Nia ya ziara ya Steinmeier Mashariki ya Kati ni nzuri lakini matokeo ni kidogo | Matukio ya Kisiasa | DW | 08.05.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Nia ya ziara ya Steinmeier Mashariki ya Kati ni nzuri lakini matokeo ni kidogo

Ziara ya waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani, Frank Walter Steinemeir, katika Mashariki ya Kati imechukua siku sita. Leo hii waziri huyo anarejea mjini Berlin kushiriki kwenye mkutano kati ya mawaziri wa mambo ya kigeni wa nchi za Umoja wa Ulaya na baraza la ushirikiano la mataifa ya Ghuba. Je waziri Steinmeier amefaulu katika ziara yake ya Mashariki ya Kati?

Mazungumzo mengi, matokeo kidogo. Hivyo ndivyo inavyoweza kuelezwa ziara ya waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani, Frank Walter Steinemeier, katika Mashariki ya Kati. Kwa mara ya saba sasa Steinmeier amelitembelea eneo hilo, lakini ingawa kila anakokwenda anakaribishwa kama mwenyeji au rafiki, kiongozi huyo hajafaulu kurejea na ujumbe mpya mjini Berlin. Kwamba hatua mpya imefikiwa katika kuutanzua mzozo wa Mashariki ya Kati, bwana Steinmeier bado hajakaribia angalau mara moja kulifanikisha jambo hilo.

Kwa mara nyengine waziri Steinmeier alizungumza na rais wa mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas. Lakini rais Abbas ni sehemu ndogo tu ya Wapalestina wote na ushawishi wake una mipaka. Kwa majuma kadhaa sasa serikali ya umoja wa kitaifa ya mamlaka ya Palestina imekuwa katika umaskini. Waziri Steinmeier aliipa matumiani serikali hiyo wakati wa ziara yake aliyoifanya awali katika eneo hilo. Lakini tangu hapo hadi sasa kumekuwepo na mabadiliko machache.

Ili mradi wabunge wa chama cha Hamas hawataki kuitambua Israel, Ujerumani na pande zinazoudhamini mpango wa amani wa Mashariki ya Kati zikiwemo Marekani, Urusi , Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa, haziko tayari kufanya mazungmuzo na serikali ya Wapalestina.

Hali ya kimaisha ya Wapalestina inaendelea kuwa mbaya, wanamgambo wanaendelea kuvurumisha maroketi aina ya Kassam nchini Israel na mwanajeshi wa Israel, Koplo Gilad Shalit, bado anaendelea kuzuiliwa na wanamgambo katika Ukanda wa Gaza.

Waziri Steinmeier anajitahidi kuitoa Palestina kutoka kwa matatizo huku Marekani ikiendelea kuishinikiza na miito inayotarajiwa kuboresha usalama wa Israel na Palestina. Katika mtazamo mzima wa juhudi za kidiplomasia inaonekana harakati zote hazikupangwa vizuri wala hakuna ahadi nyingi za matumaini.

Hata nchini Israel waziri Steinmeier hakuweza kufanikisha lolote kwani alifanya ziara yake wakati serikali ya Israel ikikabiliwa na mgogoro mkubwa. Waziri mkuu wa Israel, Ehud Olmert, anashinikizwa ajiuzulu kufuatia ripoti ya uchunguzi wa vita vya Lebanon, iliyomkosoa vikali jinsi alivyoviendesha vita hivyo.

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Israel, Tzipi Livni, alimtaka Olmert ajiuzulu. Kwa hiyo ni wazi kwamba waziri mkuu Ehud Olmert kwa sasa ana mambo mengine muhimu yanayomtia wasiwasi kuliko mkutano wa kilele wa Mashariki ya Kati unaondaliwa na pande nne zinazoudhamini mpango wa amani wa eneo hilo.

Waziri Steinmeier alilazimika kurudia tena kwamba ipo haja ya kuzungumza na rais Abbas na hata viongozi wa mataifa ya kiarabu kuhusu hali ya kisiasa ndani ya Palestina, ili mradi serikali haitaendeleza uhasama dhidi ya Israel.

Steinmeier kwa upande wake alimualika mwenzake Tzipi Livni kuhudhuria mkutano wa mawaziri wa mashauri ya kigeni wa Umoja wa Ulaya, unaofanyika mda mfupi kabla Ujerumani kumaliza awamu yake kama mwenyekiti wa umoja huo. Mkutano mwingine, mazungumzo mengine, lakini kwa wakati huu mengi yanaonekana hayawezekani.

Bila shaka hakuna anayetarajia mengi kutoka kwa waziri Steinmeier katika juhudi zake za kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa Mashariki ya Kati. Lakini serikali ya Ujerumani ilijiwekea matarajio makubwa mno kwa kuahidi kutaka kuushughulikia kwa dhati mzozo wa Mashariki ya Kati wakati wa kuongoza Umoja wa Ulaya.

Ujerumani imeufufa mchakato wa amani wa Mashariki ya Kati na kuzitolea mwito pande zinazohasimiana kuwa tayari kufanya mazungumzo. Hiyo ilikuwa nia nzuri, lakini matokeo yake hayatoshi. Matumaini makubwa hayasaidii tena katika swala hili. Umoja wa Ulaya unaweza tu kuchukua jukumu dogo katika kuumaliza mzozo wa Mashariki ya Kati.

 • Tarehe 08.05.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHEi
 • Tarehe 08.05.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHEi

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com