1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nusu ya Wakenya wako kwenye mkwamo wa kifedha - Utafiti

8 Februari 2024

Utafiti mpya wa kampuni ya Financial Services Monitor unaonesha nusu ya Wakenya wanakabiliana na mkwamo wa fedha na kuzongwa na madeni kwa sababu ya hali ngumu zaidi ya kiuchumi ikilinganishwa na hali kabla ya UVIKO-19.

https://p.dw.com/p/4cBj5
Hali ya Wakenya yazidi kuwa ngumu.
Hali ya Wakenya yazidi kuwa ngumu.Picha: DW

Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti huo, pato la Wakenya wengi limepunguwa, ambapo hata wale walioajiriwa wanalazimika kukimu mahitaji ya wazazi na watoto kwa mpigo.

Kwa upande mwengine, wajasiriamali ndio walioko katika hali mbaya ukizingatia mkwamo wa fedha.

Utafiti huo unaonesha kuwa, watu watano kati ya 10 - sawa na asilimia 48 - ya Wakenya wanazongwa na mkwamo wa fedha huku walio na kipato kidogo na wanawake wakikabiliana na hali ngumu zaidi.

Walio pabaya zaidi ni wale wanaopata mshahara wa kiasi ya shilingi za Kenya 20,000, sawa a dola 120 kwa mwezi, nusu yao wakielezea kupata msongo wa mawazo ikilinganishwa na wanaopokea kiasi ya shilingi 50,000 kwa mwezi.

Kadhalika asilimia 62 ya Wakenya wanapokea kiwango kilichopungua cha mshahara kuliko kabla ya janga la UVIKO-19 kutua.

Mishahara midogo kulinganisha na hali ya maisha

Asilimia 29 wanapokea mshahara ule ule ijapokuwa hali ya uchumi imekuwa ngumu na mfumko wa bei na ongezeko la gharama vikiendelea kuwa kikwazo kwa mteja. Kimsingi mifuko ya Wakenya imetoboka, kwa mujibu wa Brian Mwendwa, dereva jijini Nairobi.

“Mshahara wako ni uleule lakini matumizi yamezidi.Kama serikali ingeweza kuingilia kodi ikashuka kidogo isiwe tunakatwa kodi kupita maelezo kwani iko juu kuliko tunachopata.” Alisema kijana huyo.

Hali ya maisha ya raia nchini Kenya inazidi kuwa ngumu.
Hali ya maisha ya raia nchini Kenya inazidi kuwa ngumu.Picha: DW

Mwenzake, Vivian Atieno, aliiambia DW kwamba anaamini sarafu ya shilingi ya Kenya haina thamani tena. “Siku hizi pesa ni kitu ambacho hata hakina thamani.” Alisisitiza.

Soma zaidi: Nairobi. Wanarakati wapinzani wa utandawazi waandamana.

Kwa upande mwengine, utafiti huo wa Financial Services Monitor unaonesha walio na ajira wanajikuta njia panda kwani wanalazimika kukimu mahitaji ya wana wao ambao wanachukua muda mwingi zaidi kujisimamia na wazazi ambao wamekuwa watu wazima.
Idadi ya walio katika hali hii inaongezeka kwasababu watu wanaishi kwa muda mrefu zaidi kwa hiyo walioajiriwa hawapati nafasi mujarab ya kujiandaa kwa maisha baada ya kustaafu.

“Nikidhani kwa uvumilivu na kujikaza na kujaribu kupunguza matumizi yetu. Tusitegemee sana kuwa serikali itaingilia kwa kila jambo katika maisha yetu.” Alisema Joshua Mutua, mfanyabiashara ambaye kwa mtazamo wake serikali haiwezi kumnasua Mkenya wa kawaida.

Magonjwa ya akili na msongo wa mawazo

Hali yote hii huenda ikasababisha matatizo ya akili na afya kwa jumla kutokana na msongo wa mawazo na pia wahusika hawana bima maalum ya afya kugharamia matibabu.

Maandamano ya Wakenya
Maandamano ya Wakenya Picha: Monicah Mwangi/REUTERS

Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, utafiti huo umeashiria kuwa kiasi ya asilimia 40 wamelazimika kuomba mikopo kutoka kwa jamaa na marafiki huku asilimia 38 wakichovya kwenye buyu la akiba kukidhi mahitaji ya kila siku na ya dharura.Tathmini inabainisha kuwa Wakenya wengi wanakopa kulipa madeni jambo ambalo limekuwa la msingi kwa baadhi.

Kadhalika, asilimia 74 ya Wakenya hawana nafasi ya kujiandaa kwa maisha baada ya kustaafu kwani hela ni finyu ijapokuwa wanakiri ni jambo la msingi.

Soma zaidi: Tume ya uchaguzi Kenya yapendekeza mabadiliko.

Idadi isiyofikia nusu wanaamini watoto wao hawana uwezo wa kuwatazama watakapozeeka na asilimia 14 wanahisi kuwa ni wajibu wa serikali kukidhi mahitaji yao.

Nelson Mwangi, mfanyabiashara katika sekta ya magari ya umma ya matatu, alisema ongezeko la bei ya mafuta limeathiri biashara na maisha.

“Vile bei ya mafuta imekuwa ikiongezeka mwezi hadi mwezi,hilo limekuwa likituumiza sana kwasababu inachukua ile faida kidogo tunayopata.Hatuwezi kuwa kila mwezi bei ya mafuta ikiongezeka tunapandisha nauli kwani mteja naye pia anaumia.” 

Hali ngumu ya uchumi imezua tatizo jipya nalo ni ujasiriamali, mikataba mifupi ya kazi na biashara ndogo za pembeni kujaza kibaba. Wengi wanautambua umuhimu wa kutenga akiba kwa siku za usoni na ni la sita kwenye orodha ya mambo muhimu maishani.

Walio na umri ulio chini ya 30 wanatenga hela kwa madhumuni ya kupata mtaji wa kuanzisha biashara nao walio na umri mkubwa zaidi wanazipa kipaumbele juhudi za kuwahifadhia watoto wao karo ya shule.