Obama ayaunga mkono mageuzi ya Arabuni | Matukio ya Kisiasa | DW | 20.05.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Obama ayaunga mkono mageuzi ya Arabuni

Rais Barack Obama ametoa hotuba maalum ya sera za nje za Marekani na kusema kuwa nchi yake inayaunga mkono mageuzi yanayofanyika sasa katika Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika.

Rais Barack Obama

Rais Barack Obama

Akizungumza kwenye wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani jijini Washington, Rais Obama alisema kuwa Marekani inapaswa kubadili sera zake ili iweze kukabiliana na mabadiliko yanayotokea katika nchi za Kiarabu.

Rais Obama amesema sera ya kipaumbele kwa Marekani sasa ni kuyaunga mkono mageuzi yanayotokea katika nchi za kiarabu na Kaskazini mwa Afrika. Obama amesema Marekani inapinga matumizi ya nguvu yanayoelekezwa kwa watu wanaopinga ukandamizaji.

Waandamanaji wa Kipalestina katika siku ya Nakba

Waandamanaji wa Kipalestina katika siku ya "Nakba"

Ameeleza kuwa sasa pana fursa ya kihistoria kwa Marekani ya kuonyesha kwamba inathamini zaidi maadili yaliyoonyeshwa na mchuuzi wa Tunisia aliyejitia moto kuliko, mamlaka ya madikteta.

Akisisitza juu ya harakati za kupigania haki za kidemokrasia katika nchi za Kiarabu na Kaskasini mwa Afrika Obama amesema kuwa Marekani inaunga mkono mageuzi ya sehemu hizo. Ameeleza kuwa Marekani inayaunga mkono mageuzi ya kiuchumi na kisiasa yanayofanyika katika nchi za Kiarabu na Kaskazini mwa Afrika

Rais Obama amesema nchi yake itasimama kidete kuunga mkono maendeleo ya kidemokrasia na ya kiuchuni nchini Misri na Tunisia. Na kwa ajili hiyo Rais huyo ametangaza mpango mpya wa msaada wa kiuchumi kwa Misri na Tunisia ikiwa pamoja na kuzisaidia serikali mpya za nchi hizo kuzirejesha mali zilizowekwa nchi za nje kwa njia ya rushwa. Amesema Marekani itazisaidia nchi hizo kuzirejesha mali zilizoibiwa na kufichwa nje. Kiongozi huyo wa Marekani ameziita nchi hizo kuwa ni mfano wa eneo linaloshuhudia mabadiliko.

Obama ameeleza kuwa matukio ya nusu mwaka uliopita yameonyesha kwamba mikakati ya ukandamizaji haifanyi kazi tena.

Rais Obama alikuwa anazungumza kwenye wizara ya mambo ya nje ya Marekani jijini Washington katika hotuba ndefu juu ya mapinduzi yanayotokea katika Mashariki ya kati na Kaskazini mwa Afrika. Amesema Marekani na nchi za Kiarabu zinapaswa kushirikiana ili kuondoa hali ya kutoaminiana iliyokuwapo kwa muda wa miaka mingi na hivyo kuweza kuujenga mustakabali mzuri.

Ameonya kwamba ikiwa Marekani itashindwa kubadili sera zake panaweza kutokea kizungumkuti cha mfarakano baina yake na jamii za Kiislamu.

Katika hotuba yake Rais Obama pia alizungumzia juu ya uhusiano baiana ya Israel na Wapalestina. Amesema Marekani haitakubali Israel itengwe kwenye Umoja wa Mataifa mnamo mwezi wa septemba. Amesema mpango wowote juu ya kuundwa taifa la Wapalestina lazima uwe katika msingi wa mipaka ya kabla ya mwaka wa 1967 na uwe katika msingi wa mapatano baina ya Israel na Wapalestina lakini pia amesisitiza msimamo wa Marekani juu ya kuulinda usalama wa Israel. Ametamka kwamba msimamo huo hautatetereka.

Ameeleza wazi kwamba, juhudi za wapalestina za kujaribu kuuondoa uhalali wa Israel zitashindikana. Amesema hatua za kujaribu kuitenga Israel kwenye Umoja wa Mataifa mnamo mwezi wa Septemba hazitaunda taifa huru la Wapalestina.

Mwandishi: Abdu Mtullya/RTRE/AFP

DW inapendekeza

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com