1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Opereshini za kijeshi zaingia awamu ya mwisho Mali

20 Februari 2013

Jeshi la Ufaransa na lile la Mali,limeanzisha hujuma katika milima ya Ifoghans kaskazini.Wanajeshi 2 wa Ufaransa wameuwawa.Raia wa Ufaransa wametakiwa waondoke kaskazini ya Camerun.

https://p.dw.com/p/17hpJ
Wanajeshi wa Mali na UfaransaPicha: picture alliance / dpa

Wanajeshi karibu 150 wa Ufaransa na wenzao wa Mali wameanzisha hujuma katika milima ya Adrar,katika eneo la Ifoghans ambako ghala mbili za silaha za waasi zimeripuliwa.

Mwanajeshi mmoja wa Ufaransa ameuwawa katika hujuma hizo zilizopelekea pia kuvunjwa nguvu wanamgambo 20 wa itikadi kali."Tunabidi tuendelee.Hii ni awamu ya mwisho ya ukombozi wa Mali,tukisubiri vikosi vya wanajeshi wa Afrika vitakaposhika nafasi ya vikosi vya Ufaransa" amesema waziri wa ulinzi wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian aliyeitaja awamu hiyo kuwa ngumu kupita kiasi.

Akiwa ziarani mjini Athens nchini Ugiriki rais Francois Hollande wa Ufaransa aliyezungumzia pia kuhusu kuuliwa mwanajeshi huyo wa pili wa Ufaransa tangu opereshini za kijeshi zilipoanza january 11 mwaka huu,amesema mapigano makali yamezuka kati ya kikosi maalum cha jeshi kiitwacho Legionaire na wanamgambo wa itikadi kali ya dini ya kiislam."Tunabidi tupigane mpaka mwisho,mpaka watakapokamatwa viongozi wa mwisho wa makundi ya magaidi waliojificha katika maeneo ya mbali kabisa ya kaskazini nchini Mali."Amesema rais Hollande aliyeashiria pia jeshi la Ufaransa limeaingia katika awamu ya mwisho ya opereshini zake nchini Mali.

Wafaransa wametakiwa wawe macho

Kamerun / Waza Nationalpark / Entführung
Mbuga ya wanyama ya Waza, nchini Camerun,karibu na mahala wafaransa sabaa walikotekwa nyaraPicha: picture-alliance/dpa

Wakati huo huo wizara ya mambo ya nchi za nje ya Ufaransa imewatolea wito wafaransa wote walioko kaskazini ya Camerun walihame haraka eneo hilo na kuhamia sehemu nyengine,baada ya familia moja ya watu sabaa,ikiwa ni pamoja na watoto wanne kutekwa nyara jana katika eneo hilo na akuhamishiwa Nigeria.

Wanamgambo wa itikadi kali wa Nigeria,Boko Haram wanatuhumiwa kuhusika na kuiteka nyara familia hiyo ya kifaransa.

Wafaransa zaidi ya elfu sita wanaishi nchini Camerun ambako makampuni zaidi ya 200 yanasimamia shughuli za kuchimba mafuta,misitu,kutengeneza saruji ,simu za mimono na kadhalika.

Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Ufaransa imewasihi pia raia wake wasitembelee maeneo ya mpakani ya Tchad na Camerun,na eneo lote linalopakana na ziwa Tchad,

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP

Mhariri:Yusuf Saumu