1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Paul Kagame: Shujaa au Dikteta?

3 Aprili 2024

Wafuasi wa rais wa Rwanda Paul Kagame wanamchukulia kama mwokozi aliepambana kusitisha mauaji ya kimbari na kurejesha amani katika taifa hilo. Lakini wakosoaji wake wanamtuhumu kuingoza Rwanda kimabavu. Kagame ni nani?

https://p.dw.com/p/4eOUx
Rais wa Rwanda Paul KAgame
Rais wa Rwanda Paul KagamePicha: Trinidad Express Newspaper/AFP

Aprili 7, 2024, Rwanda inaadhimisha miaka 30 tangu kutokee mauaji ya kimbari yaliyosababisha vifo vya karibu watu 800,000. Paul Kagame alikuwa na umri wa miaka 36 tu wakati jeshi lake la waasi la Rwandan Patriotic Front (RPF) lilipowashinda Wahutu wenye itikadi kali ambao kwa muda wa siku 100 walikuwa wamewaua mamia kwa maelfu ya Watutsi. Hatua hiyo ilimfanya kuwa kiongozi mkuu wa nchi hiyo iliyokuwa imesambaratika na kukumbwa na janga baya zaidi lisiloelezeka.

Kagame alimwagiwa sifa kutoka kwa mataifa ya Magharibi ambayo yalidhamiria kujitakasa kwa kuwa yalishindwa kuchukua hatua wakati wa mauaji hayo na amekuwa akitajwa kama mtu aliyeufufua uchumi wa  Rwanda  ambapo pato la taifa la limekuwa likikua kwa karibu asilimia nane kila mwaka.   

Rwanda - Paul Rusesabagina
Shujaa wa filamu ya "Hotel Rwanda" na mkosoaji wa serikali ya Kigali, Paul Rusesabagina akisindikizwa na Polisi kuelekea katika Mahakama mjini Kigali: 20.10.2020Picha: Clement Uwiringiyimana/REUTERS

Lakini rais huyo ameweka wazi nia yake ya kuzima ukosoaji na kumfuatilia mtu yeyote ambaye serikali yake inamchukulia kama adui wa taifa, akiwemo shujaa wa filamu ya "Hotel Rwanda" Paul Rusesabagina, ambaye aliwahi kusema kuwa Wanyarwanda ni "wafungwa katika nchi yao".   

Soma pia: Wanyarwanda 'ni wafungwa katika nchi yao': Rusesabagina

Mwandishi Philip Gourevitch ambaye aliandika historia kuhusu mauaji hayo ya kimbari, anaielezea haiba ya Kagame kama ya mtu mwenye kutumia mabavu na iliyojengeka kutokana na kukulia kwake uhamishoni. Familia ya Kagame ni watutsi waliolazimika kukimbilia nchini Uganda mnamo mwaka wa 1960 ili kuepuka mauaji ya halaiki.   

Wakimbizi hao walikabiliwa na ubaguzi na wengi wao walisajiliwa katika makundi ya waasi yaliyokuwa yakiongozwa na Yoweri Museveni. Baada ya Museveni kujinyakulia madaraka na kuwa rais mnamo mwaka 1986, Paul Kagame alipandishwa cheo na kuwa mkuu wa idara ya ujasusi nchini Uganda. Lakini hakukata tamaa ya siku moja kurejea nchi mwake.

Uasi wa RPF dhidi ya utawala wa Wahutu 

Kagame alipata mafunzo ya kijeshi nchini Marekani na Cuba na baadaye mnamo mwaka 1990 alichukua uongozi wa kikosi kidogo cha waasi ambao walilazimishwa kuikimbia Rwanda na ambao waliorejea nyumbani kwa siri wakiwa na nia ya kuupindua utawala wa wahutu chini ya rais Juvenal Habyarimana.      

Mabaki ya ndege iliyodunguliwa ya aliyekuwa rais wa Rwanda Juvenal Habyarimana
Mpiganaji wa Rwanda Patriotic Front (RPF) akiwa karibu na mabaki ya ndege iliyokuwa imembeba Rais wa Rwanda Juvenal Habyrimana iliyodunguliwa Aprili 6, 1994 mjini KigaliPicha: AP

Hatua hiyo ilipelekea kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe. Lakini janga baya zaidi lilishuhudiwa baadaye wakati ndege ya rais Habyarimana ilipodunguliwa mnamo Aprili 6 mwaka 1994, jambo lililopelekea Wahutu wenye itikadi kali kuanzisha chuki, vurugu na mauaji makubwa yaliyowalenga jamii ya walio wachache ya Watutsi na Wahutu wenye msimamo wa wastani waliochukuliwa kama wasaliti.

Soma pia: Wataalamu wa Umoja wa Mataifa waitia hatiani Rwanda kushirikiana na M23

Karibu watu 800,000 waliuawa wengi wao kwa kukatwakatwa kwa mapanga. Umwagaji damu uliodumu kwa siku 100 ulisitishwa baada ya wanamgambo wa Kagame wa RPF kuuteka mji mkuu wa Kigali.Huku hazina ya taifa ikiwa tupu kabisa, kundi hilo la waasi lililazimika kuijenga upya nchi hiyo kwa msaada mkubwa wa jumuiya ya kimataifa.

Harakati za vikosi vya Rwanda Mashariki mwa Kongo

Licha ya kundi la RPF kushutumiwa kwa kuwaua makumi ya maelfu ya watu katika nchini jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakati wakiwasaka wahusika wa mauaji ya halaiki, mataifa ya kigeni yalifumbia macho madai hayo. Mwaka 2012, Marekani ilisitisha msaada wake wa kijeshi kwa Rwanda baada ya serikali mjini Kigali kushutumiwa kuyafadhili makundi ya waasi mashariki mwa Kongo.

DRC | Waasi wa M23
Wapigani wa kundi la uasi la M23 wakijiondoa huko Kibumba karibu na Goma: 23.12.2022Picha: Arlette Bashizi/REUTERS

Mwaka 2023, Umoja wa Mataifa, Marekani na mataifa kadhaa ya Magharibi yaliishutumu waziwazi serikali ya Kagame kwa kuwaunga mkono waasi wa kitutsi wa M23 ambao wameteka maeneo makubwa ya jimbo la Kivu Kaskazini. Madai ambayo yamekuwa yakikanushwa na Rwanda inayosema kuwa Kongo huwahifadhi wanamgambo wa Kihutu wenye nia ya kuwashambulia.

Hata hivyo, alipoulizwa na gazeti la kila wiki la  The East African  katika mahojiano yaliyochapishwa mwezi Machi, iwapo kuna wanajeshi wa Rwanda nchini DRC, Kagame alisema kwamba iwapo usalama wa Rwanda utakuwa kwenye kitisho, haitaji ruhusa ya mtu yeyote kufanya lolote, na kuwa ni lazima ahakikishe kuwa Rwanda inalindwa.

Soma pia: UN yawawekea vikwazo waasi wa Kongo huku mapigano yakiendelea

Kumekuwa na ongezeko la ukosoaji kuhusu rekodi mbaya ya haki za binadamu nchini Rwanda huku wapinzani wakifungwa jela, kulazimishwa kukimbilia uhamishoni au kuuawa. Hii imempa nafasi Paul Kagame ambaye alikuwa rais wa Rwanda kwa mara ya kwanza mwaka 2000, kujishindia chaguzi tatu kwa kujipatia zaidi ya asilimia 90 ya kura na anatarajiwa pia kushinda tena katika uchaguzi wa urais mwezi Julai mwaka huu.

(Chanzo: AFPE)