PHUKET:Uchunguzi waendelea kwenye mabaki ya ndege iliyodondoka | Habari za Ulimwengu | DW | 18.09.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Habari za Ulimwengu

PHUKET:Uchunguzi waendelea kwenye mabaki ya ndege iliyodondoka

Wachunguzi wanaendelea kutafuta maiti zilizosalia kwenye mabaki ya ndege ya abiria iliyodondoka jana asubuhi ilipojaribu kutua kisiwani Phuket.Ajali hiyo ilisababisha vifo vya watu 89 wengi wao raia wa kigeni.Orodha ambayo si rasmi iliyotungwa na Wizara ya mambo ya nje ya Thailand inaonyesha kuwa baadhi ya waliopoteza maisha yao ni raia 6 wa Uingereza,3 wa Israel,2 wa Marekani ,2 wa Ufaransa,mmoja kutoka Austria na Ujerumani,Iran,Ireland na Sweden.Hata hivyo orodha hiyo haijakamilika kwani zaidi ya raia 30 wa kigeni bado hawajatambuliwa.Uongozi nchini Thailand unapanga kufanya tathmini ya shanga za urathi za maiti ambazo bado hazijatambuliwa kulingana na Meja Jenerali Santhan Chayanon.Ndege hiyo ya kampuni ya One Two Go inayotoza nauli za bei nafuu iliyokuwa na abiria 123 na wahudumu 7 ilikuwa ikielekea kisiwani Phuket kutoka mjini Bangkok pale ilipodondoka ilipojaribu kutua.Ndege hiyo iliteleza na kushika moto huku kukiwa na mvua kubwa na upepo mkali.

Kwa mujibu wa mazungumzo yaliyonakiliwa kati ya wahudumu wa usafiri wa ndege na rubani ,maafisa hao walimuarifu rubani Arief Mulyadi kutotua kwasababu ya upepo mkali ila alikiuka agizo hilo.Taarifa hizo zilitolewa na Mkurugenzi wa kitengo cha Usafiri wa ndege nchini humo Bwana Chaisak Ungsuwan aliyehojiwa na kituo cha televisheni cha Nation.

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com