1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Olmert hana tamaa ya muwafaka wa amani mwaka huu

Othman, Miraji29 Julai 2008

Olmert anasema ugumu wa amani mwaka huu uko katika Jerusalem

https://p.dw.com/p/Elpt
Rais George Bush wa Marekani akimkumbatia waziri mkuu wa Israel, Ehud OlmertPicha: AP

Waziri mkuu wa Israel, Ehud Olmert, amesema nchi yake na Wapalastina hawataweza kuafikiana mwaka huu juu ya mkataba wa amani ambao utaingiza suala gumu la mustakbali wa mji wa Jerusalem. Hata hivyo, mbele ya bunge la nchi yake, alielezea matumaini kwamba pande hizo mbili huenda zitaweza kutanzua tafauti zao juu ya masuala mengine kuhusu mzozo wao huo uliodumu miongo kadhaa.

Ehud Olmert aliondosha uwezekano wa kupatikana maafikiano jumla ifikapo mwisho wa mwaka huu, licha ya ahadi zilizotolewa na pande mbili hizo katika mkutano uliosimamiwa na Rais George Bush wa Marekani huko Annapolis, mwaka jana, na ambao uliyafufua mazungumzo ya amani ya Mashariki ya Kati. Licha ya kusema kwamba hakuna uwezekano wa kufikia muwafaka juu ya mustakbali wa mji wa Jerusalem, hata hivyo, alisema kuna nia ya kuweko utaratibu ambao utaendelea kulishughulikia suala hilo kwa kipindi kirefu zaidi hadi pale yatapatikana maelewano ambayo yatakubaliwa na pande mbili hizo. Alisema Israel na Wapalastina huenda wakaweza kukubaliana mwaka huu juu ya masuala ya mipaka na wakimbizi.

Mjini Washington, msemaji wa serekali ya Marekani, Dana Perino, alisema ikulu ya nchi yake itaendelea kuyasukuma mambo mbele ili mapatano yafikiwe mwisho wa mwaka huu.

Israel iliiteka sehemu ya mashariki ya mji wa Jerusalem inayokaliwa na Waarabu, ukiwemo mji wa kale na mwahala patakatifu kwa Wakristo, Waislamu na Wayahudi, katika vita vya mwaka 1967, na muda mfupi baadae ukaitwaa sehemu hiyo. Israel imeutangaza mji huo mzima kuwa ni mji mkuu tena wa daima usiogawika wa Israel, dai ambalo halijawahi kutambuliwa na jamii ya kimataifa au na Wapalastina ambao wanataka Jerusalem ya Mashariki uwe mji mkuu wa dola yao ya baadae. Wapalastina wameyapinga matamshi hayo ya Ehud Olmert, wakisema hawatayakubali maafikiano ambayo hayataiingiza Jerusalem. Msemaji wa wa Rais Mahmud Abbas wa Wapalastina, Nabil Abu Rudeina, amesema Jerusalem ni msatri mwekundu wa serekali ya ndani ya Wapalastina na wananchi wa Kipalastina, na wao hawako tayari kurejea nyuma hata nchi moja. Alisema Jerusalem ya Mashariki ni mji mkuu wa dola ya Kipalastina na matamshi ya Olmert ni jaribio la kuzikimbia ahadi zilizotolewa katika mkutano wa Annapolis, na ile fikra ya Rais Bush. Aliitaka serekali ya Marekani iisukume Israel iingie katika mashauriano ya kweli na iache kupoteza wakati.

Mwanzoni mwa mwezi huu, Ehud Olmert alisema Israel na Wapalastina hawajawahi kuwa karibu sana kufikia makubaliano kama ilivyo sasa. Inasemakana Olmert amekubali kurejesha asilimai 92.7 ya ardhi ya Wapaalstina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wote wa Gaza. Pia amependekeza mabadilishano ya asilimia 5.3 ya ardhi kwa ajili ya makaazi makubwa ambayo Israel inataka kubakia nayo kama sehemu ya mapatano yeyote. Mahmud Abbas ametaka arejeshewe Ukingo mzima wa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza, lakini maafisa wanasema huenda atakubali asilimia 1.5 hadi asilimia mbili ya ardhi ili pande mbili hizo zibadilishane, ambapo Wapalastina watapewa fidia ya ardhi kutoka Israel ya sasa. Ehud Olmert anataka mapatano ya baadae yataje kwamba Israel ni nchi ya Wayahudi, na Palastina ni nchi ya Wapalastina. Utaratibu huo utawanyima Wapalastina kile wanachokiona kuwa ni haki yao ya kurejea makwao katika yale maeneo ambayo yamegeuka kuwa dola ya Israel hapo mwaka 1948.