1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

New Zealand yasitisha utafutaji miili

24 Desemba 2019

Polisi ya New Zealand imesema inasitisha harakati za kuitafuta miili ya watu wawili ambao bado hawajulikani walipo kutokana na mripuko mkubwa wa volcano mapema mwezi huu.

https://p.dw.com/p/3VHtc
Neuseeland Whakatane PK nach Vulkanausbruch auf White Island
Picha: AFP/M. Melville

Andy McGregor ni mkuu wa polisi na amesema kwamba familia za watu hao wawili zimefahamishwa kuhusiana na uamuzi huo wa kusitisha shughuli hizo.

"Polisi bado wanasalia tayari kujishughulisha endapo taarifa yoyote itaibuka kuhusiana na watu hao ambao hawajulikani walipo," alisema McGregor.

Mtu mmoja amefariki katika hospitali Auckland

Watu hao ambao wanakisiwa kwamba wamefariki dunia ni mtalii wa Australia aliyekuwa na umri wa miaka 17 Winona Langford na Hayden Marshall-Inman ambaye ni raia wa New Zealand aliyekuwa mwelekezi wa watalii. Miili yao inadhaniwa kusombwa na maji na kupelekwa baharini katika kisiwa hicho cha volcano ambacho hakiishi watu.

Neuseeland Whakatane nach Vulkanausbruch auf White Island
Ndugu na jamaa wakiliwazana kwa kukumbatiana baada ya tukio hilo la mripukoPicha: Reuters/J. Silva

Polisi hapo Jumatatu ilisema mtu mmoja aliyejeruhiwa katika mripuko huo amefariki katika hospitali moja ya mjini Auckland na kupelekea idadi ya waliofariki dunia kufikia watu 17.

Kulingana na Wizara ya Afya ya New Zealand, watu 13 ambao walijeruhiwa bado wanapokea matibabu katika hospitali nne nchini humo na wengine 13 wamehamishwa na kupelekwa Australia. Watu wawili wamekubaliwa kwenda nyumbani. Watu tisa kati ya wale wanaotibiwa New Zealand bado wako katika hali mahututi.

Kulikuwa na jumla ya watu 47 wengi wao wakiwa ni watalii kutoka Australia, wakati mripuko huo wa volcano ulipotokea Disemba 9 na kufikia sasa watu 25 bado wako hospitali. Wengi wao bado wako hali mahututi.

Huenda kukawa na mabadiliko sekta ya utalii NewZealand

Kulingana na mkuu wa polisi McGregor, uamuzi huo wa kusimamisha shughuli za utafutaji wa miili hiyo miwili wiki mbili baada ya mripuko huo kutokea unakuja baada ya juhudi za utafutaji wa hewani na ufuoni wa miili hiyo.

White Island Neuseeland Vulkaninsel
Kisiwa hicho cha volcano kisichoishi mtu New ZealandPicha: Reuters/J. Silva

Kumekuwa na ukosoaji kwamba watalii walikubaliwa kuelekea katika kisiwa hicho licha ya hatari ya volcano zinazoweza kuripuka. Jambo hilo limepelekea tetesi kwamba huenda kukawa na mabadiliko makubwa katika uongozi wa sekta a utalii ya New Zealand.

Waziri Mkuu wa New Zealand Jacinda Ardern amesema uchunguzi rasmi wa polisi na maafisa wa kuchunguza usalama wa kazi huenda ukachukua hadi mwaka mmoja na watakaopatikana na hatia huenda wakahukumiwa kama wahalifu na kufungwa kwa hadi miaka mitano jela.