1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama kwenda Jordan

22 Machi 2013

Rais Barack Obama wa Marekani baadae leo anakwenda Jordan, ambapo pamoja na mambo mengine, atakuwa na mazungumzo na Mfalme Abdullah wa Pili.

https://p.dw.com/p/182Qj
Rais Obama akiweka shada la maua kwenye kaburi la Theodor Herzl
Rais Obama akiweka shada la maua kwenye kaburi la Theodor HerzlPicha: Getty Images

Ziara ya Jordan anaifanya baada ya kukamilisha ziara yake Israel ambapo ameuzuru kaburi la Yitzhak Rabin na pia atatembelea Kanisa la Bethlehemu huko Palestina. Mazungumzo kati ya Rais Obama na Mfalme Abdullah wa Pili wa Jordan yatahusu zaidi vita vya wenyewe kwa wenyewe katika nchi jirani ya Syria na matarajio ya Israel na Palestina kurejea katika meza ya mazungumzo ya amani.

Ziara hiyo ina lengo la kuihakikishia Jordan kwamba Marekani inaiunga mkono katika wakati huu inapokabiliwa na wimbi la wakimbizi kutoka Syria na mzozo wa kiuchumi uliosababishwa na vuguvugu la mageuzi katika utawala kwenye mataifa ya Kiarabu. Jordan imewapokea karibu wakimbizi 436,000 wa Syria na idadi hiyo inaweza ikaongezeka hadi 700,000 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Obama kumuhimiza Mfalme Abdullah kuhusu mageuzi ya kisiasa na kiuchumi

Afisa wa Marekani amesema Rais Obama anatarajiwa kumuhimiza Mfalme Abdullah wa Pili kuendelea na mpango wa kufanya mageuzi ya kiuchumi na kisiasa. Aidha, amesema Marekani inashirikiana kwa karibu kabisa na serikali ya Jordan, kama sehemu ya nchi ambayo inawaunga mkono waasi wa Syria kuushinikiza utawala, na kuujenga upinzani. Rais Obama amesema Marekani inachunguza madai kuwa silaha za kemikali zilitumika wakati wa mzozo wa Syria.

Kabla ya kuelekea Jordan, Rais Obama amekamilisha ziara yake Israel na Palestina kwa kuzuru makaburi ya Waziri Mkuu wa zamani wa Israel, Yitzhak Rabin na shujaa wa nchi hiyo, Theodor Herzl, kwa kuweka mashada ya maua kwenye makaburi hayo. Kiongozi huyo wa Marekani, atatembelea pia kituo cha kumbukumbu ya mauaji ya Wayahudi cha Yad Vashem. Rais Obama atakutana na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ambaye tayari walishafanya mazungumzo baada ya kuwasili Jerusalem siku ya Jumatano.

Azuru Bethlehemu

Kisha, atatembelea Kanisa la Uzawa la Bethelemu katika Ukingo wa Magharibi, ambalo kwa utamaduni Wakristo wanalichukulia kama sehemu aliyozaliwa Yesu Kristo. Akizungumza jana na wamafunzi wa Jerusalem, Rais Obama aliwataka wanafunzi hao kuanzisha amani kwa kutatua masuala ya kikanda yanayotishia taifa lao na kwamba mataifa mawili, ndio suluhisho pekee la kuhakikisha Israel inabakia kama taifa la Kiyahudi, licha ya mabadiliko ya idadi ya watu.

Kanisa la Bethlehemu
Kanisa la BethlehemuPicha: Reuters

Afisa mwandamizi wa Palestina, amesema kuwa Rais wa Mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas ameridhishwa na hotuba ya Rais Obama. Kiongozi huyo alilaani vitisho vinavyoendelea vya mashambulizi kutoka kwa kundi la Hamas katika Ukanda wa Gaza, baada ya maroketi mawili kushambulia kusini mwa Israel karibu na mji wa Sderot. Rais Obama, akizungumza mbele ya Rais Abbas, amesema suluhisho la mataifa mawili bado linawezekana, licha ya madai kuwa ujenzi wa makaazi unaofanywa na Israel umeharibu ndoto za Wapalestina.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE,DPAE
Mhariri: Josephat Charo