1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa ajisikia "aibu" vijana kurithi dunia iliyogawika

Sekione Kitojo
31 Machi 2018

Kiongozi wa kanisa Katoliki Papa Francis jana Ijumaa  amesema "anaona aibu"  kwamba vizazi vijavyo vitarithi dunia "iliyogawika  na vita".

https://p.dw.com/p/2vHAk
Vatikan Karfreitag - Papst betet Kreuzweg
Picha: Reuters/S. Rellandini

Akizungumza  mjini  Roma mwishoni  mwa utamaduni  wa  vituo vya  Ijumaa  kuu  katika  njia  inayopita msalaba, kiongozi  huyo  wa kidini  alisema  dunia "inatafunwa na ubinafsi ambamo  vijana, wagonjwa na wazee wanatengwa".

Vatikan Karfreitag - Papst betet Kreuzweg
Papa Francis akitoa hutoba baada ya utaratibu wa utamaduni wa njia ya msalaba siku ya Ijumaa kuuPicha: Getty Images/AFP/M. Bertorello

Huku  kukiwa  na  ulinzi  mkali, kiasi  ya  waumini 20,000 , wengi wao wakibeba  mishumaa, walikusanyika  kuzunguka ukumbi wa kale wa makumbusho  mjini  Roma kwa  ajili  ya  kanuni  hiyo  ya  kidini ambayo ni kurudiwa kwa  njia  ambayo  Yesu  alipitia kuelekea katika  kusulubiwa. Mji  mkuu  wa  Italia umewekwa  katika  uangalizi mkubwa  kufuatia  wiki  ambayo  iligubikwa  na  wimbi  la  kukamatwa kwa watu  wanaosadikiwa  kuwa  ni  magaidi.

Waziri  wa  mambo  ya  ndani  wa  Italia  Marco Minniti  alionya  wiki hii kuhusu  kitisho  cha  hali  ya  juu  cha  shambulio  nchini  italia, na kiasi  ya  polisi  10,000 waliwekwa  kuhakikisha  usalama  mjini Roma, hususan wakati  wa  sikukuu  ya  pasaka  zinazosimamiwa na  papa mwishoni  mwa  juma  hili  na  kufikia  kilele kwa  sherehe za  Pasaka siku  ya  Jumapili.

Papa  aliwaongoza  Wakatoliki  katika  sala  ya Ijumaa kukiwa  na ulinzi  mkali , na  kuwataka  watu, ikiwa  ni  pamoja  na  viongozi katika  kanisa, kutafakari  kiwango cha  kujisikia  aibu  kwa  jukumu walilonalo  katika  madhila  ya  dunia.

Vatikan Karfreitag - Papst betet Kreuzweg
kituo kimojawapo katika njia ya msalaba katika ukumbi wa kale wa Colosseum mjini RomaPicha: Getty Images/AFP/M. Bertorello

Tujisikie aibu

Francis  alielekeza matamshi  yake, aliyotoa mwishoni  mwa  njia hiyo  ya  msalaba  huku watu wakiwa  wameshika  mishumaa, katika muktadha wa  kujisikia  aibu  na  kutubu, kulikonasibishwa  na taswira ya  dunia  ya  kisasa  ambako, fahari, kiburi na ubinafsi mara  nyingi  hukandamiza ubinadamu  na ukarimu.

Akizungumza  kwa  sauti ya  unyenyekevu, alizungumzia  kuhusu "aibu kwa sababu  watu  wengi, hata  baadhi  yenu , watumishi  wa Mungu , wamejiweka  kuamuliwa na  matamanio na sifa ya ushindi, na  hivyo  kupoteza thamani yake."

Tangu  kuchaguliwa  kwake mwaka  2013, Francis mara  nyingi amewataka mapadre  na  maaskofu  wa  Katoliki  kuishi  maisha ya kawaida, kuwatumikia  wengine, na  sio kutafuta  ukubwa  katika kanisa  ama  katika  jamii  kwa  jumla.

Vatikan Karfreitag 2018
Papa Francis alala chini akiomba wakati wa sherehe za upendo wa Mungu katika Ijumaa kuu katika kanisa la Mtakatifu Petro mjini Roma Ijumaa ya tarehe 30 Machi 2018Picha: Getty Images/AFP/A. Solaro

Ijumaa Kuu  siku ya  utulivu  na  unyenyekevu  mkubwa  katika kalenda  ya  Wakristo, ni  kumbukumbu  ya  siku  Biblia  inasema Yesu  alisulubiwa. Njia  ya  msalaba  ina matukio  14, yanayoitwa vituo, kutoka  enzi  za  gavana  wa  Roma  Pontius Pilate alipomhukumu  Yesu  kifo  hadi  kuzikwa  kwake  katika  kaburi.

Francis  amesema  watu  wengi  duniani  hii  leo wanapaswa kujisikia "aibu kwa  kupoteza hisia  za  aibu",  na  kuongeza  kwamba aibu inaweza  kuonekana  kuwa " hisani  2 kutoka  kwa  Mungu. Amesema wengi wanapaswa kujisikia  aibu kwa sababu  kizazi  chetu kinawaacha  vijana katika  dunia  ambayo  imepata nyufa kwa migawanyiko  na  vita, dunia iliyotafunwa  na  ubinafsi..

Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre, afpe

Mhariri: Daniel Gakuba