1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nishati mbadala yadhihirisha umuhimu wake.

Mohammed Abdul-Rahman26 Februari 2007

Makampuni makubwa sasa yatambua umuhimu wa kushughulikia hifadhi ya mazingira, kuinusuru dunia.

https://p.dw.com/p/CHlZ
Jinsi moshi wa viwanda unavyochangia kuharibu mazingira na kusababisha ongezeko la ujoto duniani.
Jinsi moshi wa viwanda unavyochangia kuharibu mazingira na kusababisha ongezeko la ujoto duniani.Picha: AP

Upepo unazidi kuchukua nafasi ya kuwa kitu kinachoweza kutumiwa kwa nishati mbadala, baada ya mwanzo mbaya mnamo miaka ya nyuma na kusababisha ushirikiano ulio tete kati ya makampuni makubwa na walinzi mazingira-huku wawekezaji wakichuma na kuzidi kunusa fedha. Hivi sasa kitisho kinachotokana na ongezeko la kuchafuliwa mazingira, kinazusha matumaini ya kwamba siku moja ndoto iliopuuzwa sasa inaweza kuwa kweli.

Wasi wasi huo pamoja na haja sasa ya kuanza kufikiria kwa makini shinikizo kubwa kwa ulimwengu juu ya ulinzi wa mazingira unatokana na kuzidi kwa mabadiliko ya hali ya hewa, ongezeko la uchumi wa China na suala la usalama wa nisahati duniani.

Katika miaka iliopita ya 1970 kwa mfano, zilikua ni bei za juu za mafuta zilizosababisha haja ya kusakwa njia nyengine za kutoa umeme, kama vile upepo na jua, jambo ambalo mara nyingi ndiyo zingatio la wasomi, wanaharakati wa ulinzi wa mazingira na jamii za vijijini.

Bei za mafuta zilipoanguka, haja ya kuzingatia nishati mbadala ikatoweka. Sasa bei zimepanda tena, lakini ni aina nyengine za matumizi ya nishati zilizowaamsha na kuwazindua wawekezaji, yakiwemo mabenki ya fedha, bima za malipo ya uzeeni na mifuko mengine ya fedha.

Mkurugenzi mtendaji wa taasisi ya utafiti wa nishati mpya-New Energy Finance- Michael Liebrich anasema “ kabla ya 2003 iliku ni hadithi ya wenye waadilifu na suti zao. Lakini hivi sasa yamegeuka ni suti tu au labda isemwe kuwa ni suti na maadili.” Makampuni makubwa yalikutana hivi karibuni katika chuo kikuu cha Columbia-Marekani na kutoa wito wa hatua za haraka kusaka suluhisho la kuongezeka kwa ujoto duniani kwa kupunguza viwango vya utoaji wa gesi zinazoharibu mazingira.

Suali linalojitokeza sasa ni jee lina utaanzishwa utaratibu maalum kutekeleza wajibu huo ? Jee kweli kuna ongezeko la ujoto duniani ? Ni binaadamu anayesababisha hali hiyo ? Jee waraka wa Kyoto utasainiwa kikamilifu na kweli teknolojia mbadala zitaweza kutoa changamoto katika utekelezaji wake ?

Viwanda na makampuni makubwa ambayo mwanzoni yalikua ni sehemu ya tatizo lililopo, sasa yamebadili msimamo na kuunga mkono mageuzi kutaka nishati mbadala kama ya upepo, jua, maji au nguvu za mawimbi pamoja na zile za aina ya mafuta ambayo hayataharibu mazingira, kama vile yanayotoa hewa chafu ya carbon dioxide.

Kwa hakika matumizi ya nishati za aina hiyo kwa jumla ni muhimu katika kukabiliaana na kurekebisha hali ya sasa.

Kihistoria makampuni na viwanda vikubwa duniani ndiyo waliokua maadui, lakini sasa hilo haliwezi kuendelea na mengi yameshatambua .

Hadi sasa tafauti za mtazamo kati ya walinzi mazingira na makampuni makubwa ya biashara ni pamoja na hali ya baadae ya nishati ya nuklea na njia za kuepukana na gesi ya carbon dioxide. Makampuni ya mafuta yanaelekea kuona kwamba mahitaji yataongezeka maradufu ifikapo 2050, wakati wanaharakati wanaopigania hifadhi ya mazingira duniani na baraza la nishati mbadala la ulaya wanataka mahitaji yapunguzwe.

Viwanda vya mafuta hunufaika kutokana na kuongezeka mahitaji ya nishati jambo ambalo litakua na maana ya kuendelea kutegemea mafuta yasio sababisha uharibu wa mazingira na wakati huo huo hali hiyo kuyafanya mataifa husika yafikie malengo yaliokubaliwa kulinda mazingira.

Chini ya zingatio la yote hayo pamoja na baadhi ya tafauti za mtazamo na mbinu ziliopo wakati huu, la msingi ni kuwa hata wanaochangia kwa wingi katika uharibifu wa mazingira, sasa wanaungama kwamba wakati umefika kuzuwia mtindo huo, ili kuiokoa sayari hii.