1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Timu Yetu

Nyota mpya yachomoza Ukraine

Matokeo ya mwanzo ya uchaguzi uliofanywa siku ya Jumapili nchini Ukraine,huonyesha kuwa muungano wa vyama vinavyoelemea kambi ya Magharibi unaongoza.Hata hivyo inatazamiwa kuwa vyama hivyo vitakuwa na majadiliano makali kuhusu mwongozo wa serikali mpya.

Kiongozi wa upinzani,Yulia Tymoshenko akipiga kura yake katika uchaguzi wa bunge la Ukraine

Kiongozi wa upinzani,Yulia Tymoshenko akipiga kura yake katika uchaguzi wa bunge la Ukraine

Inadhihirika kuwa vyama vilivyohusika na Mapinduzi ya Rangi ya Machungwa nchini Ukraine, vitarejea tena madarakani.Lakini pia kuna ishara kuwa Rais Viktor Yushchenko aliehusika na maandamano makuu ya mwaka 2004 anazidi kupoteza mamlaka yake.Yushchenko ni rais aliechaguliwa baada ya maandamano ya maelfu ya watu kuleta mageuzi ya kisiasa nchini Ukraine.Lakini kiongozi huyo aliependwa na mamilioni,sasa amepoteza umaarufu wake.Kwani kwa mujibu wa matokeo ya mwanzo ya uchaguzi wa siku ya Jumapili,chama chake cha „Ukraine Yetu“ kimepata asilimia 16 ya kura.Kwa upande mwingine,chama cha Viktor Yanukovych,hasimu wa Mapinduzi ya Rangi ya Machungwa,kimejinyakulia kama asilimia 31 ya kura zilizohesabiwa.

Lakini nyota mpya kuchomoza katika siasa za Ukraine,ni Yulia Tymoshenko anaeongoza kwa asilimia 33.Tymoshenko alikuwa mshirika mkuu wa Mapnduzi ya Rangi ya Machungwa na alikuwa waziri mkuu,lakini alifukuzwa na Yushchenko baada ya miezi saba tu.Sasa yaonekana kuwa hatima ya kisiasa ya Ukraine imo mikononi mwake.Pindi ataungana na Yushchenko basi vyama vyao vitakuwa na wingi wa kutosha bungeni kuweza kuunda serikali.Asipofanya hivyo basi Yanukovych pamoja na muungano wa vyama vingi vidogo ataweza kuunda serikali ya mseto.

Ukraine iliyokuwa na chaguzi tatu katika kipindi cha miaka mitatu na kwa miezi kadhaa serikali kushindwa kufanya kazi,ni maarufu kwa mizozano ya kisiasa yenye utata.Lakini kuhusu uchaguzi wa Jumapili,kiongozi wa tume ya wachunguzi wa uchaguzi wa Umoja wa Ulaya,Adrian Severin amesema:

„Kuambatana na yale niliyoona,naweza kusema kuwa licha ya kuwepo hitilafu fulani,uchaguzi huu umefikia au tuseme umekaribia viwango vya Ulaya.“

Lakini baadhi ya wachambuzi wa kisiasa wanauliza ikiwa Tymoshenko mwenye heba kubwa,ataweza kuweka kando tofauti za maoni zilizompambanisha na mshirika wake Yushchenko.Wanasema,Yanukovych na muungano wa vyama yake kwa kushinda hadi hivi sasa asilimia 33 ya kura,bado ni kitisho.

Uchaguzi wa Jumapili uliitishwa mapema,baada ya Yushchenko na Yanukovych kushindwa kuafikiana. Yanukovych amekuwa waziri mkuu,baada ya muungano wa vyama vyake kuchomoza washindi wa chaguzi za bunge Machi mwaka 2006.Yanukovych anaungwa mkono na Urussi iliyo na uhusiano wa utata pamoja na Yushchenko na Tymoshenko.

Mabomba yanayosafirisha gesi ya Urussi hadi nchi za Umoja wa Ulaya hupitia Ukraine.Ukraine ni jamhuri ya zamani ya Soviet Union inayojaribu kufanya maageuzi ya kiuchumi na kisiasa mfano wa nchi za magharibi.Lakini nchi hiyo imegawika kati ya wale wanaozungumzwa Kirussi na kuelemea upande wa Urussi na wanaozungumza Kiukraine na huelemea kambi ya Magharibi.

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com