Odinga akatisha ziara yake Cote d′Ivoire | Matukio ya Kisiasa | DW | 20.01.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Odinga akatisha ziara yake Cote d'Ivoire

Kupatikana suluhu katika mzozo wa kisiasa Cote d'Ivoire yanafifia, baada ya mpatanishi wa Umoja wa Afrika katika mzozo huo, Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga kuamua kukatisha ziara yake ya saa 48 mjini Abidjan hii leo.

default

Waziri mkuu wa Kenya Raila Odinga akatisha ziara yake nchini Cote d'Ivoire

Msemaji wa Raila Odinga, Salim Lone amesema kuwa waziri huyo mkuu wa Kenya anatarajiwa kuondoka mjini Abidjan baada ya ziara yake ya saa 48 kutopata majibu sahihi kuhusu swali la nani anatakiwa kuiongoza Cote d'Ivoire. Bwana Lone amesema Odinga jana alikuwa akiwasiliana na kiongozi anayeng'ang'ania madaraka katika taifa hilo la Afrika Magharibi, Laurent Gbagbo na mpinzani wake Alassane Ouattara anayetambuliwa kimataifa kama mshindi wa uchaguzi wa mwezi Novemba, mwaka uliopita, lakini hadi sasa hakuna jambo muhimu ambalo limejitokeza.

Bwana Odinga alitarajiwa kwenda moja kwa moja Accra, Ghana leo baada ya Jumatatu kusema kuwa atakwenda kwa mazungumzo nchini humo pamoja na Angola na Burkina Faso. Pendekezo la mazungumzo lilitolewa siku ya Jumatatu, huku viongozi wa kanda hiyo wakiimarisha msimamo wao wa kujiingiaza kijeshi ili kuondoa hali hiyo ya mkwamo. Awali, Gbagbo alisema yuko tayari kufanya mazungumzo na mpinzani wake, lakini amekataa ahadi zote alizopewa ili aondoke madarakani, ikiwemo ya kwenda kuishi uhamishoni na kupewa kinga ya kutoshtakiwa kwa makosa ya uhalifu dhidi ya ubinaadamu.

Mpatanishi huyo wa mzozo wa kisiasa nchini Cote d'Ivoire awali alikuwa na matumaini ya ziara yake ya sasa na anasubiri majibu yaliyotolewa Jumatatu. Lone amefafanua kuwa Bwana Odinga hana tena mpango wa kurudi Cote d'Ivoire, hadi atakapohitajika kufanya hivyo. Aidha, mwenyekiti wa Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi-ECOWAS, ambaye pia ni rais wa

Nigerias Präsident Goodluck Jonathan

Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria ambaye pia ni mwenyekiti wa ECOWAS

Nigeria, Goodluck Jonathan amesema katika taarifa yake kuwa jumuiya hiyo inataka kupatikana suluhuhisho kwa njia ya amani.

Hata hivyo, ameongeza kusema kuwa hawajabadilisha msimamo wao walioutangaza kwenye kikao chao kilichopita, kuwa huenda wakatumia nguvu za kijeshi iwapo itahitajika kufanya hivyo. Rais Jonathan amefafanua kwamba kura za wananchi lazima zihesabiwe mara baada ya kupigwa, la sivyo demokrasia haitakuwepo barani Afrika. Naye afisa wa ngazi ya juu wa ECOWAS, Olusegun Petinrin amesema wako tayari kutumia nguvu iwapo itahitajika na kwamba lazima hilo lieleweke wazi. Nao wakuu wa majeshi katika nchi za Magharibi mwa Afrika wanakutana kwa siku mbili ikiwa ni katika kukamilisha mpango wa kijeshi wa kumuondoa madarakani Gbagbo kinguvu. Angola kwa upande wake imetoa msimamo wake kuhusu mzozo wa kisiasa wa Cote d'Ivoire.

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Michelle Alliot-Marie ameonya matumizi ya nguvu yatumike tu kama hatua ya mwisho kabisa, kwa sababu yanaweza kukasababisha maafa makubwa zaidi. Zaidi ya watu 200 wameuawa katika mapigano tangu kumalizika kwa uchaguzi. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo linatarajiwa kupiga kura ya kuamua iwapo ipeleke wanajeshi 2,000 zaidi nchini Cote d'Ivoire baada ya Urusi kupinga. Hata hivyo, kuongezwa kwa wanajeshi hao kunahofiwa kunaweza kuhatarisha zaidi hali ya mambo kutokana na Gbagbo mara kadhaa kuvitaka vikosi vya Umoja wa Mataifa kuondoka nchini humo. Endapo wanajeshi wengine watapelekwa, basi kutakuwa na hadi wanajeshi 11,500.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/afp

Mhariri: Saumu Mwasimba

 • Tarehe 20.01.2011
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/zzbC
 • Tarehe 20.01.2011
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/zzbC

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com