1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Njaa ni tatizo la kisiasa

Ukweli ni kuwa duniani kuna chakula cha kutosha cha kumlisha kila mtu, lakini ubaya ni kwamba wanasiasa, hasa katika mataifa yanayoendelea, yameligeuza tatizo la njaa kuwa mtaji wao wa kisiasa.

Watoto wenye utapiamlo nchini Bangladesh.

Watoto wenye utapiamlo nchini Bangladesh.

Ulimwengu bila ya njaa unawezekana. Kuwalisha watu bilioni saba wakashiba ipasavyo ni jambo lisiloshindikana, maana dunia yetu inazalisha chakula cha kutosha. Kwa hakika, njaa si tatizo la kimaumbile au lililosababishwa na mizozo.

Njaa inavumiliwa tu na wanasiasa wakubwa, ambao wanaichukulia hali kama ilivyo kwa sababu kuna mengine muhimu zaidi kwao: kwa mfano, sauti za wanunuzi wa Kizungu na wamiliki wa mashamba makubwa.

Ingelikuwa hotuba za wanasiasa hawa kuhusu mshikamano ni za dhati, basi inabidi waondowe ruzuku wanazolipwa wakulima wa Ulaya, waufanyie mageuzi mfumo wa kibiashara na kupandisha bei za vyakula katika nchi za viwanda.

Lakini hali halisi hivyo ilivyo. Sauti za wenye njaa hazithaminiwi hata kidogo. Hawana wa kuwasemea. Njaa inakutikana kule hasa ambako, mazao ya chakula yanalimwa, yaani mashambani wanakaoishi wakulima wadogo wadogo.

Wanyonge hawana muombezi

Licha ya dunia kuwa na chakula cha kutosha, mamilioni wanakufa kwa njaa.

Licha ya dunia kuwa na chakula cha kutosha, mamilioni wanakufa kwa njaa.

Watu hao hawana wa kuwapigania katika taasisi kubwa kubwa za kiuchumi duniani. Makubaliano ya kiuchumi na kibiashara yanapozungumzwa, wao hawana sauti, ingawa wao wako wengi tu.

Bado mpaka sasa nusu ya wakaazi wa dunia wanategemea kwa njia moja au nyengine uzalishaji wa chakula. Idadi kubwa ya watu wanaoishi katika nchi zinazoinukia, ndio wanaobeba mzigo wa mfumo wetu wa kiuchumi. Watu bilioni moja kote ulimwenguni wanasumbuliwa na njaa au hawali vya kutosha.

Wanasiasa wa Ulaya daima wanajifanya wamezidiwa na kuuliza: "Tutawaelezaje wapiga kura wa Ulaya kama tunataka kubadilisha hali ya mambo kwa masilahi ya watu maskini?"

Hata hivyo si shida hata kidogo. Wapiga kura waelezwe kwamba kupambana na njaa inamaanisha pia kuhakikisha maslahi na neema yao. Kwa sababu Ulaya inataka kuepukana na kitisho cha kuingia wakimbizi milioni 150 wanaosemekana wataingia barani humu hadi ifikapo mwaka 2020 ili kukimbia njaa katika eneo la Afrika, kusini mwa jangwa la Sahara.

Wapiga kura waelezwe pia kwamba fedha za walipa kodi hazitupwi. Kwa kugharimia miradi ya maendeleo,watu wanataka kurekebisha kile kilichovurugika kutokana na sera zetu za kiuchumi na mfumo wetu wa kibiashara ulimwenguni.

Ulaya iambiwe kweli kuhusu njaa ya Afrika

Kitoto kikiwa kinakabiliwa na utapiamlo katika kambi ya wakimbizi wa Kisomali.

Kitoto kikiwa kinakabiliwa na utapiamlo katika kambi ya wakimbizi wa Kisomali.

Mengi yamekuwa yakiripotiwa kuhusu madhara ya njaa kwa binaadamu, lakini nani anazungumzia kuhusu wale wanaofaidika na njaa? Na hilo pia linahitaji kutamkwa wazi wazi.

Kuna wanaofaidika na hali hii: Kwanza ni sisi wanunuzi ambao tunatoa fedha haba kununua vyakula kuliko tulivyokuwa tukitoa miaka 20 iliyopita. Tunapenda kununua mkate kwa euro moja na maziwa kwa senti 70. Tunajidanganya chakula si lazma kiwe ghali. Miaka 100 iliyopita, thuluthi mbili ya mahitahji ya wanunuzi wa Ujerumani ilikuwa ikituwama katika chakula. Hii leo 20% tu ndizo zinazotumiwa kwa ajili ya chakula.

Wengine ni wakulima wa Ulaya wanaolima kupindukia mahitaji sokoni, tena bila ya kuhitaji kuingiwa na hofu. Si wanaahidiwa kulipwa ruzuku nono kufidia mazao yao pamoja na kujivunia uungaji mkono wa wanasiasa? Kwa wakulima wa nchi zinazoinukia hiyo ni ndoto tu.

Kuna wengine pia wanaofaidika: nayo ni makampuni makubwa makubwa ya shughuli za kilimo yanayoeneza mbegu zao katika masoko, ikiwa ni pamoja na bidhaa za kemikali. Pia watabiri katika masoko ya hisa ni miongoni mwa wanaofaidika na hali ya njaa.

Hebu tuache kujidanganya kuwa balaa la njaa linatokana kwa sehemu tu na vita na maafa ya kimaumbile. Hasha. Njaa kwa sehemu fulani ni matokeo ya sera za kuendelea kutengwa sehemu fulani ya wanaadamu, ambao mahitaji yao hayazingatiwi, na wanaowekwa kando na wale tuliowataja hapo awali.

Baada ya miongo ya hali ya kutegemea na unyonyaji wa wakoloni katika miaka ya '80, mataifa huru ya Afrika yalilazimishwa kutekeleza masharti yaliyowekwa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki Kuu ya Dunia, kuanzisha mfumo wa soko huru, kurekebisha muongozo wa kiuchumi na ubinafsishaji.

Sera hizo zikaingizwa katika nchi ambako hakuna miundo mbinu, hakuna wenye ujuzi, wala wawekezaji madhubuti wa kiuchumi. Madhara yake yalikuwa makubwa hasa upande wa kilimo, lakini pia kwa upande wa sekta ya elimu na ya afya.

Hata katika karne ya 21, jumuia ya kimataifa bado haijazindukana. Hilo ni kosa kubwa na sio tu la kimaadili. Tusidharau kishindo kinachoweza kuzushwa na watu maskini na wenye njaa. Mwaka 2008 kupanda bei za bidhaa kulisababisha maandamano dhidi ya njaa kuanzia Cameroon hadi kufikia Misri.

Miaka kumi ijayo, marekebisho na miradi ya misaada ya maendeleo itatugharimu mabilioni. Njaa inahatarisha utulivu wa kisiasa, kwanza katika maeneo husika na baadaye Ulaya.

Anayeelewa mafungamano yaliyoko, anabidi aelewe pia kwamba mageuzi ya kina ya kisiasa yanahitajika, na sio marekebisho, misaada ya dharura au ahadi zinazotolewa katika mikutano ya kilele na baadaye kusahauliwa.

Mwandishi: Ute Schaeffer
Tafsiri: Oummilkheir Hamidou
Mhariri: Mohammed Khelef

Viungo vya WWW