1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Olympiki: Henry Wanyoike ataiwakilisha vipi Afrika ya Mashariki

27 Julai 2012

Wakati mwanariadha wa Kenya, Henry Wanyoike, alipoanza kukimbia katika miaka ya 1980, hakuwaza kuwa siku moja atakuwa akikimbia na kuingia katika kinyangányiro cha Olympiki.

https://p.dw.com/p/15fDA
Henry Wanyoike akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya DW.
Henry Wanyoike akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya DW.Picha: DW

"Nilipoteza uwezo wa kuona, lakini sijapoteza maono yangu". Ni maneno ya Henry, ambaye hapo awali alikuwa mshona viatu. Sasa ni miongoni mwa wanariadha maarufu wa marathon, ambaye amekwishaweka rekodi tatu za dunia, licha ya upungufu alionao.

Katika maeneo mbalimbali ya dunia leo hii, jina Henry Wanyoike, si geni. Kijana huyu alizaliwa mwaka 1974 katika makazi ya watu masikini Kanjeru, maeneo yanayokaliwa na watu wa kabila la Kikuyu nchini Kenya. Leo hii, Henry amejipatia umaarufu mkubwa na mafanikio si haba katika ulimwengu wa riadha.

Mwezi Mei, mwaka 1995, miaka miwili baada ya kuhitimu elimu ya shule ya sekondari, Henry Wanyoike, akapata upofu baada ya kuugua ugonjwa wa kiharusi, ambao uliharibu neva zake za macho.

"Niliugua kiharusi mwaka 1995. Tarehe mosi, nilienda kulala, ilipofika usiku, kama mtu mwingine yeyote. Na nilipoamka siku iliyofuata, nilikuwa naona giza nene. Tangu siku hiyo, miaka 17 imepita sasa, sijawahi kuiona dunia." Wanyoike anaongeza.

Henry Wanyoike akiwa mazoezini.
Henry Wanyoike akiwa mazoezini.Picha: DW

Christoffel Blindenmission imechangia sana kumjenga Henry

Baada ya mlolongo wa ushauri nasaha na matibabu katika Hospitali ya Misheni inayoendeshwa na Christoffel Blindenmission (CBM), Wanyoike alijiunga na Taasisi ya Ufundi ya Machakos, iliyoanzishwa kwa ajili ya watu wasioona kwa ajili ya kupewa huduma zaidi za matibabu. Hapo, alijifunza kujitegemea mwenyewe na alifanikiwa kurejea tena katika fani ya riadhao.

Ni hapo ndipo alipoamua kushiriki katika michezo ya olyimpiki na baada ya kukimbia katika Siku ya Olympiki, akawa mmojawapo wa wanariadha waliochujwa ili kuunda timu ya taifa mwaka 2000, ili kushiriki katika michezo ya Paralympics nchini Australia, ambapo kirahisi tu, aliibuka kidedea na kukabidhiwa medali ya dhahabu katika mbio za mita 5,000.

Tangu kipindi hicho, Henry amekuwa akifanya vizuri katika mashindano ya kitaifa na kimataofa na katika riadha ya marathon kwa watu wazima na wale wenye ulemavu pia.

Makazi yake yamepambwa na medali za kila aina na ametambuliwa kwa mafaniko hayo ndani ya Afrika na duniani kwa ujumla.

"Nilipoanza kukimbia, ilikuwa ngumu sana kwa watu kuelewa ni kwa jinsi gani mtu asiyeona anaweza kukimbia. Si watu wengi waliamini kuwa ningeweza kukimbia. Mpaka ikafikia wakati, baadhi yao wakasema kwamba ninajifanyisha kuwa ni kipofu, kwa sababu hawajawahi kuona kitu kama hicho awali nchini Kenya.Na haikuwa rahisi kuwaelewesha kuwa hata watu wenye ulemavu pia wanaweza kufanya mambo mengi maishani." Kijana huyo anaendelea.

Kwa msaada wa Joseph Kibunja, ambaye ni rafiki yake tangu utotoni, Wanyoike amefanikiwa kutimiza ndoto yake ya kuwa mwanariadha bingwa wa dunia. Kibuja anaeleza jinsi alivyoungana na Henry.

Henry Wanyoike ni nyota inayongáa Afrika Mashariki.
Henry Wanyoike ni nyota inayongáa Afrika Mashariki.Picha: DW

Anasema alimfahamu Wanyoike tangu akiwa na miaka 10. Wamekuwa marafiki tangu kipindi hicho mpaka alipopata upofu na kuamua kujiunga na Chuo cha Ufundi cha Machakos, kwa ajili ya watu wasioona.Na aliporejea nyumbani akitokea Sydney, ambapko alituzwa medali yake ya kwanza ya dhahabu, aliniomba niambatana nae.

Henry Wanyoike ameshiriki katika shughuli nyingi za kutoa misaada nchini Kenya hususan kuwasaidia watu maskini, watu wenye ulemavu mbalimbali na makundi mengine yasiyopewa kipaumbele nchini humoAnafanya kazi pamoja na CBM, Shirika la the Boris Becker, Light for the World na shirika lake yeye mwenyewe, Henry Wanyoike Foundation.

Ana matumaini makubwa zaidi

Licha ya ukweli kwamba Henry amepoteza uwezo wa kuona, matarajio na ndoto zake bado zingali hai na hamu ya kutaka kuzitimiza zote bado inachemka moyoni mwake.

"Nilipoteza uwezo wa kuona lakini sijapoteza maono yangu kwa sababu namshukuru Mungu ninatimiza ndoto zangu zote nilizokuwa nazo maishani.", anaweka mambo hadharani.

Kupitia shirika lake, Henry amefanikiwa kutembelea shule nyingi na kuwatia moyo watu wenye ulemavu. Yeye ni mume wa mke mmoja na baba mwenye watoto wanne. Ni mkulima na hutumia muda wake kuwalisha ngómbe zake na kuwakamua maziwa.

Henry Wanyoike anataka kuuonesha ulimwengu kuwa hata watu wenye ulemavu nao wanaweza kufanya mambo ya maana na kuwa wenye kutekeleza majukumu yao katika jamii waishimo.

Mwandishi: Alfred Kiti

Mtafsiri: Ndovie, Pendo Paul

Mhariri: Sekione Kitojo