1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama kuhutubia mkutano mkuu leo.

28 Agosti 2008

Barack Obama atawataka Wamarekani leo kujiunga nae katika harakati za mabadiliko ya kisiasa, katika azma yake ya kuwania kuwa rais wa Marekani kwa tikiti ya chama cha Democratic.

https://p.dw.com/p/F6Op
Barack Obama akiwa na mgombea mwenza Joseph Biden katika mkutano mkuu wa uteuzi wa chama cha Democratic mjini Denver, Colorado.Picha: AP

Barack Obama atawataka Wamarekani leo Alhamis kujiunga nae katika harakati za mabadiliko ya kisiasa , wakati akijiweka katika njia kuelekea kukamilisha historia ambapo atateuliwa rasmi kuwa mgombea wa kiti cha urais kwa tikiti ya chama cha Democratic katika mkutano mkuu wa chama hicho.

Seneta Obama , mwenye umri wa miaka 47, ambaye baba yake ni Mkenya , atajitokeza leo Alhamis na kutoa hotuba yake ya kukubali kuteuliwa kwake na mkutano mkuu.

Seneta huyo kutoka jimbo la Illinois atakubali rasmi uteuzi huo akiwa Mmarekani wa kwanza mwenye asili ya Afrika kuwa mgombea katika uchaguzi wa rais nchini humo kutoka moja kati ya chama kikubwa, mbele ya zaidi ya watu 70,000 watakaokuwa katika uwanja wa mpira huko Colorado.

Matukio ya kihistoria yatakuwa kila mahali, hotuba ya Obama itafanyika wakati wa kumbukumbu ya mwaka wa 45 wakati ambapo mwanaharakati mashuhuri wa kupigania haki za Waafrika nchini Marekani Martin Luther King alipotoa mtazamo wake kuhusu hali ya baadaye ya usawa wa kijamii katika hotuba yake maarufu ya I have a dream. Nina ndoto.

Kukitarajiwa kuwashwa fashifashi baada ya hotuba yake, Obama atakuwa amejiweka katika njia ya mpambano halisi na mgombea wa chama cha Republican John McCain mwezi Novemba ambapo maoni yanaonyesha kuwa mpambano utakuwa wa vuta nikuvute.

Wakati jioni hiyo itakuwa yenye kila aina ya shamra shamra, Obama anafahamu kuwa anapaswa kuwasogelea wapigakura wa Marekani ambao wanahangaika kila siku kupata riziki kutokana na hali mbaya ya kiuchumi, na ambao wamekuwa wakipinga vita vya Iraq.

Hotuba hii haihusiani na Barack Obama , badala yake inahusiana na raia wa Marekani na mwelekeo unaohitajika kuchukuliwa, kuitoa nchi hiyo katika shimo iliyomo hivi sasa, amesema msaidizi mwandamizi wa Obama , David Axelrod.

Katika wakati wa kihistoria chama cha Democratic jana kilimteua rasmi Obama kuwa mgombea wa chama hicho katika uchaguzi wa rais, katika hali ya umoja, matumaini na hisia kali. rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton alikuwa mmoja wa mazungumzaji katika mkutano huo mkuu jana na alikuwa na haya ya kusema.

Barack Obama alisababisha wajumbe wa mkutano kushangilia kwa nguvu wakati alipojipenyeza bila kutarajiwa katika mkutano huo siku moja kabla , baada ya hotuba muhimu iliyotolewa na mgombea mwenza Joseph Biden pamoja na hotuba ya idhinisho kutoka kwa rais wa zamani Bill Clinton. Obama aliwasalimu wajumbe wa mkutano huo kwa ahadi ya kukutana nao hii leo tena.

Obama alipata rasmi kuwa mgombea wa chama cha Democratic wakati hasimu wake mke wa rais wa zamani Bill Clinton, Hillary Clinton alipositisha rasmi juhudi zake za kuwania nafasi hiyo katika kampeni ambayo ilikuwa na mivutano mikubwa na kutishia kukigawa chama cha Democratic, hapo mwezi May. Mgombea mwenza Biden alimsifu Obama , baada ya mtoto wake wa kiume Beau aliposababisha mke wa Obama kumwaga machozi kwa kumsifu ushujaa wa baba yake baada ya ajali ya gari iliyosababisha kifo cha mke wa kwanza wa seneta huyo na mtoto wake wa kike mwaka 1972.

►◄