadir MasharipovPicha: picture alliance/AA/A.Coskun

''Mtuhumiwa anahojiwa na polisi na nina matumaini mahojiano yatawabainisha wale walio nyuma ya shambulizi hilo. Kuna taarifa nyingi, lakini zitatolewa baadae kwa sababu ya mchakato mzima wa upepelezi. Maafisa watatoa taarifa katika wakati muafaka,'' alisema Yildirim.

Mshukiwa akiri kuhusika katika shambulizi

Gavana wa Istanbul, Vasip Sahin amesema mshukiwa huyo amekiri kuhusika katika shambulizi hilo na kwamba alipata mafunzo nchini Afghanistan. Sahin amesema inaaminika kuwa mshambuliaji huyo aliingia nchini Uturuki Januari mwaka 2016. Kwa mujibu wa gavana huyo, alama za vidole za mtuhumiwa huyo zinafanana na za mtu aliyefanya mshambulizi.

Mkuu wa polisi anatarajiwa kutoa taarifa zaidi baadae leo. Shirika la Anadolu limesema polisi pia wameendesha msako katika jengo lilaloshukiwa kuwa na wafuasi wa IS kutoka Uzbekistan katika maeneo matano ya makaazi ya Istanbul na kuwakamata watu kadhaa.

Katika ukarasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu amewashukuru polisi pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani, Suleyman Soylu kwa kufanikisha mshukiwa huyo kukamatwa.

Türkei Istanbul - Festnahme des Attentäters aus der Silvesternacht
Eneo alikokamatwa Abdukadir MasharipovPicha: picture-alliance/Zuma Press/Depo Photos

Picha za kukamatwa kwa mshukiwa huyo zilizotolewa kwenye vyombo vya habari, zimeonyesha uso wake ukiwa umechubuka na ukitokwa na damu. Televisheni ya NTV imesema mshukiwa huyo alikuwa anapinga kukamatwa. Kikosi cha askari polisi 1,000 kiliandaliwa kwa ajili ya kuhakikisha Masharipov anakamatwa.

Kundi la IS lilidai kuhusika na shambulizi hilo lililotokea katika klabu hiyo ya usiku ya Reina, likisema kuwa mauaji hayo yamefanyika ikiwa ni katika kulipiza kisasi kutokana na jeshi la Uturuki kuendesha operesheni zake kaskazini mwa Syria. Masharipov amekuwa mafichoni tangu kutokea kwa shambulizi hilo. Wengi wa waliouawa katika shambulizi la Istanbul walikuwa ni raia wa mataifa ya kigeni, wengi wao kutoka Mashariki ya Kati.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/Reuters, AFP, AP
Mhariri: Iddi Ssessanga