Niersbach apigwa marufuku mwaka mmoja
25 Julai 2016Ni kutokana na kashfa ya kutolewa kwa kandarasi kwa Ujerumani kuyaandaa mashindano ya kombe la dunia ya mwaka 2006. Niersbach ni mwanachama wa Baraza la FIFA. Kamati ya maadili ya FIFA imesema Niersbach alishindwa kuripoti uchunguzi kuhusu masuala ya ukiukaji wa maadili katika utoaji wa kandarasi hiyo kwa Ujerumani ikiwemo uwezekano wa kukiukwa kwa kanuni za kimaadili.
Niersbach, makamu wa rais wa kamati iliyoandaa Kombe la Dunia 2006 na mwanachama wa sasa wa Baraza la FIFA na kamati kuu ya Shirikisho la Kandanda Ulaya – UEFA, alijiuzulu Novemba mwaka jana kutoka shirikisho la kandanda la Ujerumani.
Mkuu wa kamati ya maadili ya FIFA alianzisha uchunguzi mwezi Machi na mwezi uliopita akaikabidhi ripoti yake kwa jopo la kufanya maamuzi, ambalo sasa sasa limeamua kuendelea na mchakato rasmi wa kuamua kuhusu kesi ya Niersbach aliye na umri wa miaka 65. Kando na kupigwa marufuku kwa miaka miwili, jopo la uchunguzi pia limependekeza Niersbach atozwe faini ya euro 27,000
Lakini mara tu baada ya taarifa hiyo kutolewa, Niersbach alijibu kwa kusema kuwa atafanya kila liwezekanalo ili kupinga uwezekano wa kuchukuliwa adhabu hiyo. Alisema ni suali la heshima na kulinda haki zake za kibinafsi kutumia mbinu zote za kisheria kupinga hatua yoyote dhidi yake.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Sessanga Iddi