1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis aikosoa sera ya Marekani ya uhamiaji

John Juma
20 Juni 2018

Papa Francis amesema anaunga mkono kauli za hivi karibuni za maaskofu wa kikatoliki wa Marekani waliotaja hatua ya kuwatenganisha watoto na familia zao kuwa kinyume na maadili au misingi ya kikatoliki na sio sawa

https://p.dw.com/p/2zxEp
Italien Papst Franziskus in Ostia
Picha: Getty Images/AFP/A. Pizzoli

Kiongozi wa kanisa Katoliki ulimwenguni Papa Francis ameikosoa sera ya utawala wa rais wa Marekani Donald Trump ya kuwatenganisha watoto wa wahamiaji na wazazi wao katika mpaka wa Mexico, akisema kuwa umaarufu si suluhisho kwa changamoto ya uhamiaji duniani.

Akizungumza na shirika la habari la Reuters, Papa Francis amesema anaunga mkono kauli za hivi karibuni za maaskofu wa kikatoliki wa Marekani waliotaja hatua ya kuwatenganisha watoto na familia zao kuwa kinyume na maadili au misingi ya kikatoliki na sio sawa. Papa Francis ametilia uzito kauli hiyo kwa kuongeza kuwa suala la kutafutia uhamiaji suluhisho si rahisi lakini umaarufu si suluhisho.

Moja kati ya ujumbe wake mkuu ulihusu wasiwasi wake kwa sera hiyo ya rais wa Marekani Donald Trump isiyowakubali kabisa wahamiaji, ambapo maafisa wa Marekani wanapanga kuwahukumu wahamiaji wanaovuka mpaka wa Mexico bila vibali, kuwaweka kizuizini  washukiwa huku watoto wao wakipelekwa katika kambi za serikali.

Vyumba ambavyo watoto waliotenganishwa na wazazi wao wanaishi Marekani
Vyumba ambavyo watoto waliotenganishwa na wazazi wao wanaishi MarekaniPicha: Reuters/M. Blake

Ghadhabu dhidi ya sera ya uhamiaji Marekani

mezusha ghadhabu Marekani na imeshutumiwa kote ulimwenguni huku video na sauti za watoto waliotenganishwa na wazazi wao zinazoonyesha wakilia sakafuni katika vyumba ambavyo wamefungiwa zikisambaa katika mitandao ya kijamii.

Maaskofu wa kikatoliki nchini Marekani wameungana na viongozi wa dini nyingine kuishutumu sera hiyo ya Trump. Na Papa Francis ameungana na kuheshimu msimamo wa maaskofu hao.

Kauli za Papa zinaongeza shinikizo kwa Trump kuhusu sera yake ya uhamiaji. Papa anaongoza takriban waumini bilioni 1.3 ulimwenguni kote na ndiyo dini kubwa zaidi ya Kikristo Marekani.

Hata hivyo Rais Trump ametetea vikali hatua ambazo utawala wake umezichukua huku akielekeza lawama kwa Wademocrats.

Uteuzi wa maaskofu wa China

Papa Francis na maaskofu wa Chile mnamo Mei 17, 2018 Vatican
Papa Francis na maaskofu wa Chile mnamo Mei 17, 2018, VaticanPicha: Reuters/Vatican Media

Katika mahojiano hayo ambayo ni nadra na yaliyogusia masuala kadhaa, Papa amesema ana matumaini kuhusu mazungumzo, yatakayopelekea makubaliano ya kihistoria ya kuteua maaskofu kutoka China na ameongeza kuwa anaweza kuwakubalia maaskofu zaidi wanaojiuzulu kufuatia kashfa za dhuluma za kimapenzi kwa watoto nchini Chile.

Kuhusu uongozi wake wa miaka mitano kama papa mjini Vatican, alitetea mbinu yake ya uongozi wa kanisa Katoliki dhidi ya ukosoaji kutoka kwa wahafidhina walioko ndani na nje ya kanisa wanaosema mafundisho yake ni ya kiliberali sana.

Kadhalika Papa amesema anataka kuwateua wanawake kushikilia nyadhifa za juu katika uongozi wa kanisa Katoliki Vatican. Kwa sababu wanawake wako bora katika kusuluhisha mizozo.

Kuhusu afya yake, Papa amesema kando na maumivu ya mguu yanayofungamana na maumivu ya mgongo, ana afya nzuri. Alirejelea kauli yake punde alipochaguliwa kuwa huenda angejiuzulu kutokana na hali ya kiafya jinsi mtangulizi wake alivyofanya mwaka 2013, lakini kwa sasa hilo halipo kwenye fikra zake.

Mwandishi: John Juma

Mhariri: Yusuf Saumu