1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Oscar Pistorius aachiwa kwa dhamana

8 Desemba 2015

Mwanariadha wa Afrika Kusini Oscar Pistorius amepewa dhamana akisubiri kuhukumiwa kwa mauaji ya mpenzi wake Reeva Steenkamp mnamo mwaka wa 2013

https://p.dw.com/p/1HJ7R
Südafrika Anhörung Oscar Pistorius
Picha: Reuters/S. Sibeko

Pistorius anahitajika kulipa dhamana ya kiasi cha Randi 10,000 akisubiri kikao cha kumhukumu mnamo Aprili 18 mwaka ujao.

Jaji Aubrey Ledwaba ameiambia mahakama kuwa hakuna hatari yoyote kwamba mwanariadha huyo mlevamu anaweza kutoroka ikiwa atapewa dhamana kwa sababu alijiwasilisha mahakamani mwenyewe leo.

Kwa sasa bingwa huyo wa Olimpiki ataendelea kutumikia kifungo cha nyumbani na atakuwa na kifaa cha kumfuatilia kielektroniki. Anaruhusiwa kuondoka nyumbani kati ya saa moja asubuhi hadi saa sita mchana katika eneo lisilozidi kilomita 20 kutoka nyumba anamoishi. Aidha amesalimisha pasipoti yake kwa mahakama.

Anakabiliwa na hukumu ya kifungo cha zaidi ya miaka 15 jela, ingawa jaji huenda akampunguzia hukumu. Bingwa huyo wa Olimpiki alirejea mahakamani leo baada ya mahakama ya rufaa kubatilisha uamuzi wa awali wa mahakama uliompata na hatia ya kuuwa bila kukusudia na badala yake ikaagiza ahukumiwe upya kwa mauaji. Alikiri kumuua mpenzi wake, Reeva Steenkamp, Februari 2013 lakini akasema alidhani alikuwa ni mwizi aliyevamia nyumbani kwake.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Sekione Kitojo