1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

New York yatikiswa na mauaji ya polisi

22 Desemba 2014

Mji wa New York ulikumbwa na simanzi kufuatia mauaji ya maafisa wawili wa polisi yaliyofanywa na bwana mmoja ambaye aliwaambia wapita njia kuangalia alichokuwa anaenda kukifanya muda mfupi kabla ya mauaji hayo.

https://p.dw.com/p/1E8UE
New York zwei Polizisten erschossen 20.12.2014
Picha: Reuters/S. Keith

Maafisa hao wawili - Wenjian Liu mwenye umri wa miaka 32 na Rafael Ramos mwenye miaka 40 walipigwa risasi kupitia kioo cha gari lao la doria mchana kweupe siku ya Jumamosi katika mji wa Brooklyn, katika shambulio lililoutikisa mji mkubwa zaidi wa Marekani New York kuelekea siku ya Krismas. Polisi ilimtaja muuaji kuwa ni Ismaaiyl Brinsley mwenye umri wa miaka 28, ambaye alijiua pia kwa kujipiga risasi kichwani baada ya kutenda unyama huo.

Mauaji hayo katika mji ambao unashuhudia kiwango cha chini kabisaa cha mauaji katika kipindi cha miaka 20, yamezidi kuudhofisha uhusiano kati ya Meya wa New York Bill de Blasio na jeshi la polisi, ambalo linamlaumu kwa kushindwa kuwasaidia na kuonyesha huruma zaidi kwa waandamanaji, ambao wameingia mitaani hivi karibuni kupinga mauaji ya polisi dhidi ya Wamarekani wenye asili ya Afrika.

Mwanaume aliewauwa maafisa wa polisi na kisha kujiuwa mwenyewe,Ismaaiyl Brinsley.
Mwanaume aliewauwa maafisa wa polisi na kisha kujiuwa mwenyewe,Ismaaiyl Brinsley.Picha: picture-alliance/Zuma Press

Rais Obama alaani

"Sote tumenufaika na kitendo chao cha kishujaa na ndiyo maana viongozi wetu wa Kiislamu, viongozi wetu wa Kiyahudi, viongozi wetu wa Kibaptisti, viongozi wetu wa Kikatoliki, jamii yetu kwa ujumla iko hapa kama jamii moja, mji mmoja na hatutaki chochote kutugawa kuhusu namna gani tunawashukuru askari wetu wanapohakikisha usalama wetu kila siku," alisema Eric Adams, rais wa Manispaa ya Brooklyn alipotembelea kituo cha muda cha kumbukumbu ya maafisa hao.

Rais Barack Obama, alieko mapumzikoni mjini Honolulu, alimpigia simu Kamishna wa Polisi wa Philadephia Charles Ramsey jana kuelezea kughadhabishwa kwake na mauaji ya maafisa hao wa polisi, na kumtaka mwenyekiti huyo mwenza wa kikosi kazi alichokiunda kutathmini matendo ya polisi nchini Marekani kote, kutumia kikosi hicho kusambaza ujumbe wake kwamba vitendo kama hivyo dhidi ya Polisi vinapaswa kulaaniwa.

Rais wa chama cha maaskari wa doria Pat Lynch akizungumzia mauaji yao, ambapo alimlaumu meya wa New York Bill de Blasio na kusema damu yao iko kwenye mikono yake.
Rais wa chama cha maaskari wa doria Pat Lynch akizungumzia mauaji yao, ambapo alimlaumu meya wa New York Bill de Blasio na kusema damu yao iko kwenye mikono yake.Picha: Reuters/S. Keith

Mauaji ya kisasi

Brinslay alisema kwenye mtandao wake kuwa mauaji hayo yalikuwa ya kulipa kisasi kwa vifo vya Eric Garner mjini New York, na Michael Brown mjini Ferguson Missouri. Polisi ilisema bwana huyo alikuwa na rekodi ya uhalifu, chuki dhidi ya polisi na serikali, na alikuwa na historia ya ulemavu wa akili ambayo ilihusisha jaribio la kujinyonga mwaka mmoja nyuma.

Polisi nchini Marekani wamekosolewa kwa muda kutokana na mbinu zao, kufuatia kifo cha Eric Garner aliekabwa hadi kufa na afisa wa polisi mjini New York, na Michael Brown aliepigwa risasi mjini Ferguson, jimboni Missouri. Uamuzi wa baraza la wazee wa mahakama kukataa kuwafungulia mashtaka maafisa waliohusika katika vifo vya raia hao wenye asili ya Afrika ulisababisha maandamano makubwa mjini New York na maeneo mengine ya Marekani.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre,afpe,ape
Mhariri: Oummilkheir Hamidou