1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nini hatma ya Brexit?

Angela Mdungu
23 Oktoba 2019

Baada ya kushindwa kwa Waziri mkuu Boris Johnson kwa mara nyingine bungeni suala la Brexit linazidi kuwa gumu. Lakini mwandishi wa DW Bernd Riegert anasema ni hakika kuwa Uingereza haitojitoa Umoja wa Ulaya wiki ijayo

https://p.dw.com/p/3Rlkb
Großbritannien London | Boris Johnson will keine Brexit Verlängerung verhandeln
Picha: picture-alliance/dpa/PA Wire/House of Commons

Moja ya maswali yakujiuliza katika sakata la Brexit ni waziri mkuu wa Uingereza anaweza kukubali kushindwa mara ngapi? Bunge la Uingereza limeukataa mpango wa serikali wa kujadili kupitia bunge sheria zinazotekeleza makubaliano ya Brexit ndani ya siku tatu pekee. Matokeo yake, Boris Johnson aliachana na ombi lake la kuendelea na mpango wa Brexit.

Mivutano hii kati ya Waziri mkuu na wabunge inasababisha kushindwa kuwa na uwezekano wa kukamilisha makubaliano ya kujitoa na Umoja wa Ulaya kabla ya muda uliopangwa, Oktoba 31.

Kifungu cha sheria kinachomtaka Waziri mkuu Johnson kutoiruhusu Uingereza kujitoa kwenye umoja huo bila ya makubaliano kinachojulikana kama "Ben Act" kinatumika tena. Hii ikimaanisha tarehe iliyokuwa imepangwa kwa Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya si suala la mjadala tena. Kwa sasa, Umoja wa Ulaya hauna budi kuamua haraka juu ya ombi la waziri mkuu mtukutu lililotumwa mjini Brussels kwa umoja huo kupitia barua zisizo na sahihi Jumamosi iliyopita.

Kifungu hicho cha sheria cha "Ben Act" kinaitaka Uingereza kuomba muda wa miezi mitatu zaidi. Kuna mashaka kidogo iwapo Umoja wa Ulaya utaruhusu kuongezewa muda. Huenda wakatoa muda mfupi ama mrefu zaidi. Rais wa Baraza la Ulaya Donald Tusk na nchi 27 wanachama wa umoja huo kasoro Uingereza, wanalifikiria hilo.

Uamuzi unaweza kutolewa ndani ya siku kadhaa zijazo, ama labda katika mkutano wa kilele mjini Brussels. Johnson ameshatangaza kuwa hatohudhuria katika mashauriano. Hili si jambo rasmi wala lenye kuwa na umuhimu. Waziri mkuu huyu ambaye ameendelea kupatwa na mapigo bado anataka Uingereza ijitoe kwenye Umoja huo ifikapo Oktoba 31. Lakini huenda ni vizuri zaidi akaondoka madarakani na kutoa nafasi kwa mtu mwingine kurithi cheo chake.

Boris Johnson analenga uchaguzi

Wakati huohuo, Johnson analenga kuwa na uchaguzi mpya wa bunge ambalo kwa maoni yake halifai. Anataka kutambuliwa kama mteule anayelinda haki za watu.  Kulazimisha uchaguzi huu ambao una uwezekano wa kusababisha kupigwa kura ya maoni, kuwa mgumu ama kuufuta mchakato wa Brexit, chama cha Conservative kina njia mbili pekee.

England Brexit Parlamentssprecher John Bercow
Spika wa bunge la Uingereza John Bercow katika moja ya mijadala ya BrexitPicha: picture-alliance/empics/House of Commons

Ya kwanza ni kwa Johnson kuliomba bunge tarehe ya uchaguzi. Lakini hii itahitaji kupata theluthi mbili ya wabunge walio wengi jambo ambalo si rahisi.  Njia ya pili ni kujiuzulu ama anaweza kuondolewa madarakani kwa kura ya kutokuwa na imani naye. Baada ya hapo, Itakuwa ni lazima uchaguzi ufanyike iwapo Bunge la nchi hiyo lililo na mgawanyiko mkubwa halitakuwa na makubaliano juu ya mkuu mwingine wa serikali .

Hata hivyo kunazidi kuwa na mkanganyiko na ni wazi kwamba mchakato wa Uingereza kujitoa Umoja wa Ulaya utaahirishwa kwa muda huku hali ya sintofahamu ikiendelea kutawala kati ya Uingereza na umoja huo.

Mwandishi: Riegert, Bernd

Tafsiri: Angela Mdungu