1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pande zinazohasimiana zabadilishana wafungwa Yemen

Angela Mdungu
14 Aprili 2023

Pande mbili zinazohasimiana katika mzozo wa Yemen zimeanza kubadilishana zaidi ya wafungwa 800 leo.Taarifa hiyo ni kwa mujibu wa kamati ya kimataifa ya msalaba mwekundu

https://p.dw.com/p/4Q3y4
Jemen Sanaa Airport | Gefangenenaustausch
Picha: KHALED ABDULLAH/REUTERS

Hatua hiyo iliyopigwa ni muhimu ili kujenga uaminifu wakati wajumbe wa Saudi na kundi la waasi wa Houthi wakiendelea na mazungumzo ya kutafuta amani.

Kamati ya kimataifa ya msalaba mwekundu ICRC, inayosimamia mchakato huo wa kubadilishana wafungwa imesema ndege zake ndizo zitakazotumika kuwabeba wafungwa walioachiliwa kati ya miji sita ya Yemen na Saudi Arabia.

Akizungumzia hatua hiyo naibu waziri wa haki za binadamu wa serikali inayotambuliwa kimataifa ya Yemen Majed Fadail amesema ndege hizo zitawabeba wafungwa waliokuwa wakishikiliwa kwa muda mrefu na waasi wa Ki Houthi wanaoungwa mkono na Iran.Awamu mbili za kuwasafirisha wafungwa hao kutoka pande zote zimeanza leo kati ya Aden na Sanaa. 

Wafungwa wengine huenda wakaachiliwa

Pande zinazohasimiana katika mzozo huo wa Yemen, zilikubaliana kuwaachili wafungwa 887 katika majadiliano yaliyofanyika Uswisi mwezi uliopita. Zilikubaliana pia kukutana tena kwa mara nyingine mwezi Mei mwaka huu ili kujadili  kuwaachilia wafungwa wengine.

Mgogoro huo ambao umekwishauwa maelfu ya watu na kusababisha wengi kutumbukia kwenye baa la njaa, umekuwa ukionekana kama vita vinavyochochewa na mataifa ya  Saudi Arabia na Iran

Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia uliingilia kati vita nchini Yemen mwaka 2015 baada ya wahouthi kuiondoa serikali mjini Sanaa mwaka 2014. Saudi Arabia na Iran, zilikubaliana mwezi uliopita kurejesha uhusiano wa kidiplomasia uliovunjika mwaka 2016. Jambo hilo limeleta matumaini kuwa huenda juhudi za kutafuta amani nchini Yemen zikawa na mafanikio.

Soma zaidi:Pande mbili zinazozozana Yemen zaanza mazungumzo

Jemen Sanaa Airport | Gefangenenaustausch
Wafungwa walioachiliwa wakiwasili uwanja wa ndege wa SanaaPicha: KHALED ABDULLAH/REUTERS

Jana Alhamisi, wawakilishi wa Saudi walihitimisha mazungumzo ya amani mjini Sanaa pamoja na wawakilishi wa wahouthi ambapo maafisa wao walionesha kuwepo kwa hatua nzuri. Wawakilishi hao wa wahouthi waliongeza kuwa, mazungumzo zaidi yanahitajika ili kuondoa tofauti zilizosalia.

Vita nchini Yemen, imeshasababisha vifo vya zaidi ya watu 150,000 wakiwemo wapiganaji na raia na kuufanya mzozo huo kuwa moja kati ya migogoro mibaya zaidi ya kibinadamu duniani.

Chanzo: RTR/AFP