1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

NEW YORK : Mjumbe kwa Somalia ataka kusitishwa vita

27 Desemba 2006
https://p.dw.com/p/CCfy

Mjumbe mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia amelihimiza Baraza la Umoja wa Mataifa kutowa wito wa kusitishwa mapigano mara moja nchini Somalia venginevyo kuna hatari ya mzozo huo kuja kulihusisha eneo zima la Pembe ya Afrika.

Mwakilishi huyo maalum Francois Lonseny Fall alikuwa akizungumza kwenye kikao cha dharura cha nchi wanachama 15 wa baraza hilo.Fall ameonya kwamba kushindwa kufikiwa kwa suluhisho la kisiasa kati ya Uongozi wa Kiislam na vikosi vya serikali ya nchi hiyo inayoungwa na mkono na Ethiopia kunaweza kuwa na matokeo mabaya sana kwa eneo zima.

Ethiopia imesema hapo jana kwamba vikosi vyake viko njiani kuelekea Mogadishu ngome kuu ya Muungano wa Mahkama za Kiislam kufuatia mapigano ya wiki moja na kwamba wanaweza kuuteka mji huo katika kipindi cha masaa 24 hadi 48.

Wakati Marekani imedokeza kuunga mkono operesheni hiyo ya kijeshi ya Ethiopia kwa wasi wasi wake wa kiusalama kutokana na kuibuka kwa vikosi vya Kiislam katika nchi jirani yake Umoja wa Nchi Za Kiislam OIC umevitaka vikosi vya Ethiopia kuondoka Somalia mara moja kwa kusema kwamba mapigano hayo yanatishia kulikumba eneo zima la Pembe ya Afrika na kuhusisha mataifa mengine nje ya eneo hilo.

Repoti zisizothibitishwa zinasema watu 1,000 wameuwawa katika mapigano hayo na wengine 3,000 wamejeruhiwa.