1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nicolas Sarkozy atimiza mwaka mmoja madarakani

Abdulrahman, Mohamed6 Mei 2008

Umaarufu wake washuka , huku wafaransa wengi wakikasirishwa ,kwa kushindwa kuinua hali zao za maisha na mtindo wake wa maisha.

https://p.dw.com/p/Duc2
Rais Sarkozy akifafanua jabo katika mkutano na waandishi habari.Picha: picture-alliance/ dpa

Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa leo ametimiza mwaka mmoja tangu alipochaguliwa kushika wadhifa huo. .Tarehe 6 Mei mwaka jana wakati Bw Sarkozy, wanasiasa wa mrengo wa kulia alipomshinda mpinzani wake kutoka chama cha kisoshalisti Bibi Segolene Royal, wafaransa na walimwengu walikua wakikodoa macho kwa shauku kuona kama atatekeleza ahadi yake ya kubadili Ufaransa au atakua sawa tu na mtangulizi wake na kuridhia shinikizo la maadamano ya upinzani mitaani dhidi ya hatua kali za mageuzi ya kiuchumi.

Wafaransa walivutiwa na heba yake katika miezi ya kwanza ya kuchukua madaraka ikipanda hadi 67 asili mia ya . Lakini muda si muda hali ya kuvunjwa moyo ikaanza kujitokeza.

Sarkozy akaachana na mkewe wa pili Cecilia mwezi Oktoba na hatua hiyo ikafuatwa na ndoa mpya na mrembo Carla Bruni. Hayo yakatoa hisia kwa wapiga kura kwamba kiongozi wao ameshughulika zaidi na matajiri na watu mashuhuri kuliko kusghulikia matatizo yanayowakabili. Hayo ni miongoni mwa yale yalimfanya Sarkozy mwenye umri wa miaka 53 kugeukiwa na waliomchagua na kuwa Rais asiyependeza machoni mwao kuwahi kushuhudiwa kwa miaka mingi.

Ahadi za Sarkozy kuimarisha uchumi zilishindwa na mwezi Januari mwaka huu akasema hakuweza kufanya kitu kwa sababu ,"hazina ya taifa ni tupu." Ripoti ya bunge, ilisema moja wapo ya mipango yake ya mageuzi, iliolenga katika kuimarisha pato kwa kuondoa kodi kwa maasaa nyongeza ya kazi, ni wa gharama kubwa na hautowi mafanikio yoyote.

Aidha rais huyo pia amekumbana na mkosi wa kuingia madarakani katika wakati ambao kulikua na msukosuko wa fedha duniani uliosababisha kupanda bei ya mafuta -kiwango cha juu kabis cha kihistoria kuwahi kushuhudiwa hapo kabla. Kutokana na hayo ughali wa maisha Ufaransa ukapanda hadi kiwango cha 3.2 asili mia-cha juu katika kipindi cha miaka 17 iliopita.

Baadhi ya wachambuzi wansema, hata hivyo Sarkozy ameonyesha nia ya kuleta mageuzi, isipokua kosa lilikua kutangaza miradi mingi kwa wakati mmoja na matokeo yake kuwa ni kushindwa kuitimiza yote kwa haraka.

Sambamba na hayo katika sera ya kigeni ambapo aliahidi kulipa kipa umbele suala la haki za binaadamu , Sarkozy anakosolewa kuwa ameweka masilahi ya kiuchumi mbele, badala ya haki za binaadamu, katika mahusiano ya Ufaransa na Urusi, China .Libya na makoloni ya zamani ya Ufaransa barani Afrika.

Aidha Chama chake UMP kilipata pigo katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwezi Machi. Wakati haiba ya Sarkozy inazidi kushuka, wasoshalsisti nao wamo katika mivutano ya ndani chamani na wanaelekea kuzingatia zaidi juu ya nani atakayekua kiongozi wao mpya , kuliko kuwasilisha sera mbadala ya zile za Sarkozy. Kutokana na hayo mchambuzi mmoja anasema pamoja na yote , kwa hivi sasa Sarkozy hana upinzani wa kweli. Uchaguzi mwengine nchini Ufaransa unatarajiwa 2012.